Monday, March 4, 2013

Je, Yesu Aliagiza Wafuasi Wake Wawaue Maadui wa Yesu?


Katika makala yangu niliyoipa kichwa kisemacho: Je, Muhammad Ametabiriwa Kwenye Biblia? – Sehemu ya II, yaliyo hapa; ambayo kimsingi ninaonyesha kimaandiko kwamba Muhammad kamwe hajatabiriwa kwenye Biblia, rafiki yangu Ibra kwenye sehemu ya maoni (comments) umenipa changamoto mojawapo ya muhimu sana.

Unasema: Mr. James, Kitu kibaya kwako ulichokiona kimeandikwa ndani ya qurani ni juu kuwachinja watu waovu? Sasa kama ndio hivyo, wewe hujasoma biblia au biblia hauijui vizuri. Unafanana na mtu wa kucopy na kupaste.

Katika kuthibitisha hoja yako, Ibra umenukuu Luka 19:27, ambayo inasema: Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.

Sababu  hasa ya kuleta andiko hili ni kwamba, mimi na Ibra tumeanzia mbali katika kujadiliana kwetu. Ilifika mahali ambapo anasema kuwa Muhammad amekuja duniani na ujumbe wa amani. Ndipo nikamwambia hiyo si kweli hata kidogo. Je, mtu wa amani huua watu wasiokubaliana naye? Hiyo ndiyo amani? Na ndipo Ibra akaleta jibu kama ilivyo hapo juu.

Kwa andiko hili, Ibra pamoja na Waislamu wengine, mnataka kuonyesha kuwa eti Yesu naye alikuwa ni mwuaji wa waovu. Angalia Ibra, isije ikawa wewe ndio unacopy na kupaste.


Sasa, hebu tusome muktadha mzima uliozaa andiko hilo badala ya kusoma mstari wa 27 peke yake. Tutasoma Luka 19:12-27.


Yesu alikuwa anaongelea mfano (parable) inayohusu ule wajibu ambao Mungu ametupatia sisi wanadamu na kile kitakachotokea mbinguni baada ya maisha haya, pale Mungu atakapokuwa anatulipa wanadamu wote sawasawa na matendo yetu.


Imeandikwa hivi:

12  Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

13  Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.

14  Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

15  Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

16  Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17  Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18  Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19  Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

20  Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

21  Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22  Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23  basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24  Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25  Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26  Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.

27  Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.


Ndugu yangu Ibra, Bwana Yesu alipotoka mbinguni na kuja duniani, baada ya hapo alisafiri hadi nchi ya mbali – yaani alirudi mbinguni ambako ndiko aliko hadi sasa. Mtu anayesafiri maana yake ni kuwa atarudi.


Ndiyo maana alipokuwa anaondoka, alisema hivi: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. (Yohana 14:1-3)


Kila mmoja wetu amepewa talanta (vipawa) mbalimbali kwa lengo la kumtumika Mungu. Lakini wengine wanavitumia kwa faida zao wenyewe tu, au hawavitumii kabisa. Sote tunajua kuwa hukumu ya mwisho ni kutupwa kwa waovu jehanamu. Na atakayewatupa waovu si shetani, bali ni  Mungu mwenyewe.


Kwa hiyo, sisi ni watumwa wake ambao tumekabidhiwa ‘mafungu mbalimbali ya fedha’ kwa lengo la kufanya ‘biashara ya ufalme.’ Biashara ya ufalme ni pamoja na kuhubiri Injili, kumwamini Kristo, kuwasaida wahitaji, n.k. Kwa ujumla ni kuishi sawasawa na amri za Mungu.


Lakini hebu soma kwa makini mstari wa 14 unasemaje: Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.


Asilimia kubwa sana ya wanadamu, ukiwamo wewe Ibra kwa sasa, wanasema, “Hatumtaki Yesu awe Mungu wetu!”


Yafuatayo ni maneno yako mwenyewe Ibra ambayo umeyasema kwenye hoja yako hiihii:


Na swala ya Yesu kuwa mungu, mimi nasema hivi, hawezi kuwa mungu, si mungu, hana mpango wa kuwa mungu, hatakuwa mungu ila, ni mtume tu wa mungu kwa wana waisrael peke yao kwa ushahidi wa maandiko yafuatao:

Yohana 17:3-4 Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.
4 Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.
Yohana 17:6-9 6 Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika.
7 Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako.
8 Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
9 Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;
KAULI YA YESU INASEMA HAUOMBEI ULIMWENGU, BALI WALE ALIOPEWA.

