Khalida ni mwanamke
aliyekuwa Mwislamu, lakini baada ya kukutana na Bwana Yesu na kutembelea
mbinguni, kila kitu kilibadilika kwake. Je, ni kitu gani kilitokea maishani
mwake hadi kufikia kupelekwa mbinguni na Bwana Yesu? Tafadhali soma au sikiliza
ushuhuda huu wa kweli wenye nguvu ambao utakuonyesha upendo, uweza, mamlaka na
nguvu za Bwana Yesu, ambavyo vyote viko kwa ajili yako pia. Khalida anafanyiwa
mahojiano na Sid Roth.
Sid
Roth:
Khalida ni Mwarabu kutoka
Palestina. Na sijawahi kusikia … sijui uliwezaje kupona, Khalida! Na una
tabasamu usoni mwako … Ngoja niwaeleze kidogo kuhusu Khalida. Alipokuwa na umri
wa siku 11, mama yake alikufa na baba yake alimtelekeza. Kisha alipelekwa
kwenye nyumba ya mayatima. Alikaa humo hadi alipofikia umri wa miaka 9. Siku moja
alitoka kwenda kutafuta maji ya kunywa, na bomu lililipuka kwenye hiyo nyumba
na ile familia yake mpya iliteketea yote! Baada ya hapo watu hawakujua wampeleke
wapi. Matokeo yake aliuzwa kama mtumwa. Huko utumwani alikuwa akipigwa na
chakula alichopewa ni makombo tu.
Hatimaye askari walimwokoa
na kumpeleka kwenye nyumba nyingine ya mayatima. Baadaye walimpata baba yake
mzazi lakini alimkataa tena. Ni kukataliwa, kukataliwa, kukataliwa!
Kisha baba yake alimfanya
mtumwa na Khalida alipofikisha miaka 15, alimwoza kwa nguvu. Baada ya kukaa na
huyo mumewe na kuzaa mtoto, alipewa talaka na kufukuzwa. Kwa kuwa baba yake
alikuwa bado hamtaki, alimwoza kwa nguvu kwa mume mwingine tena!
Khalida na mumewe
mpya walienda Marekani. Lakini mume huyu alikuwa akimpiga hadi akamvunja taya! Kwa
nini alifanya hivyo?
Khalida:
Alikuwa ni mtu
mwenye hasira sana. Na katika Uislamu wanaume huwa wanafundishwa kuwa
wanatakiwa kuwarekebisha wake zao. Kwa hiyo, alikuwa ananifundisha njia njema
na alifanya hivyo hadi akanivunja taya. Hata hivyo sikujifunza chochote
(kicheko).
Sid Roth:
Kwa hiyo, una
watoto watatu na umeolewa kwa mume katili tena. Sielewi kabisa! Uliwezaje
kuvumilia hayo yote? Si tu kwa mume huyo, lakini maisha yako yote! Uliwezaje?
Khalida:
Nilikuwa nikichukia
sana. Kabla sijamjua Bwana nilikuwa nikighadhibika sana. Lakini ni kwa neema ya
Bwana.
Sid Roth:
Halafu mambo yakawa
mabaya zaidi. Alimwambia kuwa atamuua. Ulifanya nini kuhusiana na hilo?
Khalida:
Ilinibidi kukimbia
kuponya maisha yangu.
Sid Roth:
Ulisikia sauti.
Khalida:
Nilisikia sauti. Kabla
ya kusikia sauti ile, nilijaribu kujiua. Kisha nilisikia sauti ikisema kwa
Kiarabu, “Ondoka gizani na uende kwenye nuru. Japo nilikuwa na hali mbaya
niliamua kutii sauti ile maana niliona sina cha kupoteza.
Sid Roth:
Lakini angefanya
nini mwanamke ambaye hazungumzi Kiingereza, hana fedha na ana watoto wadogo
watatu akizunguka nao mitaani? Nini kilitokea?
Khalida:
Nilikutana na mama mmoja
wa Kikristo ambaye alinichukua kama binti yake na akanieleza juu ya upendo wa
Yesu.
Sid Roth:
Lakini wewe ulikuwa
unaupenda Uislamu! Uliupenda sana Uislamu.
Khalida: Niliupenda …
Sid Roth:
Ulimpenda huyu mama
kwa kile alichokutendea lakini hukumtaka Yesu wake.
