Mungu
alinijibu Mimi!
Huu ni
ushuhuda wa kweli kuhusiana na maisha ya mtu aliyekuwa anamtafuta Mungu.
Habari
yako na Mungu akubariki. Jina langu ni Amal na ninashuhudia kwamba kile ambacho
unaenda kusoma ni cha kweli kabisa na sahihi kwa kadiri ya kumbukumbu zangu
maana Mungu mwenyewe ni shahidi yangu. Maombi yangu ni kwamba Mungu aseme na moyo wako na kutumia ushuhuda huu
kukubariki wewe kwa namna ya pekee maishani mwako.
Kimsingi
mimi nilikulia kwenye familia ya Uislamu mkali. Baba yangu ni Mpalestina kutoka
Israeli. Mama yangu ana asili ya Brazili. Alikuwa ni Mkatoliki. Baba yangu
alikutana naye Brazili. Walioana na mama yangu alibadili dini na kuwa Mwislamu.
Kama
ilivyo kwa watu wengi wanaohamia Marekani, familia yangu nao walikuja hapa ili
kutafuta maisha bora. Walikaa Los Angeles ambako ndiko nilikozaliwa mwaka mmoja
baadaye.
Niliamini
kila kitu nilichofundishwa kuhusu Uislamu na niliamini kuwa dini yetu ilikuwa
bora kuliko dini zingine duniani. Ingawaje, kadiri nilivyokua, baadhi ya
mafundisho ya Uislamu yalianza kunikera, kwa mfano kuvaa mavazi yanayokufunika
kabisa. Sikuelewa kwa nini nivae nguo zenye mikono mirefu, yaani ni kwa vipi
mwanamume atatamanishwa na kiwiko change, kwa mfano? Kisha kulikuwa na taratibu
za swala. Sikupenda kusema kitu kilekile tena na tena. Nilijisikia kama mambo
ya ajabu na kutengwa mbali na Mungu. Nilifundishwa kwamba ukimwomba Mungu kwa
Kiarabu, basi utasikiwa zaidi. Lakini sikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha hiyo,
hivyo nilijisikia kama nimeachwa nyuma. Nilijaribu kuziandika sala za Kiarabu
kwa Kiingereza, lakini bado kulikuwa na kitu kimepunguka. Nilitamani kuomba kutokea moyoni mwangu, na si kutokana
na maneno ambayo si yangu.
Mafundisho
mengine nayo yalinikera kama vile kuzuiwa kula baadhi ya vyakula – lakini kubwa
lililonikera zaidi ni suala la kuwa na wake wengi mbinguni. Nilimwuliza baba
yangu kama nilikuwa naenda mbinguni lakini hakunijibu. Alibaki kimya tu kuhusu
swali lile. Nikiwa tineja, niliwaza, “Sitaki kabisa kuwa mbinguni halafu niwe
mmojawapo kati ya kundi la wanawake wa mwanamume fulani … wazo tu lenyewe lilifanya
mwili wangu usisimuke. Hapana. Hakika kabisa nilijua kuwa sitaki kwenda kwenye
“mbingu” ya aina hiyo.
Mwaka
1981, nikiwa na miaka kumi na nane, nilifanya uamuzi wa kuolewa na binamu yangu
wa kwanza ili tu kuiridhisha familia yangu. Siku zote nilipenda kuwafurahisha
familia yangu, hasa baba yangu. Sikuwahi kwenda kwenye muziki wa dansi nikiwa
sekondari au kuwa na rafiki wa kiume, maana hayo yalikuwa kinyume kabisa na
matakwa ya baba yangu. Lakini miezi miwili tu baada ya kumaliza sekondari,
niliolewa. Hata hivyo, katika hali
inayokatisha tamaa, hata jambo hili halikuonekana kumfurahisha baba yangu.
Mwaka
1985 nilijiandikisha kwenda chuoni kinyume na mapenzi ya mume wangu na baba
yangu. Wao waliona kuwa sehemu yangu inapaswa kuwa nyumbani na jikoni ‘ambako
mwanamke anatakiwa kuwa.’ Kwa makubaliano kwamba nitafanya wajibu wangu wote wa
‘mke’ nyumbani, nilikubaliwa kuendelea na chuo.