Matendo 13:23 Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;
Matendo 5:31 Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi.
Matayo 15:24 Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
Hapa Yesu hajakosea kwa sababu msingi umeshawekwa na mungu katika ISAKA ya kwamba atafanyanae agano kwa ajili ya uzao wake tu baada yake.

Marco 16:15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.

matayo 28:19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
Mr. iko wapi kauli sahihi ya yesu?
Alafu ukisikia neno mataifa, kibiblia ina maana nyingi:
1 makabila 12 ya waisraeli:
2 nchi
Fungua biblia za kale utaona ramani ya ulimwengu, tanzania haipo na nchi nyingine pia.
YESU KRISTO NI MTUME MWENYEZI MUNGU KWA WANA WA ISRAELI.

Sasa, Yesu atakaporudi tena ulimwenguni kutoka kwenye hiyo safari yake ya mbali, ndipo kila mwanadamu atawekwa mbele zake, wakati huo Bwana Yesu akiwa ni HAKIMU. Atataka kujua umefanya nini na vipawa alivyokupa. Mstari wa 15 unasema: Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.


Ni wazi kuwa wengine watakutwa wameishi sawasawa na amri za Mungu na wengine walimkataa Mfalme huyo na wakaishi maisha ya uasi na ubinafsi.


Ndipo sasa tunafika kwenye andiko lako la Luka 19:27, ambalo linasema: Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.


Lakini nilikuambia usome kwa makini mstari wa 14. Mstari huo ulisema: Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.


Hawa ndio maadui wa Mfalme. Yaani hawataki kusikiliza maagizo yake na kuishi sawasawa na amri zake. Ndipo Yesu, kwa kuwa ameshaupata ufalme, Yeye ndiye mwenye amri ya mwisho; basi (wakati huo) atatoa agizo, akisema: Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.


Simulizi yote hii haikuwa ni maagizo ya Bwana Yesu kwa wafuasi wake na wala haukuwa msimamo wake juu ya maisha yetu hapa duniani dhidi ya watenda dhambi. Hapana! Huu ulikuwa ni mfano (parable) wa kile kinachoendelea hapa duniani baada ya Yesu kuondoka na kile kitakachotokea mbinguni baada ya Yeye kurudi. Na kwa vile siku zote mfano huwa unawakilisha jambo fulani halisi, katika maandiko haya, 'safari ya mbali' ni kitendo cha Yesu kwenda mbinguni; 'mafungu ya fedha' ni talanta na vipawa; 'kufanya biashara' ni kuishi maisha ya utakatifu, utii na utumishi; na 'kuchinjwa' hapa kunawakilisha kutupwa jehanamu ya moto siku hiyo kwa wale waliomkataa Mfalme.


Hapa Bwana Yesu haongelei kamwe kuchinja wanadamu hapa duniani! Hakuna mahali popote kwenye Biblia ambako Bwana Yesu anaagiza uuaji na uchinjaji wa wanadamu hapa duniani. Hakuna! Badala yake, Bwana Yesu anaagiza kupendana, kusamaheana, na hata kuwapenda wale wasiotupenda.


Haya Ibra, ni wapi ambako mimi nimecopy na kupaste?


Ndugu zangu Waislamu, amkeni. Kila ninapowatafakari, ninawahurumia sana kwa jinsi mnavyotumia juhudi na nguvu kubwa kueneza uongo kwa lengo la kuhalalisha kitabu chenu. Uongo huo ni kupindisha Maandiko ya Biblia ili kwamba yaendane na kile kilicho kwenye kitabu chenu. Kwa bahati mbaya, hamwezi kamwe kufanikiwa kwa sababu hicho mnachokisaka kwa shauku kubwa hivyo hakimo kabisa kwenye Biblia. Biblia haina chochote kinachounga mkono Quran; maana hivi ni vitabu viwili ambavyo, kimoja kinatazama mashariki na kingine kinatazama magharibi.


