Naeem alikuwa ni Mwislamu tangu
utoto wake. Ulifika wakati ambapo alikutana na Yesu Kristo. Matokeo yake,
aliweza kuyajua makusudi ya kuumbwa kwake. Na sasa anamshangilia Mwokozi na
Muumba wake ampendaye, yaani Yesu Kristo. Je, ilikuwaje? Tafadhali soma
ushuhuda wake ufuatao:
********************
Nilikua nikiwa Mwislamu.
Nilikulia Mashariki ya Kati. Tulikuwa tukienda kuswali, hasa Ijumaa. Nakumbuka
tulikuwa tukiswali swala tano kwa siku. Kila kitu tulichofanya kilihusiana na
imani yetu.
Na ninakumbuka kukulia
kwenye utamaduni huo, huku shauku yangu ikiwa ni kutaka kuwa na uhusiano na
Mungu nikijua kuwa hii ndiyo dini na Allah ni Mungu na Muhammad ni mtume wake;
na njia ya kufika kwa Allah ni kufuata mafundisho ya Uislamu, na maneno ya
Muhammad, yaani Hadith.
Wakati nikikua, nilikuwa
nawafahamu Wahindu, Masingasinga, hata Wakristo, Wakatoliki. Nina marafiki wa
karibu ambao walikuwa Wahindu. Hivyo, huwa tunazungumza kuhusu dini. Lakini
akilini mwangu, nilijua kuwa, kwa kuwa nilizaliwa na kukulia katika Uislamu,
basi ningebakia tu Mwislamu.
Nilishasikia juu ya Yesu
na injili; juu ya yale aliyotenda, lakini halikuwa ni jambo linalonivuta kwa
sababu wakati ule, Uislamu kwangu haukuwa tu ni dini bali ni namna fulani ya
utaifa. Hivyo, moyoni mwangu ingekuwa ni kama kichekesho kubadili utaifa wangu!
Pamoja na kwamba kulikuwa
na mambo kadha wa kadha ambayo sikukubaliana nayo (kuhusu Uislamu), ukweli ni
kwamba, Uislamu haukubali mtu kuwa na maswali na mashaka juu ya imani.
Kaka yangu alikuwa chuoni.
Kwa hiyo alipokuwa akija wakati wa likizo, alianza kuongea kuhusu Ukristo.
Alileta Biblia nyumbani. Tulianza kuwa na mijadala. Na wengi wa marafiki zake
walikuwa wameokoka; wana uhusiano binafsi na Yesu. Walianza kuzungumza nami juu
ya hayo. Nilikuwa napinga sana na sikutilia maanani.
Wakati hayo yakiendelea,
nilikuwa nikienda na kaka yangu kwenye mikutano ya kila wiki. Niliona sinema
kuhusu unyakuo wa kanisa ambayo ilinigusa sana. Na usiku ulipofika, walifunga
kipindi kwa sala.
Nilikuwa nimekaa nyuma,
labda kwa ujinga, au ujasiri au kiburi, nikasema, “Sijui kama wewe ni wa kweli.
Siamini upuuzi huu. Lakini kama wewe ni wa kweli, njoo ujionyeshe kwangu.” Hiyo
ndiyo iliyokuwa sala yangu.
Siku kadhaa baadaye
nilikuwa niko chumbani kwangu kwenye saa tano hivi, nikiwa nimemaliza kusoma
riwaya yangu, nikaweka kitabu chini, nikajinyoosha. Nikagundua kuwa chumba
kilianza kuwa na giza. Si giza hasa lakini kilikuwa kinajaa namna fulani ya
uovu. Nikawa nawaza, ni kitu gani kinaendelea hapa?
Wakati nikiwaza haya, kitu
kilinishika begani na kunivutia kwenye mto kitandani. Kisha mwili wangu ulianza
kuwa na mwitikio. Halafu mlango ukafunguliwa na mimi nikawaza labda ni kaka
yangu.
Lakini badala yake
kiliingia kiumbe ambacho baadaye nilikuja kujua kuwa alikuwa ni pepo. Alipokuwa
akija kitandani kwangu, akawa anasema kuwa ataniua. Nikaamini kabisa kuwa
akinifikia, ataniua.
Hapohapo nikawaza kuwa
Allah ni Mungu wa Uislamu, je, anaweza kunisaidia? Kwa namna fualani, nikajua
moyoni mwangu kuwa hili ni jambo ambalo haliwezi. Hivyo, nikawaza, je, Yesu
anaweza kunisaidia?
Wakati nikiwaza haya, huyo
pepo akawa anaendelea kuja kitandani kwangu. Alifika kitandani kwangu, kisha
akatoweka; sikumuona tena.
Kile ambacho kilikuwa
kimenishikilia pale kitandani nacho kikaniachia. Nikaweza kuamka tena. Nikainuka
kitandani kwangu na kukimbia nje ya chumba na kwenda kumwamsha kaka yangu.