Tayari nilikuwa na ujauzito wa mwanangu wa kwanza na wa pekee. Nilipata
mtoto mzuri wa kiume. Huenda haya yalikuwa na mashindano makubwa kabisa
maishani mwangu, lakini nilifanikiwa kumaliza kazi zangu za nyumbani na
kushinda tuzo mbili shuleni, nikawa mama, na hatimaye nilihitimu chuo.
Ninapotafakari sasa, najua kuwa niliyafanya hayo yote ili kumfurahisha baba
yangu, lakini bado haya nayo hayakuonekana kumfurahisha.
Ilikuwa
ni mwaka 1991 nilipokuwa kwenye safari ya kikazi pamoja na mume wangu. Alikuwa
ameanzisha biashara ya kuuza nguo kwenye maonyesho kwenye majimbo. Mume wangu,
mimi pamoja na rafiki yetu, ambaye nitamwita “John” ili kutunza usiri,
tulisafiri kwenye majimbo mbalimbali. Tulilala kwenye mahoteli na kufanya kazi
kwa saa 16-18 kwa siku.
Oklahoma
kilikuwa ni kituo chetu kinachofuata. Tulikuwa na saa 14 mbele yetu za kusafiri
kwa gari na ilibidi kuondoka harakaharaka ili kufika kule kwa wakati ili kuweka
kila kitu sawa kwa ajili ya maonyesho yale. Nilitamani kuwa na kitu cha kusoma
kwenye safari hii ndefu, lakini sikuwa na chochote na hatukuwa na muda wa
kusimama kwenye duka. Ili kuepuka kukaa tu kwa muda wote ule, niliamua kuchukua
Biblia ya kahawia iliyokuwa kwenye chumba cha hoteli tulikolala. Nilipofika mlangoni ili kuondoka, rafiki yangu
John alinisimamisha na kusema, "Amal, haujawahi kuiba kitu maishani mwako
na sasa unataka kuanza wizi, tena kwa Biblia? Hautafanya hivyo. Uko sawa?”
Nilicheka.
“John, hii ni Biblia tu. Hakuna mtu
atakayeona kwamba kuna kitu kimepungua. Hakuna mtu anayesoma vitu kama hivi. Na
hata hivyo, naiazima tu. Nitairudisha kwa njia ya posta.”
Kisha
John akasema, "Nilidhani wewe ni Mwislamu. Kwa nini unataka kusoma Biblia
ghafla kiasi hiki?”
Nikasema,
“Unajua, nina shauku tu ya kujua inasema nini na licha ya hivyo, hakuna kitu
kingine cha kusoma tutakapokuwa kwenye hii safari.”
Baada
ya kusema hayo, sote tukaingia kwenye gari na kuanza safari yetu ndefu. Tukiwa
garini, kwa takribani saa nzima, nikawa najisikia kuchoka tu. Nilikaa kwenye
kiti kidogo katikati ya John (aliyekuwa anaendesha) na mume wangu aliyekuwa
amekaa kwenye kiti cha abiria. Nilikuwa natazama kwa ushangao miali ya jua
lililokuwa linatua ilivyokuwa ikitoa rangi mbalimbali kwenye mawingu. Wakati
huohuo nikaanza kuimba wimbo nilioukumbuka wa utotoni … "Utukufu, utukufu,
haleluya, utukufu, utukufu, haleluya." Kisha nikaacha kuimba kwa kuwa
sikuweza kukumbuka maneno mengine. Tulikuwa tunapita mahali pazuri sana ambapo
nilimshukuru Mungu kwa kupaumba. Halafu nikaimba tena maneno yale huku nikiwa
sijui yana maana gani lakini kwa namna fulani, nilijua kuwa yanamwinua Mungu
kwa ajili ya uumbaji wake.