Lakini ni muhimu nikiri pia kwamba, najua kuwa kuna Waislamu wengi ambao wanaamini kwa moyo wa dhati kabisa kwamba wako kwenye njia sahihi. Pale wanapotumia haya Maandiko ya Biblia kuhalalisha Uislamu hawafanyi hivyo, labda kwa nia ya kuwapotosha na kuwanasa Wakristo au watu wengine ili kuwaangusha. Hapana. Wanafanya hivyo kwa kuamini kabisa kuwa wako sahihi na kwamba hicho wanachokifanya ni utumishi wa kweli kwa Mungu. [Ingawaje wapo wanaojua kabisa kuwa wanadanganya na hivyo wanafanya makusudi].


Ila ukweli unabaki kwamba, ama unamwamini Yesu na kupokea uzima wa milele; au unamkataa na kuchinjwa (yaani kutupwa jehanamu) siku ya mwisho. Basi!!!

Tafakari.
Hoji.
Chunguza mambo.
Chukua hatua.

7 comments:

 1. Mr.James, kama unakumbuka, umewahi kuniambia ktk moja wapo ya post zako ya kwamba, Mungu wako jina lake YEHOVA, YESU AU ROHO MTAKATIFU. Sawa?
  Kwa maana hiyo, unaposema Yesu hajawahi kuuwa unamaanisha Yehova au roho mtakatifu hajawahi kuuwa. Sasa je! ni kweli Yesu yaani, yehova au roho mtakatifu hajawahi kuuwa?
  JIBU NI KWAMBA AMEWAHI KUUWA!

  HESABU 21:5-6
  .5Nao watu wakaendelea kusema dhidi ya Mungu na Musa: “Kwa nini mmetutoa Misri ili tufe nyikani? Kwa maana hakuna mkate wala maji, nayo nafsi yetu imeuchukia huu mkate wa kudharaulika.”6Basi Yehova akatuma nyoka wenye sumu katikati ya watu, nao wakawa wakiwauma watu, hivi kwamba watu wengi wa Israeli wakafa.

  KUMB. 7:1-2
  1“Wakati ambapo Yehova Mungu wako mwishowe atakuingiza katika nchi ambayo unaenda kuimiliki, pia ataondolea mbali mataifa yenye hesabu kubwa ya watu toka mbele yako, Wahiti na Wagirgashi na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahivi na Wayebusi, mataifa saba yenye hesabu kubwa ya watu na yenye nguvu kuliko wewe.2Na Yehova Mungu wako hakika atawatia hao mkononi mwako, nawe utawashinda. Unapaswa kuwaangamiza. Usifanye agano lolote pamoja nao wala kuwaonyesha kibali chochote.

  LUKA 22:36
  36 Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue.

  MATAYO 10:34
  34 Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

  1SAMWELI 15:2-3
  2 Bwana wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
  3 Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng'ombe na kondoo, ngamia na punda.

  1SAMWEL 6:19

  19 Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu.

  HESABU 15:36
  36 Basi mkutano wote wakampeleka nje ya marago, nao wakampiga kwa mawe, akafa; kama Bwana alivyomwagiza Musa.

  HOSEA 13:16
  16 Samaria atachukua hatia yake; kwa maana amemwasi Mungu wake; wataanguka kwa upanga; watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande, na wanawake wao wenye mimba watatambuliwa.

  Mr,James vipi hapo? Acha tabia ya kwangalia upande mmoja.
  Mr. James, mimi nimetoa changamoto zangu kwa nini nasema YESU SIO MUNGU, HAWEZI KUWA MUNGU, HANA MPANGO WA KUWA MUNGU,NA HATAKUWA MUNGU MILELE AMINA.

  Sasa wewe toa andiko, ni wapi mungu anamtuma mungu kuja duniani.
  Hivi, ni nguvu gani nyie wakristo, inayowaponza kwa kukataa kauli za mwenyezi mungu pamoja na za yesu mwenyewe, badala yake mnakubari maneno ya watu wanaofanana na nyie?

  Yesu kenda karudi, ndio iwe sababu ya wewe kudai ni mungu?
  SASA BASI, YESU WAKATI ANAKATA ROHO PALE MSALABANI, ALIMLALAMIKIA MUNGU KWA NINI AMEMUACHA? UNANJUWA ANAITWAJE? NI ALLAH(ELOIM).