Nikamweleza kilichotokea.
Akasema, “Je, ulikuwa ukiota?”
Nikasema, “Hapana.
Yalikuwa ni maono halisi kabisa!” Nakumbuka nilimwambia, “Hata mabega yangu
bado yanauma kutokana na kushikiliwa.”
Alianza kuzungumza na mimi
juu ya jambo lile nami nikasema, “Ni sawa lakini ninaogopa. Nisaidie. Naamini
hili jitu litaniua!”
Akasema, “Kuna mtu mmoja
tu ambaye ana mamlaka juu ya mapepo.”
Nikasema, “Nani huyo?”
Akaniambia, “Ni Yesu.”
Nikasema, “Sawa.”
Usiku ule tuliomba pamoja na
sala yangu ilikuwa, “Yesu mimi sikujui wewe ni nani. Sijui kama nikuite Bwana;
lakini nahitaji msaada wako. Na nimeambiwa kuwa wewe tu ndio unaweza kuniokoa
kwenye jambo hili. Kwa hiyo, nakupa maisha yangu.”
Kaka yangu aliniombea na
nikajisikia vizuri lakini si vizuri kabisakabisa. Akasema, “Basi, tutaonana
asubuhi.”
Nikasema, “Mimi siondoki,
nalala humuhumu!”
Akasema, “Hapana. Nenda tu
chumbani kwako. Inabidi umwamini Yesu na uende chumbani kwako.”
Kwa hiyo, nilienda
chumbani kwangu, nikawasha taa zote, nikatoa Biblia ambayo kaka yangu
alinipatia. Nikawa nasoma kitabu cha Yohana.
Ghafla, mwili wangu
ukaanza kutetemeka. Nikasema, “Mungu wangu, amerudi tena!”
Nikajikuta hapo kitandani
kwangu ninaangalia kwenye kona mojawapo ya chumba changu. Kukawa kuna nuru na
nikawa nahisi uwepo ambao naamini ulikuwa ni uwepo wa Kristo. Na ninakumbuka
nikiwa naangalia kwenye hiyo kona ya chumba, ilikuwa ni jambo la ajabu kwangu
kwa sababu kulikuwa na amani kubwa sana kiasi kwamba ilijaza kabisa moyo wangu
na kufunika kabisa mawazo na hisia zangu zote za hofu zilizokuwapo mwanzoni.
Sidhani kama nimewahi kuwa na amani kama hiyo tena.
Nakumbuka nikawa naangalia
tu. Kilichotokea, ile hali ikanilaza usingizi, na kama sikosei nilisema, ‘Safi
sana (cool)’ – kitu cha namna hiyo.
Baada ya usiku ule,
sikujua nifanye nini. Nilijua kuwa nimekutana na Kristo. Nakumbuka nilikuwa na
mazungumzo na kaka yangu kuhusiana na wokovu; kuhusiana na kumwamini, kumkubali
na kumkiri Yesu.
Nakumbuka hata wakati
nilipokuwa nikiangalia TV, waliposema tuombe hiyo sala, nilikuwa nikiomba tena
na tena. Nadhani niliiomba hata mara kumi!
Maisha yangu yalibadilika;
hata mawazo yangu yamekuwa tofauti sasa. Mtazamo wangu kuhusiana na Mungu
ulibadilika kabisa. Zamani, kwenye Uislamu, Mungu alikuwa mbali sana lakini
sasa yuko karibu. Kwa Waislamu, hata ukimwuliza sasa, je, unakwenda mbinguni? Atakwambia
kuwa hajui. Wanasema tu, inshallah, yaani Mungu akipenda. Lakini sasa ni
tofauti. Ninajua kuwa ninao uhakika kwa imani.
Mwanzoni nilikuwa
nikiwaza, labda ukifanya matendo fulani kwa kiwango fulani, basi unakuwa karibu
zaidi na Mungu. Sasa hivi sihitaji kufanya hivyo. Matendo hayanifanyi kuwa
karibu na Mungu. Ukaribu wangu na Mungu na upendo wangu na Mungu unaweza kukua.
Lakini Yeye tayari yuko karibu kabisa nami.
Nadhani watu wanapenda mtu
mwingine awafahamu kwa ukaribu kabisa. Ni jambo jema sana kujua kuwa Mungu
anatufahamu kwa undani sana na anatupa makusudi ya maisha. Nadhani jambo kubwa
kabisa kwangu ni kwamba, tangu nilipokutana na Kristo, nimeshajua makusudi ya
mimi kuumbwa. Najua kuwa makusudi hayo ni kuwafanya watu wengi iwekenavyo
wakutane na upendo alio nao.
Tafakari
Hoji mambo
Chukua hatua.
No comments:
Post a Comment