Kati ya watu
wanaowasumbua sana ndugu zetu Waislamu ni shujaa wa Bwana Yesu, Mtume Paulo. Na
hii haikuanza kwa Waislamu pekee, bali kuanzia kwa washika torati waliokuwako
wakati wake, yaani mafarisayo, wakuu wa makuhani, waandishi pamoja na Wayahudi
wa kawaida waliofuata dini ya Kiyahudi.
Waislamu wanaendeleza
tu ili roho ya upinzani dhidi ya Injili iokoayo ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Zifuatazo ni
baadhi ya sababu ambazo Waislamu wanasema zinawafanya wamkatae Mtume Paulo,
kama nilivyozitoa kwenye facebook kwenye post mojawapo ya ndugu mmoja wa
Kiislamu.
Wanasema:
MOJA: Eti
aliweka amri ya watu wasitahiriwe, ndio maana Wakristo wengi leo wana magovi
JIBU:
Tohara ni
suala la afya ya kawaida wala halina uhusiano na kwenda mbinguni. Yaani,
ukitaka kufanyiwa tohara, ni faida kwa mwili wako tu na wala sio kwa roho yako.
Kinachoenda mbinguni ni roho na wala sio mwili. Mwili uwe umetahiriwa au
haujatahiriwa, ukifa ni kuozea tu ardhini. Kwa hiyo, Mungu alilitumia hilo
suala la tohara kama ishara ya mambo
halisi ya rohoni, na sio ya mwilini:
(Kumb 10:16)
Basi, zitahirini govi za mioyo yenu,
wala msiwe na shingo ngumu.
(Kumb 30:6) BWANA, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao
wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote,
upate kuwa hai.
(Yer 4:4) Jitahirini kwa BWANA, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
MBILI: Eti
alikuwa gaidi wa kuwaua wanafunzi wa Yesu kisha akadai ni mtume wao ili azidi
kuwaua kifkra
JIBU
Hii ni hoja
kichekesho. Tangu lini mkawa na huruma na wanafunzi wa Yesu? Mnasemaje kuhusu
makundi yenye itikadi kali ambayo yanaua Wakristo duniani hivi leo, yanavunja
makanisa na kuwalazimisha kufuata miungu
yao? Je, nayo mnayalaani?
Paulo
alikuwa muuaji KABLA ya kumjua Kristo kama ambavyo SISI SOTE nasi tulikuwa
wenye dhambi kabla ya kumjua Kristo. Na Yesu anasema:
(Luk
5:31-32) wenye
afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye
haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.
Yesu anawaita
wenye dhambi ili Yeye ndiye awape mioyo mipya iliyojaa upendo, huruma na msaada
kwa wanadamu wengine. Yeye hakuja kumtafuta Paulo asiye na dhambi, maana hakuna
Paulo wa hivyo au mwanadamu yeyote wa hivyo.
Kama Paulo
alikuwa mwuaji, wa kulalamika alitakiwa awe Kristo Yesu mwenyewe na wala sio
wewe uliye na chuki na Paulo.
TATU: Eti ndiye aliyeleta ushoga duniani
JIBU
Huu ni uongo kutoka kwenye shimo la kuzimu. Paulo
anasema:
Au hamjui ya
kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati
hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, (1Kor
6:9)
Jipime mwenyewe kama usemayo ni mambo yanayoingia akilini
au la. Unayejidanganya ni wewe mwenyewe wala si mtu mwingine.
NNE : Eti ndiye aliyesema pombe ni dawa ya
magonjwa.
JIBU :
Huu ni uongo kutoka kwenye shimo la kuzimu. Alichosema Paulo ni kwamba
unaweza kutumia mvinyo kidogo kwa ajili
ya tumbo.
Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa
yakupatayo mara kwa mara. (1Ti 5:23)
Wala hapa Paulo
haongelei kunywa kimpumu, mbege, kangara, komoni na safari kama kiburudisho au
kukata kiu. Anasema, ‘Mvinyo kidogo!
Na mvinyo huo kidogo ni kwa kusudi maalum – kwa ajili ya magonjwa
ya tumbo.