  KWA KUWA NYIE NI WABISHI NA BADO MNA'GAN'GANIA YESU KUWA NI MUNGU WENU, SISI MUNGU WETU NI YULE AMBAYE YESU ALIKUWA ANAMUOMBA NA KUMTEGEMEA.

  YOHANA 20:17
  17 Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.


  ReplyDelete
  Replies
  1. Ibra, katika jibu lako hili naona hoja kuu mbili: 1. Unataka kuonyesha kuwa Mungu wa Biblia aliua. 2. Ni jambo lisilowezekana kwamba Yesu ni Mungu maana mara nyingi tu alikuwa anasikika akimwomba Mungu; au akimzungumzia Mungu, mambo ambayo yanaashiria kuwa kulikuwa na Mungu na pia kulikuwa na Yesu.
   Nikianza na suala la kwanza, Ibra uko sahihi kabisa juu ya kile nilichokisema kuwa Mungu wangu anaitwa Yehova/Yesu/Roho Mtakatifu.

   Pamoja na kwamba mimi sikusema “Yesu hajawahi kuua,” bado hata hivyo maneno hayo ni ya kweli. Ila mimi nilichosema ni hiki: “Hakuna mahali popote kwenye Biblia ambako Bwana Yesu anaagiza uuaji na uchinjaji wa wanadamu hapa duniani.”
   Ibra katika Ukristo tunaamini katika Mungu mmoja tu ambaye anajidhihirisha katika nafsi tatu, ambazo ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Unapomuwaza Mungu katika Umungu wake, hivi ndivyo anavyosema: Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; NAUA MIMI, NAHUISHA MIMI, NIMEJERUHI, TENA NAPONYA; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu (Kumbukumbu 32:39).

   Kwa hiyo ukiniuliza iwapo Mungu huua nitakwambia kuwa ndiyo kwa sababu hivyo ndivyo anavyosema kwenye Neno lake takatifu. Naamini utakumbuka kwamba nilikwambia kuwa ni muhimu sana kutambua kuwa Biblia YOTE ni Neno la Mungu. Na ni muhimu sana kutambua mpango WOTE wa Mungu juu ya mwanadamu, yaani kuelewa majira na nyakati katika Biblia nzima.

   Delete
  2. Si kila kitu kwenye Biblia kinahusiana na SASA. Kuna mambo yanayohusu SASA, mengine yalihusu ZAMANI, na mengine yanahusu BAADAYE. Kwa kifupi uumbaji wa Mungu umepangwa kama ifuatavyo:
   HATUA YA 1: Kuumbwa kwa mwanadamu katika utakatifu wote (yaani Adamu na Hawa).

   HATUA YA 2: Anguko la mwandamu kwenye dhambi, yaani Adamu na Hawa waliasi sheria ya Mungu na kujinajisi kwa dhambi. Ule utakatifu mkamilifu uliokuwa ndani yao ulinajisika. Matokeo yake hata uzao wao, (yaani wanadamu wote), nao ulinajisika. Biblia inasema wazi: Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi (Warumi 5:12).

   HATUA YA 3: Kuletwa kwa sheria (torati) ili:
   - Kwanza kuifanya dhambi ijulikane na pili kuwafanya watenda dhambi (yaani wanadamu wote) watambue jinsi walivyo na hatia mbele za Mungu. Imeandikwa: Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu (Warumi 3:19).

   Naamini utakubaliana na mimi kuwa unaweza ukawa unapita njia fulani kila siku wala usijisikie hatia yoyote moyoni mwako. Lakini siku ukikuta kibao kimewekwa kikisema “Marufuku kupita hapa,” kuanzia hapo kama utaamua kupita njia ile, LAZIMA utajisikia hatia kwa sababu tayari kuna sheria. Kabla ya hapo inawezekana kabisa mwenye eneo hakupenda watu wapite hapo. Lakini kwa vile hakuwa ameweka sheria, ndio maana waliopita hawakujisikia hatia japokuwa walikuwa wanatenda makosa. Kwa upande wa kuvunja sheria za Mungu ni vivyo hivyo. Biblia inasema: Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa. (Rom 4:15). Hii maana yake ni kuwa, kabla Mungu hajaleta torati wanadamu walikuwa wanatenda dhambi na Mungu hakuwa anapendezwa na dhambi hizo. Lakini kwa vile hakuwa ameweka sheria, watu hawakujua kosa ni lipi na usahihi ni upi. Pia, walitenda makosa bila kujisikia hatia. Ndipo Mungu akaleta torati. Imeandikwa: Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana (Warumi 5:20).