Kutokana
na kushindwa kukumbuka maneno yaliyobakia ya wimbo ule, nikaomba, “Mungu
nifundishe wimbo mpya wa kukuimbia wewe.” Niliyatazama mawingu huku nikiwaza
hakika atanijibu. Lakini ah, sikusikia sauti kama radi ikija kutokea mawinguni
kama ambavyo nilikuwa nikiwaza hivyo ndivyo Mungu anavyoongea. Ghafla, niliwaza
jinsi nilivyokuwa mpumbavu, maana nilifundishwa kwamba Mungu huwa hazungumzi na
yeyote. Niliitazama ile Biblia niliyokuja nayo ambayo ilikuwa miguuni mwangu na
nikaifungua. Nilikuwa nimeamua kuwa nitasoma ukurasa wowote nitakaofungua
kwanza. Na hiki ndicho nilichosoma:
Zaburi
108
wimbo au Zaburi ya Daudi.
wimbo au Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba,
nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu.
2 Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.
3 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
4 Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na
uaminifu wako hata mawinguni.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya
nchi yote uwe utukufu wako.
6 Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono
wako wa kuume, uniitikie.
7 Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami
nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na
Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,
9 Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia
Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.
10 Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma?
Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?
11 Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee
Mungu, hutoki na majeshi yetu?
12 Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa
binadamu haufai.
13 Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana
Yeye atawakanyaga watesi wetu.
Ilikuwa
ni ajabu sana, lakini nilihisi kuwa kwa namna fulani Mungu alikuwa akizungumza
na mimi kupitia kile nilichosoma. Kutokana tu na udadisi, nilitazama ukurasa
niliokuwa nikisoma. Nikakuta ni ukurasa wa 666. Ha! Nilifunga kitabu kile
haraka sana, maana nilikumbuka mafundisho yote kuhusu shetani na namba yake
666. "Hivi Mungu anataka kuniambia
kuwa kitabu hiki ni cha kishetani?" niliwaza.
Baada
ya kutafakari kwa muda, nilifikia uamuzi kwamba vitabu vyote vyenye kurasa
nyingi ni lazima viwe na ukurasa wenye namba hiyo. Huku nikijiona kama mjinga,
nilitupilia mbali wazo lile la kwamba Biblia ni kitabu cha kishetani.
Siku
chache baadaye kule Oklahoma, niliugua mafua makali sana. Nikawa najisikia
kizunguzungu na siwezi kutembea. Hivyo nilibakia kwenye chumba cha hoteli huku
mume wangu na John wakiwa kwenye biashara. Nilikuwa peke yangu nimelala
kitandani kwenye chumba hiki ambacho kilikuwa na mwanga hafifu. Nilianza kuwaza
mengi na jinsi maisha yangu yalivyo magumu. Nilikuwa sina furaha. Nilitamani
sana kumwona mwanangu maana nilikuwa sijamwona kwa mwezi mzima. Nami sasa
nilikuwa hapa eti kwenye “safari ya kibiashara.” Mume wangu hakuwa
mfanyabiashara mzuri sana. Kila wakati alikuwa ni mtu wa kutafuta mafanikio
yasiyopatikana. Nilipiga hesabu na kukuta kwamba kila siku tulikuwa tunapoteza
dola 400, lakini hata hivyo hatukuwa na uwezo wa kuondoka maana tulikuwa
tumefungwa na mkataba wa maonyesho yale.
Hili
pamoja na matatizo mengine maishani mwangu yalianza kupiga kelele ndani ya
kichwa changu. Niliamua kwamba, kama nikiendelea kuwaza juu ya matatizo yangu,
itakuwa hatari kwa afya yangu. Baada ya hapo nilikamata rimoti na kuwasha TV.
Nikawa natafuta chaneli ya sinema au nyingine ambayo ingenisahaulisha mawazo
yangu. Hata hivyo nilikuwa nimeshachelewa. Nikaanza kulia na kwa hasira
nilitupa ile rimoti kitandani na TV ikawa inabadili chaneli yenyewe. Sikujua imeshia kwenye chaneli gani maana
macho yangu yalijaa machozi.
Wakati naendelea kulia, nilimsikia
mtu kwenye TV akisema jambo kuhusiana na Yesu. Mara moja niliwaza, “Aha,
vizuri. Hicho ndicho ninachohitaji kwa sasa. Mmoja wa wale wahubiri wa kwenye
TV walio na wazimu.” Kutokana na kujihurumia, nililia hata zaidi huku huyu
mwanamume akiendelea kuzungumza. Alisema, “Unajisikia kuchanganyikiwa kwa
sababu una matatizo mengi.”