Maana yake
ni kuwa, kama huumwi na unataka tu huo mvinyo, wewe ni mlevi tu wa pombe. Shauku
yako si kupona ugonjwa bali kunywa pombe. Na zaidi ya hapo, kwa dunia ya leo
dawa za magonjwa ya tumbo ziko tele.
Ni Paulo huyohuyo ambaye anasema katika Waefeso 5 :18 --- Tena msilewe
kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho.
TANO : Eti ndiye aliyesema; Mungu
haangalii mwili bali roho. Ndio maana leo Wakristo wanatembea nusu uchi tena
mpaka wakienda makanisani.
JIBU
Kwanza, sio
Paulo tu anayesisitiza juu ya roho
kwanza mwili baadaye. Yesu mwenyewe anasema:
Ole wenu waandishi na mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa
mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na
kutokuwa na kiasi.
Ewe farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.” (Mat 23:23-27).
Ewe farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.” (Mat 23:23-27).
Pili, sio kweli kwamba Paulo au Yesu au Biblia
inakubaliana na watu kuwa uchi.
Paulo anasema : Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu
yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu. (1 Kor
8:13). Maana yake ni kuwa, jambo linalokwaza wengine na kuwatendesha dhambi, ukilitenda,
hukumu iko juu yako ; hata kama jambo lenyewe lingekuwa ni jema kama kula
chakula, sembuse kukaa au kutembea uchi!!
Je, hujui kuwa Paulo huyohuyo ndiye anayesema haya?
Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya
kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala
kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani (1 Tim 2:9)
Yesu anasema : Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya
mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake
mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! (Mathayo 18:7)
SITA : Eti ndiye aliyesema watu
wasalimiane kwa kupigana busu tena akaliita ni takatifu.
JIBU
Mtu akiwa na chuki na wewe,
chochote utakachofanya atatafuta neno linalobeza ufanyacho. Kwa hiyo, suala sio
ubaya wa tendo bali ni chuki iliyo moyoni mwake.
Je, kwani hujui tofauti kati ya
jambo takatifu na jambo lisilo takatifu? Nikikwambie, “Uwe unakunywa maji safi”
ubaya wangu uko wapi? Huoni kuwa hapa ninakuambia, “Usinywe maji machafu”?
Paulo anasema watu wasalimiane
kwa busu takatifu. Sasa kama busu ni takatifu, wewe mwenzetu unapata shida
gani?
SABA: Eti
ndiye pekee aliyesema kila chakula ni halali.
JIBU
Si Paulo pekee aliyesema hivyo. Hata Yesu alisema:
Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita
tumboni, kikatupwa chooni? Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo
vimtiavyo mtu unajisi. Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi,
uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu
unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi. (Mat 15:15-20)
Kila watu hapa duniani wana utamaduni na vitu
wanavyokula WAO. Wanaokula mbwa, acha wale. Wewe kama huwezi, usianze
kuwahukumu. Wanaokula nyoka, acha wale; chura, konokono, nk. Kama utamaduni wao
unawaruhusu kula vitu hivyo, acha wale. Hata wewe unayekula keki, kila
kiingiacho tumboni, hakiendi rohoni bali
mwisho wake ni chooni!
NANE : Eti ndiye aliyeleta dini mseto ya ukristo duniani.
JIBU
Sisi tunamfuata
Kristo Yesu kama ambavyo Paulo naye alimfuata Kristo Yesu. Je, wewe unamjua Paulo
kuliko Petro ambaye aliishi naye kwenye nyakati zilezile ; alikutana naye
uso kwa uso na aliyapima mafundisho yake?
Petro anasema :
Nanyi uhesabuni
uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama
vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile
kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika
nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio
na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine,
kwa uvunjifu wao wenyewe. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni
nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha
uthibitifu wenu. (2 Petro 3:15-17)
Kama mtu ataamua
kukusikiliza wewe mpinzani wa Paulo aache kumsikiliza Mtume Petro hiyo ni juu
yake na roho yake. Lakini sisi hatutaacha kusikiliza watumishi waaminifu wa
Yesu Kristo tukae kusikiliza chuki zako wewe zisizo na msingi wa kweli ya Mungu.
TISA : Eti ndiye pekee aliyedai Yesu ni Mungu
Mkuu hali ya kuwa Yesu alikana hilo.
