Sunday, March 17, 2013

Majibu Yangu kwa Ibrabura - Sehemu ya 2



JE, BIBLIA NI KITABU KILICHOPOTOSHWA?

Yeremia 8:8 inasema kwamba: Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.


Waislamu walipoona maneno haya: “Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo,” kama kawaida, wakajua kuwa huu tayari ni ushahidi kwamba Biblia imetiwa maneno ya uongo, kwa hiyo si Neno la Mungu na haiwezi kuaminika.


Lakini mara zote ni lazima kwenda kwenye muktadha wa kila andiko au hoja ili kuona kama kweli hoja hizo zina nguvu ya kusimama.


Basi ili tuweze kufika kwenye Yeremia 8:8, tutaanzia nyuma zaidi kidogo. Hebu tuanzie kwenye Yeremia 7:1-11.


1)  Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,

2)  Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana.

3)  Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.

4)  Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.

5)  Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake;

6) kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe;

7)  ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.

8)  Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.

9)  Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;

10)  kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?

11)  Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.


Hapa tunaona mambo kadhaa ya msingi. Mwito mkuu kabisa wa Bwana ulikuwa si kuhukumu, bali alitaka watu wa Yuda wajirekebishe. Ndio maana kwenye mstari wa 3 anawaambia “Tengenezeni njia zenu.”

Hii ina maana kuwa njia zao zilikuwa zimepotoka kinyume na amri za Mungu. Na kwa nini njia zao zilipotoka? Mungu anatupa jibu kwenye mstari wa 4 na wa 8 – walikuwa wanatumainia au kuamini maneno ya uongo.

Maneno hayo ya uongo waliyoyaamini, yaliwafanya wasihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; wawaonee wageni, yatima na wajane; wamwage damu isiyo na hatia; wafuate miungu mingine, n.k.

Na licha ya kufanya mambo hayo, walikuwa wakijifariji na kujidanganya wakisema kwamba, “Hakuna shida. Sisi tunaishi mahali ambako kuna nyumba ya Mungu muumba mbingu na nchi. Hakuna watu wengine duniani wenye nyumba kama hii. Unadhani Mungu atakubali nyumba hii maalum namna hii iharibiwe? Hapana. Mungu atatulinda tu.”

Lakini Mungu akawaambia kupitia nabii Yeremia:


14)  basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.

15)  Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.

Walikuwa wanajiona ni watu maalum sana na wenye akili na hekima. Ndipo tunapoendelea kusoma, tunafika hadi sura ya 8. Bwana anasema:


7)  Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.

8)  Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.

9)  Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?


Maandiko haya yanafafanua sababu ya upotovu wao. Kumbe kulikuwa na manabii na walimu wa dini waliokuwa wakiwadanganya. Mambo haya yapo hata leo. Ukiwa hujui Neno la Mungu linasema nini, walimu wa uongo wanaopenda fedha, vyeo, umaarufu na mafanikio ya dunia hii watakudanganya tu. Wewe utakuwa unadhani uko kwenye njia ya uzima kumbe ulishatumbukia shimoni siku nyingi!

Watu hawa si tu kwamba walikuwa wanajigamba kutokana na kuwapo kwa nyumba ya Mungu (yaani hekalu la Sulemani), bali pia walijigamba kwa sababu wana torati – kitu ambacho hakikuwapo kwingineko duniani. Lakini sasa hawakujua inasema nini na hawakuifuata.

Tunasema hawakuifuata kwa sababu kwenye sura ya 7 hapo juu Mungu amefafanua waziwazi ule uongo waliokuwa wakiufuata, ambao bila shaka walifundishwa na hao manabii wa uongo.

Sasa, swali ni kwamba, ni wapi huko kwenye Biblia ambako maandiko yanawaagiza Wakristo wafanye mambo hayo yaliyokuwa yakifanywa na watu wa Yuda [yaani kutohukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; kuwaonea wageni, yatima na wajane; kumwaga damu isiyo na hatia; kuifuata miungu mingine, n.k.]?   

Kama Waislamu wataonyesha mahali popote panapotoa maagizo hayo ambayo Mungu alikuwa akiyalalamikia, ndipo hoja hii yao, kwamba Biblia ni kitabu kilichopotoshwa, itakuwa na ukweli. Vinginevyo huu ni upotoshaji mtupu ambao unawala wao wenyewe kwa kuwa unawazuia kumwamini Mwokozi pekee wa ulimwengu, Yesu Kristo. Biblia ni Neno la Mungu la kwelikweli.

Tafakari

Hoji mambo

Chunguza

Chukua hatua.

No comments:

Post a Comment