Huku nikiendelea kulia, nilikubali
na kusema, "Ndiyo, ninajisikia
kuchanganyikiwa na nina matatizo mengi sana."
Kisha akasema, "Unalia na
umekata tamaa."
Nami nikajibu kwa sauti, "Ndiyo,
ninalia na nimekata tamaa."
Ilikuwa ni hapo ndipo nilipoamua
kuinua macho yangu ili nione ni nani huyo aliyekuwa akiongea nami. Kwa hiyo
nilikaa kitandani na kuchukua tishu ili nifute machozi yangu niweze kumwona
vizuri huyo mtu kwenye TV. Ndipo alipaza
sauti akisema, "Hivi sasa umeshakaa!"
Nilianza kulia hata zaidi na kwa
sauti huku nikifunika uso wangu kwa mikono na kutikisa kichwa changu kulia na
kushoto.
"Ndiyo, nimekaa," nilijibu.
Kisha akasema, "Umeweka mikono
yako usoni kwa namna hii na unatikisa kichwa chako namna hii.”
Nilivuta pumzi ya ghafla na
nikakodoa macho kwa nguvu sana kwenye TV wakati mwanamume yule akiwa anaiga
vitendo nilivyokuwa navifanya. Sikuamini macho yangu. Alikuwa anaongea na mimi!
Kisha akasema kwa sauti ya juu huku
amenyoosha kidole chake moja kwa moja kwangu kupitia TV, “Mwanamke, Yesu ndiye
jibu lako! Njoo moja kwa moja kwenye TV yako!”
Bila
kujiuliza lolote niliruka kutoka kitandani na kukimbilia kwenye TV ambapo
nilipiga magoti mbele yake. Ukumbuke kwamba kabla ya hapa nilikuwa siwezi
kutembea lakini sasa kwa namna fulani niliweza kuruka kwa ghafla kiasi kile.
Akasema,
"Haraka, hakuna muda wa kupoteza. Weka mikono yako kwenye mikono yangu na
urudie nitakachosema.” Aliinua mkono wake na kuelekeza kiganja chake kwangu.
Nilipogusisha mkono wangu katika mkono wake kwenye TV, alisema, "Sasa
rudia baada yangu."
Ndipo
alianza kusema kile ambacho leo ninakijua kama “sala ya toba.” Kwa namna fulani
nilijua kutokea ndani yangu kwamba hii ilikuwa ni njia ya kuelekea kwa Mungu.
Alianza
kuongea harakaharaka huku mimi nikijaribu kuwa makini sana kwenye maneno
aliyosema.
Unajua,
kwenye Uislamu nilifundishwa kwamba kama nisiposema sala kwa usahihi, Mungu
hataipokea. Nilipoanza kurudia baada yake, kile ninachoweza kusema ni kuwa,
mwanga wa buluu ulipenya katikati kabisa ya kiganja changu kilichogusa skrini
ya TV. Mwanga ule ulipita kwenye mkono wangu, ukapanda mabegani, na kichwani,
na ukashuka miguuni lakini upande wa kulia tu wa mwili wangu. Kisha ukahamia
upande wa kushoto. Ilikuwa ni kama nguvu fulani iliyo nzuri.
Halafu
hii nguvu ya mwanga wa buluu ilianza kwenda kimzunguko ndani ya mwili wangu na
kuanza kukua ikitoka nje. Kisha ikaanza kumwagikia kwenye chumba kile ambacho
kilikuwa na nuru hafifu. Sikuwa na hofu hata kidogo na nilijua kuwa hili
lilikuwa ni jambo zuri. Lile duara la mwanga lilikua na kuwa kubwa na rangi
yake ikawa nyepesi hadi chumba chote kikajawa na nuru nyeupe.
Hisia
za upendo ambazo sikuwahi kukutana nazo zilinifunika. Nilijisikia niko salama.
Kwa namna fulani, nilijiona nimekuwa kitu kimoja na ile nuru. Nikajua wazi kuwa
huu ulikuwa ni wakati ambapo nimewahi kuwa karibu kabisa na Mungu kuliko wakati
mwingine wowote.