   - Tatu, kuonyesha jinsi Mungu anavyochukia sana dhambi. Hii inatokana na ukweli kwamba dhambi iliadhibiwa kwa ukali sana. Kwa mfano torati inasema: Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema. Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko. (Kutoka 21:22-25).

   - Nne, kutuonyesha jinsi ambavyo hatuwezi kamwe kujiokoa au kutii kikamilifu sheria za Mungu hata kama tungejitahidi namna gani. Mwanadamu yeyote anayesema kuwa yeye anaweza kuishi sawasawa na sheria zote za Mungu huyo ni mwongo na mwenye kiburi (proud). Biblia inasema: kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria (Warumi 3:20). Kwa nini? Kwa sababu hakuna mwanadamu anayeweza. Hakuna! Hakuna!

   Matokeo ya hali hii yalikuwa ni kumfanya mwanadamu awe chini ya utumwa wa dhambi na anguko la milele. Ni utumwa wa dhambi kwa sababu sasa alikuwa anajitambua jinsi alivyo mtenda dhambi, lakini kibaya zaidi kila akijaribu kuacha dhambi anakuwa hawezi kabisa. Dhambi inakuwa ndio mtawala wake katili. Yeye anakuwa mtumwa wa hiyo dhambi – iwe ni ulevi, hasira, tamaa, uzinzi, chuki, uchawi, uongo, n.k. Kwa hiyo, wakati wote anakuwa chini ya hukumu ya Mungu na mwisho wake, bila shaka ni kutupwa jehanamu ya moto. Tusiongee kinadharia. Tuongee ki-hali halisi. Je, Ibra wewe unaweza kujisema kuwa umefanikiwa kuacha dhambi na kuishi sawasawa na sheria za Mungu? Najua kuwa hujaweza na hutaweza kamwe daima dawamu!! Si kwa sababu wewe ni Ibra au kwa kuwa ni mwislamu, hapana. Bali kwa kuwa wewe ni mwanadamu. Huna uwezo wa kufikia viwango vya Mungu.

   Delete
  3. Angalizo: Torati haikuja ili mwanadamu aweze kuitimiza na kujiokoa kwa huko kuitimiza kwake. Anayedhani kuwa anaweza kuitimiza anajidanganya na mwisho wake ni kuangamia milele – maana sheria ya Mungu inasema kuwa “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23).

   HATUA YA 4: Kuokolewa kwa mwanadamu. Kwa vile basi kwa asili mwanadamu ni mtenda dhambi, Mungu kwa upendo wake aliamua kuleta wokovu kwa huyu mwanadamu. Hapa ndipo Mungu alivaa mwili wa kibinadamu akiwa kama Yesu na kuja kuishi maisha ya kibinadamu bila kutenda dhambi. Kisha akabeba dhambi zetu zote sisi wanadamu. Na kwa kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, Yesu aliuawa kwa niaba yetu. Yaani ni kuwa, alipata mauti kutokana na dhambi zetu ili sisi tupate uzima wa milele kwa utakatifu wake kama tukimuamini tu.

   Ibra, nikija sasa kwenye hoja yako kwamba Mungu wetu aliua, hilo ni kweli kama aambavyo tumeona anasema Yeye mwenyewe. Kwani si ni Mungu ndiye aliyemweka shetani hata hivyo?

   Lakini jambo la kutambua ni kuwa, wakati wa majira ya torati (ambayo sasa yameshapita), watu waliuawa kwa amri za torati ya Mungu huyohuyo katika nafsi ya Baba. Lakini katika kipindi hiki (ambacho kinaitwa ni kipindi cha neema, Mungu huyohuyo katika nafsi ya Mwana (Yesu), Yeye sasa ndio kaamua kuja kuuawa badala ya watu wake kuuawa kwa kutenda makosa. Tunachotakiwa tu ni kuamini kwamba alikufa kwa ajili yetu na kuomba msamaha. Simple! Ibra, unataka upendweje na Mungu zaidi ya upendo huo? Kwa ninibado unakimbilia kujibebesha kongwa la sheria ambalo hata kulibeba kwenyewe huwezi? Yaani unakimbia uhuru na kukimbilia utumwa? Inashanza kweli?