JIBU
Je, Paulo
aliandika kitabu cha Isaya?----Maana kwa
ajili yetu MTOTO amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme
utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU MWENYE
NGUVU, BABA WA MILELE, Mfalme wa amani. (Isaya 9:6)
Je, Paulo
aliandika Injili ya Yohana? ---- Hapo
mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. (Yoh 1:1)
KUMI: Eti
ndiye pekee aliyekuja kuleta injili kwa
mataifa wakati ni kwa ajili ya Waisraeli pekee.
JIBU
Tangu karne
na karne huko nyuma, Mungu wa Israeli alishasema haya :
Msikie Yesu
mwenyewe anachosema: ---- Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,
mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19)
Maana Mungu
hakumtuma Mwana ulimwenguni ili
auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe
katika yeye. (Yohana 3:17).
Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. (Yohana 12:47).
Nami nautoa
uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na
kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta;
sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako
kundi moja na mchungaji mmoja. (Yohana 10:15-16).
Tena habari
njema ya ufalme itahubiriwa katika
ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho
utakapokuja. (Mat 24:14).
KUMI NA MOJA : Eti ndiye pekee aliyekuja
kuitukana torati kwa kuiita ni laana.
JIBU
Torati sio laana,
bali torati ni amri ambazo kwa kuwa wewe
mwanadamu hauna uwezo wa kuzitimiza zote, unaishia kubeba laana. Sheria
ikisema USIIBE maana yake kuiba ni kitendo
kinacholeta laana kwa mwibaji sio lile neno lenyewe la sheria. Unapoiba, unayelaanika
ni wewe kibaka na sio sheria iliyosema usiibe!!
Sasa msikie Paulo mwenyewe asemavyo juu ya torati:
Basi torati ni takatifu,
na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa
mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa (Warumi
7:12-13).
Habari ya kusema Paulo
kaita torati kuwa ni laana ni uongo, uzushi na upotoshaji wa maandiko.
KUMI NA
MBILI : Eti Paulo ndiye aliyekuja kuitangua
torati na kudai kuwa sasa torati isitumike tena. Kumbuka Yesu Alisema: Kwa
maana, amin, nawaambia , Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala
nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie. (Mat 5:18)
JIBU
Nikikwambia kosa hili hautasamehewa hata utakapolipa
senti ya mwisho, je, maana yake kosa hilo ni la milele au lina mwisho?
Haihitaji ujuzi
wowote mkubwa kubaini kuwa maana ya maneno hayo ni kuwa kosa hilo lina mwisho.
Na mwisho wake ni pale utakapolipa kikamilifu kile unachodaiwa.
Hicho ndicho Yesu anachosema katika aya hiyo.
Kila neno kwenye torati halitatanguka
hata yote yatimie. Maana yake ni kuwa andiko
litafikia mwisho pale tu litakapotimia. Kwa mfano, torati ilisema kuwa Yesu
atazaliwa.
Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu
mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala
Atakayewachunga watu wangu Israeli. (Mathayo 2:6)
Sasa kama wewe hadi leo bado unashikilia
ATATOKA, ATATOKA, ATATOKA kisa tu eti imeandikwa yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka basi ujue kuwa umekula hasara. Andiko hilo LILISHATIMIA.
Lakini kwa mantiki ya wale ndugu zangu Waislamu
wanaopindisha maandiko ya Biblia, ukiwaambia Yesu alishazaliwa, bila shaka kulingana
na Mat 5:18 watasema, hapana. Yesu alisema neno HALITANGUKI, kwa hiyo bado liko
vilevile.
…………………..
UTADANGANYWA
HADI LINI?
UTAKUMBATIA
UANGAMIVU HADI LINI?
Chuki humfanya mtu atiwe giza la moyo hata asiweze kuona
mbele yake. Halafu huanza kuzusha uongo dhidi ya wengine, kisha akauamini yeye
mwenyewe ili kujipa namna fulani ya amani ya uongo kwamba yuko sahihi.
………………………..
Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, kusikia
mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. (Mat 13:14)
barikiwa sana
ReplyDeleteAmen Gerald. Ubarikiwe nawe pia
Delete