Kila
kitu kilipofikia mwisho, yule mwanamume wa kwenye TV alisema tupige simu kwa
namba iliyokuwa kwenye skrini kama mtu umesema ile sala. Mara moja nilinyanyua
simu na kupiga ile namba. Sauti tamu ya mwanamama iliitikia. Alinipongeza kwa
kumpokea Yesu moyoni mwangu. Nami nikasema, “Asante sana. Nilijua kuwa kuna
jambo zuri lingetokea kwangu leo. Unajua, ni kwa sababu nyota yangu ilisema
hivyo.”
Yule
mama akanijibu, "Sasa mpenzi wangu … kama Wakristo, sisi hatusomi nyota.”
Hili lilikuwa ni somo langu la kwanza. Alisema kwamba Mungu alitaka kunipatia
zawadi kwa kuwa sasa mimi ni Mkristo na akauliza kama ningependa kujua namna ya
kuzipata zawadi hizo.
"Bila
shaka ningependa," nilijibu huku akili yangu ikiwa inapiga picha ya boksi
zuri lililofungwa kwa utepe. Kwa kweli sikujua alichokuwa anamaanisha. Lakini
bado nilimpatia anwani yangu ili anitumie hiyo taarifa. Nilikata simu na kukaa
kitandani huku nikitafakari yote yaliyonitokea.
“Hivi
haya yalikuwa ya kweli? Ni nini hasa kilichotokea?” Mara moja Mungu aliniletea kumbukumbu
za siku moja miaka miwili nyuma. Nikakumbuka kwamba nilikuwa nikimlilia Mungu
kwa mateso huku nikiwa nimepiga magoti sakafuni nyumbani kwangu. Nikakumbuka
kuwa niliinua mikono yangu kuelekea juu na kumwambia Mungu, “Hivi wewe kweli upo? Kwa nini basi hunijibu kama upo?
Kwa nini maisha yangu yamejaa mateso kiasi hiki? Nataka wewe unijibu na si mtu
mwingine yeyote maana siwezi kumwamini mtu mwingine yeyote tena! Nataka
kukufuata wewe lakini sitaki kupoteza muda wangu kwenye dini isiyo ya kweli.
Nataka kuwa na uhakika. Nijibu tafadhali. Nijibu!”
Mungu
alikuwa akinikumbusha kuhusu maswali yangu kwake kwa namna iliyo wazi sana.
Ilikuwa ni kama skrini ya sinema mbele za macho yangu. Sasa nikajua kile
ambacho kilitokea punde. Mungu yeye mwenyewe alinijibu kwa namna yake ya ajabu.
Sifahamu
kama mwanga niliouona kwenye kile chumba siku ile ulikuwa ni kwa njia ya maono
au ulikuwa ni mwanga wa kweli. Ila ninachojua ni kwamba, kile nilichoona na
kusikia kilikuwa ni jambo halisi kabisa na kwamba hatimaye nilikuwa nimekutana
na Mungu mmoja wa kweli kwa namna ya pekee sana.
Siku
iliyofuata nilienda tena kwenye maonyesho. Huko nyuma, nilikuwa nimepata Biblia
ya buluu kwenye chumba cha hoteli ambayo ilikuwa inafanana kabisa na ile ya
kahawia niliyoichukua kwenye chumba cha mwanzo. Huku kwa siri moyoni mwangu
nikiwaza kwamba ile ya buluu itapendeza zaidi ikiwa chumbani mwangu,
nilibadilisha zile Biblia; nikachukua ile ya buluu.
Akili
yangu haikuwa kwenye kazi, bali kwenye Biblia na nilikuwa na shauku kubwa sana
ya kuisoma kuliko nilivyowahi kufanya. Pale mume wangu alipoondoka tu kwenye
banda letu, nilitoa ile Biblia yangu, huku nikiwa makini sana asije akaniona.
