Tuesday, March 5, 2013

Mpiganaji wa Hezbollah Akutana na Yesu na Kuokoka – Sehemu ya II





Afshin Javid alikuwa ni askari wa Hezbollah ambaye aliyatoa maisha yake kikamilifu kwa ajili ya Allah. Katika maisha yake yote, alijifunza kumtii Allah na alikuwa tayari kufanya lolote, ikiwa ni pamoja na kufa kwa ajili ya Allah.


Lakini baada ya kukutana uso kwa uso na Bwana Yesu, kila kitu kilibadilika. Sikiliza ushuhuda wake huu wenye nguvu sana, ambao si  tu kwamba utakutoa machozi, kama yeye mwenyewe anavyoeleza kwa machozi mengi, bali pia utajua jinsi Bwana Yesu alivyo Mungu Mkuu na wa kweli ambaye, kila anayemtafuta kwa moyo wa kweli, anamwona.


Hii ni sehemu ya pili ya ushuhuda wake. Ili kupata picha kamili, tafadhali anza kwa kusikiliza au kusoma ushuhuda wake, sehemu ya kwanza HAPA.


*******************


Nikasema, “Mbona sielewi? Jina lako ni nani?”


Akasema, “Yesu Kristo.”


Nikaanguka kifudifudi. Na nikalia! Na nikalia! Unajua, nikiwa kama Mwislamu, nilifundishwa kwamba mwanamume halii. Lakini nilishindwa kujizuia kwa sababu nilitambua kwamba mimi ni mali yake. Yeye ni njia, Yeye ni kweli, Yeye ni uzima. Nilitambua kuwa nilikuwa nimedanganywa; kwamba nilikuwa nimeondolewa kwenye nyumba yake. Nilitambua kuwa mimi ni wa kwake. Nilitambua kuwa nilikuwa nikiabudu mungu wa uongo! Nilitambua, lakini … niko nyumbani sasa.

Na alisema, “Afshin, inua macho yako.”

Na mara nilipoinua macho yangu, mbele yangu kukawa kama kuna skrini ya TV na nikaona watu wa mataifa yote na kila uzao.

Akasema, “Angalia.”

Nikaona dhambi zote. Zilikuwa nyingi sana. Nikasema, “Mungu, ninaishi katikati ya hawa wenye dhambi wote!”

Akasema, “Imekuwaje rahisi kwangu kukusamehe, Afshin?”

Nikasema, “Kirahisi sana. Kirahisi kama kunywa maji. Hapana. Hapana. Ni rahisi zaidi ya kunywa maji!”

Akasema, “Kama ilivyokuwa rahisi kukusamehe wewe, naweza kuwasamehe wote. Nani sasa atakayekwenda kuwaambia?”

Nikasema, “Mimi nitakwenda.”

Akasema, “Nenda. Nitakuwa pamoja na wewe.”

Nilitoka mbio na kukimbilia msikitini. Nilipofika, kila mtu alinikimbilia. Wakasema, “Unataka kutufundisha nini leo? Ni kutoka kwenye Quran au kwenye hadithi?”

Nikasema, “Hapana. Hapana. Sahauni Uislamu! Msahauni Allah! Sahauni Quran! Maana muda huuhuu nimemwona Yesu Kristo! Na amesema Yeye ni njia, na kweli, na uzima! Yeye peke yake ndiye kweli! Yeye peke yake ndiye njia! Yeye peke yake ndiye uzima! Na Yeye peke yake ndiye anayeweza kuwasamehe wote! Anaweza kuwasamehe wote!”

Nakupenda Yesu!

Unajua, si tu kwamba alinitoa kwenye giza, lakini pia aliponya moyo wangu. Hamuwezi kuelewa jinsi ambavyo niliingoja siku hii kwa muda mrefu sana! Maana nilikulia kwenye jeshi  nikipaza sauti kwa Kifarsi nisema, “Mar bar Israyili” – yaani “Kifo kwa Israeli.” Na nilikuwa nina shauku ya kupata siku moja ya kusema, “Baba unisamehe! Nisamehe kwa kusema hivyo! Kama Mpershia, kama Mwirani, napenda kuomba msamaha kwa ajili ya taifa langu. Kama Mwislamu, napenda kuomba msamaha kwa niaba ya kila Mwislamu kwenye dunia hii. Na kama Mpershia, napenda kusema, “Shav turuu bar Israyili”, ambayo ina maana ya “Uzima, mafanikio kwa Israeli, baraka juu ya Israeli!”

