Monday, March 31, 2014

"Sikuja kutangua torati" maana yake ni nini?




Bwana Yesu alisema: Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.(Mt. 5:17-18). Ni nini maana ya andiko hili?
  
Baadhi ya watu hudhani kuwa maneno haya yanamaanisha kwamba hakuja kubadili yale yaliyokuwako zamani; yaani kwamba yale ya zamani bado yanatakiwa kutendeka kama ilivyokuwa katika nyakati za zamani.

Lakini maana hasa ya maneno haya ya Bwana Yesu ni nini? 

Ulimwengu huu unaenda kwa ratiba. Inaeleweka kwamba, katika uumbaji wote wa Mungu, macho ya Mungu yameelekea zaidi kwa kiumbe huyu, mwanadamu! 

Imeandikwa kwamba: Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (Zab. 8:4-6).

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, hiyo ratiba ya Mungu inahusiana zaidi na mwanadamu. Ndiyo maana hata ardhi inalaaniwa au kubarikiwa kulingana na mwenendo wa mwanadamu.

Tunaweza kuigawa ratiba hiyo ya uumbaji katika hatua nne, yaani: 

  • Kwanza ilianza kwa mwanadamu kuumbwa katika utakatifu na ukamilifu. Imeandikwa: Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. (Mwa. 1:31). Hii inaonyesha kuwa mwanadamu naye alikuwa ni mwema, mtakatifu na mkamilifu kabisa.
  • Lilifuata anguko la mwanadamu kutokana kuasi sheria ya Mungu na kuingia kwa dhambi na laana ulimwenguni. Kwa mfano, Mungu anamwambia Adamu: Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako... (Mwa. 3:17). 
  • Kisha ulikuja ukombozi kwa njia ya mauti ya Yesu Kristo. Imeandikwa: Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. (Yoh. 3:16). 
  • Hatimaye, kitafuata kipindi cha kumilikishwa mambo yote katika nchi na mbingu mpya. Maana maandiko yanasema: Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamona yeye Aliyemfanya mdogo punde kuliko kuliko malaika, yaani Yesu...(Ebr. 2:8-9).

Kutokana na anguko katika bustani ya Edeni, mwanadamu alitengwa mbali na Mungu. Dhambi ni kitu kibaya sana mbele za Mungu aliye mtakatifu. Kwa sababu hiyo, iliingizwa torati/sheria. ...ili kosa lile liwe kubwa sana... (Rum. 5:20). Maana maandiko yanasema kwamba: ... sheria haimhusu mtu wa haki, bali waasi, na wasio wataratibu, na makafiri, na wenye dhambi... (1 Tim. 1:9). Hii ni kusema kwamba, sheria huja kwa sababu ya kuwapo kwa waasi.

Torati ina maagizo mengi ndani yake. Lakini yote yalikuwa na athari moja kubwa: yalileta mauti kwa mwanadamu. Iweje tena torati ilete mauti? Paulo naye anauliza swali hilihili: Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? (Rum. 7:13).

Mauti hii haikuja kwa sababu torati ni mbaya, hapana! Bali, mauti ilikuja kutokana na udhaifu wetu wa kibinadamu. 

Maandiko yanasema: Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti, bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haiitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. (Warumi 8:7).

Kupitia torati, Mungu alikuwa anamwambia mwanadamu, “Kwa kuwa umeniasi na kusababisha dhambi kuingia ulimwenguni, [maana maandiko yanasema katika Warumi 5:12:...kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, basi ili uweze kuishi au kutoka kwenye hali ya umauti, ni lazima utimize sheria (torati) YOTE! Maana imeandikwa: Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. (Yak. 2:10).

Hata hivyo, kama tulivyoona hapo juu, tatizo likawa kwamba, hakuna hata mwanadamu mmoja anayeweza kutimiza matakwa YOTE ya torati. Maana: Wote wamepotoka, wameoza wote pia; hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. (Rum. 3:12).

Mungu si kigeugeu hata siku moja. Akisema jambo, amesema. Alishasema kwamba matokeo ya dhambi ni mauti – basi! Mbele zake hakukuwa na uwezekano hata kidogo wa kuja tena kusema kinyume, labda: “Kwa kuwa mwanadamu ameshindwa kitimiza torati, basi nitamsamehe tu.” Hapana! 

Neno la Mungu linaeleza msimamo wa Mungu juu ya dhambi yoyote ile. Imeandikwa: ... wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe. (Nah. 1:3). 

Ilikuwa ni lazima madai au masharti YOTE ya torati yatimizwe. Na hapo ndipo anapoingia Bwana Yesu na haya maneno yake: Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. (Mt. 5:17-18). 

Kulingana na kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI, neno ‘tangua’ maana yake ni vunja kanuni au maafikiano; batilisha. 