Nikaanza kusoma kitabu cha Mwanzo. Ha! Nilikuwa nasoma Biblia ileile lakini
sasa ilikuwa tofauti; ilikuwa na nguvu zaidi; na halisi zaidi! Niliipenda na
nikaendelea kusoma hadi nikajisahau kwamba nilikuwa niko kazini. Ghafla
nilisikia sauti ya mwanamume iliuliza, "Unasoma nini?" Nikiwa nimegutuka,
niliinua kichwa na kugundua kuwa kibandani kwetu kulikuwa na karibu dazani moja
wa watu. Lakini ajabu ni kuwa sikumsikia hata mmoja wao akija. Kwa aibu,
niliinua Biblia yangu kwa yule mwanamume na kumwonyesha maneno yaliyo kwenye
jalada kisha nikaiweka chini Biblia ile. Ghafla nilijawa na aibu na woga pale nilipowaza,
“Oh, kama baba yangu akiniona ninasoma Biblia atakasirika sana.” Kisha yule
mwanamume akauliza tena kwa sauti huku akiwa na tabasamu pana, "Unasoma
nini?"
“Hivi
huyu mwanamume hajui kusoma?” niliwaza, “Ana tatizo gani?” Kama kwa hasira,
nilijibu kwa sauti, “Biblia Takatifu!”
Ghafla,
watu wengine waliokuwa kwenye kibanda walianza kusema kwa sauti, mmoja baada ya
mwingine:
"Utukufu
kwa Mungu!"
"Amina!"
"Bwana
Asifiwe!"
"Haleluya!"
Niligeuza
uso kila upande huku nikitabasamu kwa watu hawa ambao walionekana kama vile
wanang’aa kwa nuru na wenye furaha sana.
Nikamgeukia
tena yule ambaye aliniuliza swali na nikamwuliza, "Nyie wote mko pamoja?"
"Hapana.
Mimi niko hapa na mke wangu tu," alisema huku akitoa tabasamu pana. Huku nikiwa
nimezidiwa na wingi huu wa wateja waliokuja ghafla, nikamwendea kila mmoja huku
nikimwuliza kama alikuwa anahitaji nimsaidie. Hakuna aliyekuwa anahitaji msaada
wowote, lakini kila mmoja alinitia moyo niende kuendelea kusoma Biblia yangu. Walikuwa
wote Wakristo! Kisha mwanamume mwingine aliyesimama pembeni yangu alisema, "Unaonekana kufurahia hicho unachokisoma."
"Ndiyo,
ni kizuri sana. Je, wewe umewahi kusoma kitabu hiki. Kwa kweli unatakiwa
kukisoma," nilisema.
"Ndiyo,
nimeshakisoma kitabu hicho na ni kizuri sana," alijibu.
"Wewe
ni Mkristo?" nikauliza.
Alitabasamu
na kusema, "Ndiyo, mimi ni Mkristo."
"Aha,"
nilisema kwa aibu. "Je, uko pamoja na yeyote kati ya hawa Wakristo
wengine?"
"Hapana,"
alisema.
Niliinuka
kutoka kwenye kiti changu. "Unasema kweli? Naweza kukuuliza swali kuhusu
Ukristo?" niliuliza.
Alinitazama
huku akitabasamu. "Unajua,” alisema, “Naweza nikawa wa msaada kwa kuwa hiyo
ndiyo kazi yangu. Mimi ni mtumishi na baba yangu ni mtumishi na babu yangu
alikuwa mtumishi na mwanangu naye anasomea utumishi. Kwa hiyo, jisikie huru tu
kuniuliza swali lolote kuhusu Biblia.”
“Aha,”
nikasema, “Nina tatizo moja. Unajua, jana ndipo nilikubali kuwa Mkristo na
nilichukua Biblia hii kutoka kwenye hoteli moja. Na sasa ninahofia kwamba Mungu
atakuwa amenikasirika sana kwa wizi.”
Alicheka
kisha akasema, “Umefanya vema sana kuwa Mkristo lakini hakuna tatizo kuhusu
hiyo Biblia kwa sababu hiyo ni Biblia ya Wagidioni. Watu hawa hutengeneza
Biblia na kuziweka kwenye vyumba vya mahoteli kwa ajili ya watu kama wewe. Kwanza,
huwa wanafurahi wanapokuta Biblia imechukuliwa. Na Mungu naye anafurahia sana
kwa kuwa unasoma Neno lake.”
Nilijawa
na furaha sana kwamba ningeweza kubakia na ile Biblia. Watu wote walipoondoka nilikuta kwamba
nimefanya mauzo makubwa kwa saa ile kuliko nilivyowahi kufanya kwa siku nzima
yoyote katika mwezi; na hayo yalitokea wakati nikisoma Neno la Mungu.