Khalida:
Kweli kabisa. Tatizo
langu siku zote lilikuwa kwamba, nawezaje kuamini kwamba Mungu ana mtoto; maana
walitufundisha kwenye Uislamu kwamba Mungu hawezi kuwa dhaifu na kuwa na mtoto –
hiyo ni ishara ya udhaifu. Kwa hiyo nilikuwa ninashindana na hilo. Nilitamani kuwa
na upendo ule aliokuwa nao mwanamke yule; na huo ndio ukawa mwanzo wa
kubadilika kwangu. Niliona furaha yake, niliona upendo wake, niliona maisha
yake; na alikuwa kila wakati ameunganika na Mungu. Na nilikuwa nina kiu ya kuwa
kama yeye.
Sid Roth:
Kisha uliamua kuwa
huu ndio wakati ambao ninataka kuijua kweli. Hebu nieleze kile kilichotokea.
Khalida:
Nakumbuka nilikuwa
nimeshachoshwa na kuwa katika hali ya kuchoka. Na ninakumbuka niliomba
nikimwambia Yesu, “Kama wewe uko vile ambavyo watu wanasema kuwa wewe ni Mwana
wa Mungu, basi nionyeshe. Uje kwangu na unionyeshe kuwa wewe ni Mwana wa Mungu!”
Na sikutarajia kuwa kuna lolote lingetokea baada ya sala yangu ile. Lakini matokeo
ya sala yangu ile rahisi yalikuwa ni kwamba, Yesu alinitokea na nikakutana na
Bwana!
Sid Roth:
Hilo tu lingetosha.
Lakini alienda hadi mbinguni. Je, uliona nini kule mbinguni?
Khalida:
Niliona kuabudu. Niliona
jinsi ambavyo mbinguni wanamsujudia sana Yesu kama Mwana wa Mungu. Wanamwinua kama
Mfalme. Baadhi ya mambo niliyoona – watoto, watu, viumbe, walikuwa wakitupa
taji zao miguuni mwa Yesu. Alikuwa ana nguvu na mwenye utukufu.
Sid Roth:
Lakini haukujua
kuwa mambo hayo yameandikwa kwenye Biblia?
Khalida:
Sikujua. Nilikuwa sijawahi
hata kusoma Biblia kabla ya kukutana na mambo hayo. Nilichojua tu ni kwamba
mambo yale yalikuwa halisi sababu yalikuwa wazi sana. Na nilikuwa sehemu ya
mbingu; mambo yalikuwa halisi sana kiasi kwamba huwezi kuyapinga. Jambo moja
mbinguni ni kuwa Yesu ni Neno la Mungu. Na kadiri unavyomtazama usoni, na uzima
wake, na utukufu wake, ufunuo unakuwa wazi sana na halisi sana kiasi kwamba
huwezi kuukwepa!
Sid Roth:
Na
kinachonifurahisha ni kuwa (Khalida) sasa anaombea watu na wanapata miujiza – watu
wenye kansa, wanapona! Lakini kinachonifurahisha hata zaidi ni baadhi ya ufunuo
ambao aliupata kuhusiana na kuabudu. Na yeye humwabudu sana Mungu kuliko
ulivyowahi kuona – kama unavyoenda kuona maana hata wewe unaenda kuwa mtu
anayemwabudu Mungu.
Nikuombe Khalida umwabudu
Mungu kama ambavyo huwa unafanya nyumbani kwako; ambako hakuna mtu mwingine ila
Mungu tu.
Ninyi mlio hapa na
ninyi mnaotazama, napenda mmwabudu Mungu. Kama mkifanya hivi, Mungu
atajidhihirisha. (Khalida) hebu mwabudu Mungu.
Khalida:
Ndiyo. Napenda kuwatazama
watu usoni na kuwaambia kuwa kuna nguvu pale unapozungumza kwa lugha ya
mbinguni. Kwa kuwa tumeumbwa ili kumwabudu Mungu, tunapoingia kwa imani, ni
lazima aonekane na Biblia inasema kuwa kutakuwa na uwepo wake.
Sid Roth:
Sasa hivi, kama
unavyokuwa nyumbani, hebu mwabudu Mungu.