   Unapomwamini Yesu, Mungu katika nafsi ya Roho Mtakatifu anakuja moyoni mwako na kukufundisha jinsi ya kuenenda katika utakatifu. Si kwamba ataondoa kila kitu ghafla, lakini ataenda na wewe polepole katika maisha yako yote huku ukiendelea kumjua Mungu, kumfurahia na kukua katika wokovu.

   Nikija kwenye suala lako la pili: Najua kuwa kinachowasumbua Waislamu ni mazoea yenu ya KUMBEBESHA MUNGU TABIA ZA KIBINADAMU. Katika nukuu zako zote hapo juu, kwa kifupi unachomaanisha tu ni kwamba: Mungu hawezi kuwa mbinguni kisha akawa duniani kwa wakati uleule.

   Hukumuni wenyewe kama kweli mtazamo wenu huo ni sahihi. Je, kwa vile hilo kwa mwanadamu haliwezekani ndio kusema na kwa Mungu nako lisiwezekane? Kwani Mungu ni mwanadamu?

   Je, Mungu anawezaje basi kusikia maombi ya watu milioni 500 wanaomwomba China na milioni 300 wanaomwomba Marekani na milioni 200 wanaomwomba Afrika na milioni 400 wanaomwomba India, n.k., huku wote hao wakiomba kwa wakati mmoja na sehemu mbalimbali??? Au Mungu anasikiliza maombi ya wanadamu kwa zamu – yaani mmoja baada ya mwingine?

   Je, hawezi kuwasikia na hata kuwajibu wote kwa mara moja? Bila shaka kwa mantiki yenu inaonekana kuwa hawezi kabisa, si ndiyo? Maana haya mamilioni ya watu yako vijijini, mijini, nyumbani, makanisani, porini, baharini, kwenye ndege, migodini, n.k.

   Na kama anaweza kufanya hili kwenye mabilioni ya sehemu kwa mara moja, itakuwa ni ajabu sana kama atashindwa kuwa sehemu MBILI TU!! – yaani mbinguni kama Baba na duniani kama Yesu!!!! Na Mungu wa hivyo, mimi simtaki.

   Mungu wangu ninayemwamini, anaweza yote!! Hili ni jambo dogo sana kwake.

   Ndugu zangu Waislamu niwapendao kwa moyo wote, changamkeni sasa. Wakati wa kung’ang’ania mambo ambayo hamyawezi (kushika torati) ulishapita. Hiki ni kipindi cha neema ya Mungu kwa mwanadamu – wokovu kwa imani katika Kristo Yesu tu. Imani tu. Mbona mnang’ang’ania utumwa?

   Delete
  4. Mr.James!
   Mi nahisi wewe umeshindwa kabisa kulitetea kanisa. Nasema hivyo kwa sababu unakataa na kuniona mimi ni muongo kwamba wewe ujasema kuwa yesu ni mungu. Sasa huu ni ushahidi wa kile ulichokiandika katika ''Je Muhammad ametabiriwa kwenye biblia sehemu ya pili'' kwenye kurasa za comments.
   James JohnFebruary 12, 2013 at 3:58 PM
   Kuhusiana na kwamba Muhammad alitumwa kwa watu wote, hilo nalo silikatai hata kidogo. Ni jambo la kweli pia. Lakini swali la msingi ni kwamba, je, katumwa na nani? Mungu wa Biblia anaitwa Yehova, au Yesu Kristo, au Roho Mtakatifu. Ukiniambia kwamba huyu ndiye aliyemtuma Muhammad, hapo ndipo nitakwambia bila kumung’unya maneno kwamba jibu ni HAPANA!