Kuanzia
ziku ile sikuwa na hofu au aibu tena ya kusoma "Biblia Takatifu." Mungu
aliwaleta Wakristo wote hawa ambao walikuwa hata hawajuani ili kunitia moyo. Je,
hili lilitokea kwa bahati tu? Hapana! Ilikuwa ni kazi ya Mungu mwenyewe!
Baada
ya kurudi nyumbani California, nilipokea kile kijitabu kwa posta chenye taarifa
za "Jinsi ya kuupokea zawadi kutoka kwa Mungu." Nilimkumbuka yule
mwanamke wa kwenye simu siku nilipoamua kuwa Mkristo. Ilikuwa ni jioni na
nilikuwa peke yangu chumbani. Nilifungua kile kijitabu na kuanza kusoma kuhusu “zawadi.”
Zawadi ya kwanza iliitwa kunena kwa lugha. Ilisema kwamba, omba ili Bwana aguse
kinywa chako kisha usubiri. Kwa hiyo, nilipiga magoti pembeni mwa kitanda changu
na kumwomba Mungu. Kisha niliinuka, nikakaa kitandani, nikafunga macho yangu na
kusubiri.
Baada
ya kama dakika 2-3, midomo yangu ilianza kusogea na kuunda sauti "O" kisha
sauti zingine na nikawa nazungumza maneno mbalimbali. Nilikuwa nazungumza lugha
ambayo zikuwahi kuisikia maishani mwangu. Ilikuwa inafurahisha.
Nilitazama
kijitabu tena na kusoma zawadi inayofuata kuwa ni "Tafsiri." Niliomba
tena na nikapokea zawadi ile. Kisha ikafuatia “Unabii” na kadhalika kwenye
orodha ile. Kufikia siku ya tatu, Mungu ambaye alikuwa mbali sana nami, akawa
sasa ni rafiki yangu mkubwa duniani kote. Jambo la kwanza kabisa ninalokumbuka
aliniambia ni kwamba alisema, "Amal, nakupenda." Nililia kwa siku 3
baada ya hapo kwa sababu nilikuwa najisikia sistahili upendo wake. Sikuelewa kwa
nini Yesu afe kwa ajili yangu. Nilikuwa sikuzoea aina hii ya upendo.
Siku moja nikiwa katika maombi,
nilimwuliza Mungu aniambie Roho Mtakatifu ni nani. Alinijibu kwa wazi kabisa, "1
Wakorintho 2: 12, 13, 14, 15, 16."
Nikasema, "Mungu, sielewi.”
Akarudia jibu lilelile na akaniambia
nifungue Biblia yangu. Nilikuwa sijawahi kusikia neno “Wakorintho” kabla na
nikawa najiuliza namba zile zote zinamaanisha nini. Lakini Mungu alinifahamu na
alijua kuwa nitafungua sehemu ya yaliyomo. Mara nilipaona na hiki ndicho
nilichosoma:
12 Lakini sisi
hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate
kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
13 Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa
kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya
rohoni kwa maneno ya rohoni.
14 Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei
mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa
kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.
15 Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala
yeye hatambuliwi na mtu.
16 Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana,
amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.
Baada ya kusoma hayo nikamwambia
Bwana, "Una maana kuwa Roho Mtakatifu ni Mwalimu wangu?"
Nikasikia Bwana akijibu waziwazi, "Ndiyo."
Ah, nilijawa na furaha sana. Kisha nikauliza,
"Roho Mtakatifu, una maana kwamba utanifundisha hii Biblia?"
Hapo tena nikasikia Bwana Mungu
akisema, "Ndiyo."
Hisia za joto na furaha zilinijaa
kiasi kwamba nilidhani nitapasuka. Unajua, nilikuwa siruhusiwi kwenda kanisani.
Baba yangu ambaye alishaachana na mama alishanikataa. Kaka zangu walikuwa
wanaona aibu kujihusisha na mimi na mume wangu naye alikuwa akinitesa kila
siku. Nilikuwa na ndugu wa Kiislamu ambao walikuwa wakinipigia simu kila siku
maana walikuwa wanataka kunifundisha Uislamu kwa uzuri zaidi. Lakini moyo wangu
ulishaamua na hakuna ambaye angeniambia kuwa kile kilichonitokea hakikuwa cha
kweli.