Baba naomba bariki taifa lako; bariki watu wako. Unajua, tunaongea juu ya amani kwa ajili ya Israeli. Tunaomba baraka kwa ajili ya Israeli. Ili kwamba wapate nchi ambayo Mungu aliwapatia. Lakini kuna njia moja tu. Siku watakapoijua kweli; serikali za mataifa yote zitakapoijua kweli; iko njia moja tu. Tunasema tunataka Waisraeli na hata watu wengine wote kuwa na uzima kokote kule wanakoishi. Iko njia moja tu na hiyo ni Yesu Kristo wa Nazarethi.

Yesu ulisema Wewe ni njia; ulisema Wewe ni kweli. Wewe peke yako ni njia kuelekea kwenye amani ya Israeli. Kwa hiyo Yesu, Yesu, mlete Roho wako; mlete Roho wako juu ya taifa hili. Mlete Roho wako Bwana Mungu. Bwana ibariki Israeli. Ibariki Israeli. Tusamehe. Nisamehe mimi, familia yangu; tusamehe Bwana Yesu kwa kila kitu tulichofanya dhidi ya taifa lako. Asante Yesu. Asante.

Wewe peke yako ndiwe Mungu maana hakuna kabisa namna ambavyo ningeweza kutamka mambo haya kama usingekuja moyoni mwangu! Yesu najua kwamba, kama ukija kwenye mioyo ya Waislamu; na pia ukija kwenye mioyo ya Wayahudi, Yesu; Bwana Yesu kama ukija kwenye mioyo yao, watajua, watajua! Wataiona njia, kweli na uzima ndani yako Yesu. Na hicho ndicho ninachoomba Yesu. Ufalme wako uje; na mapenzi yako yatimizwe Israeli na duniani kote kama ilivyo mbinguni.


*****************


Ndugu uliyesoma au kusikiliza ushuhuda huu, Yesu Kristo ni Mungu muumba wa mbingu na nchi. Yesu Kristo ni Mwokozi wako ambaye alitoa uhai wake mwenyewe, akamwaga damu yake kwa ajili yako na kwa ajili yangu.


Wokovu unapatikana kwa imani. Unaamini juu ya kile alichofanya Yesu pale msalabani, na kwamba alikufa na kufufuka, na hakika, unapewa UZIMA WA MILELE, yaani utakuwa HAI MILELE na MILELE ukiishi mbele za Mungu, ambaye ndiye huyohuyo Yesu.


Mungu si mfanyabiashara anayeuza uzima wa milele kwa malipo ya matendo yetu mema. Usifikiri kwamba kwa kutenda kwako matendo fulanifulani ambayo wewe unayaita kuwa ni mema, eti ndiyo yatakuwa malipo ya uzima wa milele kwa Mungu. Umedanganywa! 


Yesu ndiye Njia, na Kweli, na Uzima.


Anawezaje Mwislamu kutoka Irani ambaye amekulia katikati ya Hezbollah; ambaye amelelewa katika chuki kubwa maisha yake YOTE; ambaye lengo lake lilikuwa siku zote ni kuiharibu Israeli na wote wasiomkubali mungu wake; kwamba leo aseme, “Naipenda Israeli, Yesu nisamehe kwa kuichukia Israeli; Mungu ibariki Israeli, nampenda Yesu?” Inawezekanaje? Inawezekanaje?


Haiwezekani katu!


Ni nguvu nyingine kabisa ambayo imebadili ile roho ya uuaji ndani yake na kumpatia roho ya uzima na upendo.


Yesu peke yake ndiye Njia, Kweli, na Uzima!


Njoo kwa Yesu sasa.


Tafakari.

Hoji mambo.

Chunguza.

Chukua hatua.

No comments:

Post a Comment