Khalida:
[anaanza
kuomba kwa lugha ya mbinguni – Tazama 1 Wakorintho 14:2]. Ninapenda nitafsiri
kile ambacho nilikuwa ninaomba. Nilichohisi kwenye roho yangu ni kumwinua Yesu
juu ya kila kitu – juu ya hali yako, juu ya talaka yako, juu ya mashindano
yako, juu ya ugonjwa wako, juu ya kila kitu unachopambana nacho kila siku. Unamwinua
Mfalme wa wafalme juu ya hali yako na unakuwa kama Hajiri alivyokutana na Mungu
na watu wengine kwenye Biblia. Kama sisi Waislamu tunapomwinua Yesu, tunakuwa
waabudu wa kweli wa Mungu na tunakuwa wa kweli kwa Roho wa Mungu na hiyo ni silaha
ya vita. Na kamwe hutashindwa katika mapambano yoyote kama ukimwabudu Mungu
katika roho na kweli!
****************
Ndugu msomaji,
umemsikia Khalida. Yesu Kristo ni halisi; na kila kitu ambacho Biblia inakisema
kuhusiana na Yeye ni kweli, kweli, kweli tupu!
Tafakari.
Jiulize.
Hoji mambo.
Chukua hatua!
''Na wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule, msisadiki;''
ReplyDeleteHaya, ni maneno ya yesu mwenyewe. Huyo mwanamke, kapagawa. Hajui alitendalo. Halafu, wakristo walioingia kwenye uislaam hawana hesabu.
Hivi wewe ndugu yangu, kwa nini haushangai? Maana, karibu mataifa yote yanayoizunguka israel ni ya kiislam!
Ibra rafiki yangu, waliopagawa hawako hivyo. Tazama hapa utaona mfano wa aliyepagawa: http://ajmacdonaldjr.wordpress.com/2012/05/28/demonic-activity-in-the-modern-world/
DeleteKuhusu watu kuingia kwenye uislamu, hilo sishangai hata kidogo. Watu wataendelea kuingia na kutoka kila mahali. Kuingia au kutoka si jambo la muhimu sana; cha muhimu umeingia wapi na mwisho wako ni nini? Yeyote anayetoka kwa Yesu na kwenda kuingia kwa mwingine anapotea HAKIKA. Mbingu ni za Yesu, sasa ukimkataa mwisho wa safari utaenda kwa nani?
………………………
Na kuhusu kusadiki au kutowasadiki manabii, Bwana Yesu alisema hivi:
BASI HAPO MTAKAPOLIONA CHUKIZO LA UHARIBIFU, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),
ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;
naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;
wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.
Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!
Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.
Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.
Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.
Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.
Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.
BASI WAKIWAAMBIA, YUKO JANGWANI, MSITOKE; YUMO NYUMBANI, MSISADIKI.
Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. (Mat 24:15-27)
……………………
Sasa nakuuliza hivi, Ibra, chukizo la uharibifu limeshaonekana? Wewe unaonyesha kana kwamba kila anayesema miujiza ya Yesu, kwa kuwa kwa akili za kibinadamu haieleweki, basi ni unabii wa uongo. Sivyo. Bwana Yesu yuko kazini usiku na mchana. Anatenda mambo makubwa sasa hivi ambayo kwa akili za kibinadamu huwezi kuyakubali. Mungu wa Biblia si Mungu anayeahidi na kusema, “Amini tu utajua siku ya mwisho.” Mungu wa Biblia anasema na kuishi na wanawe sasa hivi; anashughulika na mahitaji ya sasa pia – siyo ya baadaye peke yake.
Kaka James, Pole sana kwa kazi nzito ya kueneza injili na kuwavuta watu wengi kwa Yesu. Binafsi navutiwa sana na tafakari zako na huwa nikizisoma huwa napata nuru nzuri ya rohoni na naona kubarikiwa sana. Mungu azidi kukujaza kila aina ya neema na aendelee kufanya kazi ndani mwako ili yale aliyopanga kufanyika kupitia wewe yatimilike sawasawa na mapenzi yake. Ubarikiwe sana kaka.
ReplyDeleteNakushukuru ndugu yangu kwa maneno yako ya kutia moyo sana. Mungu azidi kukubariki na kufungua moyo wako zaidi na zaidi. Asante kwa sala yako pia.
Delete