Mungu
huzungumza nasi! Mungu mwenyewe alinitunza, na kila nilipokuwa na swali,
aliniambia mahali pa kutazama kwenye Biblia. Mambo haya yaliendelea kwa miezi
mitatu. Siku moja aliniambia nikabatizwe kwenye kanisa lililokuwa kwenye eneo
letu. Kwa hiyo, kwenye siku ya kubatizwa, rafiki yangu "John", ndiyo,
yuleyule tuliyekuwa naye kule Oklahoma, aliomba twende wote. Alisema kwamba hakuwahi
kabla kushuhudia “Ubatizo wa Kikristo.” Wakati wa ubatizo, John alishikilia
taulo yangu na Mchungaji alidhani kuwa naye alikuwa pale ili kubatizwa. John alimwambia
Mchungaji kuwa, alipanga kuokoka kwanza wakati wa ibada. Nilishtuka sana
kusikia kile kilichotoka kinywani mwa John. Kisha palepale aliongozwa sala ya toba
na akabatizwa pia.
Nilifurahi
sana kwa sababu rafiki yangu naye amempata Mungu. Hadi leo ninamwamini Yesu
Kristo kama Bwana na Mwokozi wangu. Na mbingu, ndiyo, nataka kuwa mbinguni
pamoja na Yesu ambako nitamsifu rafiki yangu mkubwa kabisa kuliko wote duniani.
Yeye ni Mungu Baba yangu na ni Yeye ndiye najitahidi kumpendeza leo.
Ilichukua
miaka miwili kwa Mungu kunijibu na ulikuwa ni muda sahihi kwake.
Unaweza
kuwa umemaliza kusoma ushuhuda huu sasa na huenda unajiuliza endapo haya ni
mambo ya kweli. Ninakuhakikishia kwamba, nisingehangaika kupoteza muda wangu
kuandika haya kama yasingekuwa ya kweli. Yesu Kristo ndiye jibu. Yeye ni Mungu!
Katika
utumishi kwa Bwana wangu,
Amal.
***********************
Haya
ndugu msomaji. Umemsikia dada huyu, Amal. Kwa nini usifanye kama alivyofanya
yeye? Najua unayo shauku ya kwenda mbinguni baada ya hapa. Yesu peke yake ndiye
njia ya kwenda mbinguni. Lakini wewe umefundishwa kwamba Yesu ni mtume tu na ni
mwanadamu kama sisi na si Mungu wala si Mwana wa Mungu.
Hebu
fanya kama Amal alivyofanya. Aliomba maombi ya kutoka ndani kabisa ya moyo wake. Alimwomba
Mungu Muumba mbingu na nchi. Hiki ndicho alichomwabia Mungu:
“Hivi wewe kweli upo? Kwa nini basi hunijibu kama upo? Kwa nini
maisha yangu yamejaa mateso kiasi hiki? Nataka wewe unijibu na si mtu mwingine
yeyote maana siwezi kumwamini mtu mwingine yeyote tena! Nataka kukufuata wewe
lakini sitaki kupoteza muda wangu kwenye dini isiyo ya kweli. Nataka kuwa na
uhakika. Nijibu tafadhali. Nijibu!”
Si lazima useme maneno hayohayo, lakini cha msingi ni kusema
kile hasa ambacho moyo wako unakitaka. Wewe mwenyewe ni shahidi juu ya hali ya
moyo wako katika jitihada zako zote za kujaribu kumpendeza Mungu. Nina uhakika kuwa hujafanikiwa hata kidogo. Nje ya Yesu ni maisha magumu, mazito, na yasiyo na tija. Sema naye
leo. Mwambie Mungu mwenyewe akuthibitishie kama Yesu ndiye kweli njia ya kwenda
mbinguni. Atakujibu!
Waweza pia kuusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza kwa kubofya
HAPA.
Pia unaweza kuwasiliana nami [blogger] kupitia:
Mungu akubariki.
No comments:
Post a Comment