Anachomaanisha Bwana Yesu hapa ni kwamba: Sikuja kubatilisha hata nukta moja ya torati; yote ni lazima itimizwe kama inavyotakiwa, maana uasi ulishafanyika kwa hiyo hukumu inayotolewa na torati ni lazima itimizwe kikamilifu! Kwa sababu dhambi imeshaingia ulimwenguni, na torati inasema kwamba mshahara wa dhambi ni mauti, basi ni LAZIMA hilo litimizwe. Si hivyo tu, lakini pia na madai mengine yote mahsusi kwa dhambi mahsusi nayo ni lazima yatimizwe.

Si rahisi kutaja madai na hukumu zote za torati katika makala haya mafupi, lakini inaeleweka kwamba dhambi ilipoingia ulimwenguni ilifungulia mlango wa kila jambo baya kutoka kuzimu. Mambo hayo ni pamoja na magonjwa, umaskini, chuki, dharau, uasi, hasira, n.k. Ha haya yote mwisho wake ulikuwa ni mauti. 

Kimsingi sisi wanadamu ndio tuliotakiwa kulipa kila hukumu ambayo torati inaitamka juu ya kila anayetenda dhambi. Lakini Mungu kwa huruma zake akamtuma Mwanawe Yesu Kristo ili aje alipe hukumu hizo. 

Hebu tuangalie vitu vichache vilivyoingia ulimwenguni kutokana na uasi na jinsi ambavyo Bwana Yesu alitimiza madai ya torati ili kurejesha kile kilichokuwa kimepotea:
  • Huzuni
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu. (Isa. 53:4).
  • Amani
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake. (Isa. 53:5).
  • Magonjwa
... kwa kupigwa kwake sisi tumepona. (Isa. 53:5).
  • Umaskini
Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. (2 Kor. 8:9).
  • Dhambi
Lakini BWANA  aliridhika kumchubua; amemhuzunisha; utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi. (Isa. 53:10). Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. (Yoh. 1:29).
  • Mauti
Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. (Rum. 6:23).

Kwa hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, kutokana na ukweli kwamba Bwana Yesu alitimiza sheria yote, ndio maana sisi leo tunapokea wokovu kwa njia ya imani na si kwa kujaribu kutekeleza masharti ya torati. 

Imeandikwa kwamba: Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu, .... aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani. (Kol. 2:12-15). Haleluya kwa Bwana!

Ni kweli maandiko yanasema kuwa imani pasipo matendo imekufa, lakini hatutendi matendo mema kwa lengo la kupata wokovu. Wokovu wetu tunapokea bure kwa kuamini kazi aliyofanya Bwana Yesu ya kulipa deni na hukumu nzima ya torati. Kisha baada ya hapo ndipo tunaanza kutenda matendo mema ili kuonyesha utii kwa Mwokozi wetu na pia kufaidiana sisi kwa sisi wanadamu. 

Ashukuriwe Mungu wetu ambaye alitimiza masharti yote ya torati nasi hatudaiwi tena. Tunapokea wokovu kwa imani. Si tena kama zamani ambapo torati iliagiza kwamba: ...mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo. (Law. 18:5) – jambo ambalo, kutokana na udhaifu wa mwili, HALIWEZEKANI!

4 comments:

  1. asante sana somo hili limenipa ufumbuzi wa swali lililonisumbua kwa muda mrefu. james naomba unisaidie kwa nn wakristo ukiacha wasabato wanakkula wanyama waliokatazwa? je imeruhusiwa wapi?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom ndugu katika Kristo

      Nitakujibu kwa kifupi. Biblia inasema hivi kuhusu torati ---------------- Basi mambo hayo yaliwapata wao KWA JINSI YA MIFANO, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakorintho 10:11)


      Kwa maana KRISTO NI MWISHO WA SHERIA, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. (Rum 10:4)


      Asilimia kubwa ya amri zilizomo kwenye torati zilikuwa ni MFANO WA KILE HALISI AMBACHO MUNGU ALIKIANDAA TANGU KUWEKWA KWA MISINGI YA ULIMWENGU. Yesu alipokuja, alileta hicho kilicho halisi.


      Ndio maana Bwana Yesu alipokuja, alisema hivi kuhusu chakula----------------


      Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo. Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili? HAMJAFAHAMU BADO YA KUWA KILA KIINGIACHO KINYWANI HUPITA TUMBONI, KIKATUPWA CHOONI? Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi. (Mat 15:15-20)


      Nakushauri uingie kwenye blog yangu www.injiliyakweli.blogspot.com
      Nenda kwenye section ya FREE E-BOOKS tafuta e-book inayoitwa JE, SABATO NI SIKU KATIKA JUMA?

      Hiyo itakupatia jibu lako kwa ukamilifu.

      Bwana Yesu akubariki.

      Delete