   Mr.James unaposema mungu wa biblia anaitwa yehova au yesu au roho mtakatifu inamaanisha ni kitu kimoja hiko hiko.
   Acha kuwa na kauli mbili mbili, thibitisha kitu, watu wakuelewe ili waweze kufaidika na kile unachokifundisha.
   Usiwe mjanja mjanja, mungu kaua unasema yesu sio mungu ni mtume tu. Mungu kaleta upendo, unasema yesu mungu, nikuelewe vipi?
   Mr.James, mistari ya biblia niliyokutolea nimekuthibitishia kwamba, Mungu pekee ndio mwenye uwezo wa kuua. Kwanini ushangae kuuwawa kwa watu kwenye islam na haushangai kwenye biblia?
   Kuua kwa Yesu au Kutokuua, kukata viungo vya wanadamu ndani ya biblia, haimaanishi hukumu hiyo haikuwepo kwa sababu hata muhammad hajawai kuua hila agizo la mungu kwa wanadamu inasema hivyo. Yesu hakuja kuzifuta sheria bali kutumikia.
   James, mi nina wasiwasi juu ya imani yenu nyie wakristo mnamfuata nani? Na kama mnamfuata yesu, mbona hamwenendi katika njia zake?

   Matayo 5:17-20
   17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.
   18 Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie.
   19 Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
   20 Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

   Matayo 5:29-30
   29 Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.
   30 Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.

   Matay 5:21-22
   21 Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.
   22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.

   Na kuhusu swala la bible YOTE kuwa neno la mungu unapingana na maandiko ya biblia hiyo hiyo:

   Yeremia 8:8
   8 Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.

   Biblia haiwezi kuwa neno la mungu kwa sababu inajipinga yenyewe:

   Yakobo2:24 v/s warumi 3:28
   (24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.)
   (28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.)

   Mwanzo 4:26 v/s Kutoka 6:2-3
   (26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana)

   Ezequiel 18:20 v/s Kumb. 5:9
   (9 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,)
   (20 Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.)   Delete
  5. Shalom Ibra. Nimekujibu maswali yako kwa makala. Tazama kwenye makala yasemayo: Majibu Yangu kwa Ibrabura - Sehemu ya 1. Mungu akubariki.

   Delete
  6. Yeremia 8:8 inasema kwamba: Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.


   Ibra na Waislamu wengine mlipoona maneno katika Yeremia 8:8 yasemayo: “Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo,” kama kawaida, mkajua kuwa huu tayari ni ushahidi kwamba Biblia imetiwa maneno ya uongo, kwa hiyo si neno la Mungu na haiwezi kuaminika.

   Lakini mara zote nimekuwa nikikupeleka kwenye muktadha wa kila andiko au hoja ili kuona kama kweli hoja hizo zina nguvu ya kusimama. Hebu anzia kwenye Yeremia 7:1-11.


   1) Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,

   2) Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana.

   3) Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.

   4) Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.

   5) Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake;

   6) kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe;

   7) ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.

   8) Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.

   9) Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;

   10) kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?

   11) Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.


   Mwito mkuu kabisa wa Bwana ulikuwa kutaka watu wa Yuda wajirekebishe. Mstari wa 3 anawaambia “Tengenezeni njia zenu.”

   Hii ina maana kuwa njia zao zilikuwa kinyume na amri za Mungu. Na kwa nini zilipotoka? Mstari wa 4 na 8 – walikuwa wanatumainia maneno ya uongo.

   Maneno hayo ya uongo waliyoyaamini, yaliwafanya wasihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake; wawaonee wageni, yatima na wajane; wamwage damu isiyo na hatia; wafuate miungu mingine, n.k.

   Ndipo tunapoendelea kusoma, tunafika hadi sura ya 8. Bwana anasema:


   7) Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.

   8) Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.

   9) Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?


   Maandiko haya yanafafanua sababu ya upotovu wao. Kumbe kulikuwa na manabii na walimu wa dini waliokuwa wakiwadanganya.

   Kwenye sura ya 7 hapo juu Mungu amefafanua waziwazi ule uongo waliokuwa wakiufuata, ambao bila shaka walifundishwa na hao manabii wa uongo.

   Sasa, nikija kwenye hoja yako, Ibra, ni wapi kwenye Biblia ambako tunaagizwa tufanye mambo hayo yaliyokuwa yakifanywa na watu wa Yuda? Kama sasa utakuta mahali popote kwenye Biblia panapoagiza tufanye mambo hayo, ndipo hoja yenu itakuwa na ukweli.

   Lakini kwa kuwa mambo hayo hayapo popote kwenye Biblia, bali Biblia inayo yale mambo ambayo ndiyo Bwana alitaka watu wa Yuda wabadili njia zao na kuyafanya, basi Biblia ni Neno la Mungu la kweli.

   Delete