Friday, March 15, 2013

Majibu Yangu kwa Ibrabura - Sehemu ya 1
Katika makala haya, ninajibu hoja zako rafiki yangu Ibra, ambazo umezitoa kwenye sehemu ya ‘comments’ kwenye makala yangu mengine yenye jina:  Je, Yesu aliagiza wafuasi wake wawaue maadui wa Yesu? Unaweza kusoma HAPA.


Ninatoa majibu yangu kama makala tofauti kwa sababu kuu mbili. Kwanza ni kuwapa fursa watu wengine waweze kujifunza kutokana na mjadala wetu na hata kuchangia au kutusahihisha pale tunapokosea. Pili, kutokana na urefu wa majibu yangu, ni rahisi kuyatoa kama makala kuliko maoni (comments), maana maoni ya mara moja hayatakiwi kuzidi herufi takribani 4,000 hivi.


Asante sana Ibra kwa maoni yako na changamoto unazonipatia. Lazima nikiri kwamba haimaanishi kuwa ninayo majibu ya kila kitu, lakini wakati mwingi inanibidi nifanye utafiti ili kupata majibu sahihi, maana Biblia ni kubwa na mimi kama mwanadamu, siwezi kujidai kwamba ninajua kila kitu ndani yake. Hata hivyo, tunaye Mwalimu mwema na mwaminifu, ambaye ndiye mwandishi mwenyewe wa Biblia, yaani Roho Mtakatifu – huyu anakuwa ndiye mwenye majibu sahihi. Na kila wakati Yeye ni mwaminifu na anatuwezesha kupata majibu.

Katika maoni yako, Ibra, umesema mambo kadhaa kama ifuatavyo:

Ibra unasema:
Mr.James! Mi nahisi wewe umeshindwa kabisa kulitetea kanisa. Nasema hivyo kwa sababu unakataa na kuniona mimi ni muongo kwamba wewe hujasema kuwa yesu ni mungu. Sasa huu ni ushahidi wa kile ulichokiandika katika ''Je, Muhammad ametabiriwa kwenye biblia sehemu ya pili'' kwenye kurasa za comments.

James John February 12, 2013 at 3:58 PM
Kuhusiana na kwamba Muhammad alitumwa kwa watu wote, hilo nalo silikatai hata kidogo. Ni jambo la kweli pia. Lakini swali la msingi ni kwamba, je, katumwa na nani? Mungu wa Biblia anaitwa Yehova, au Yesu Kristo, au Roho Mtakatifu. Ukiniambia kwamba huyu ndiye aliyemtuma Muhammad, hapo ndipo nitakwambia bila kumung’unya maneno kwamba jibu ni HAPANA!

Ibra, kabla ya yote niseme kwamba ‘kutetea kanisa’ hiyo ni ‘concept’ ya Kiislamu si ya Kikristo. Ninyi ndio mna mambo ya kutetea dini. Sisi hatujaitiwa kutetea dini. Tumeitwa kuitafuta kweli na kuishi katika hiyo. Kutetea dini au kanisa ni sawa na mtu aliyenunuliwa zawadi ya thamani kubwa sana iliyofungwa ndani ya boksi zuri sana. Lakini badala ya kuchukua zawadi, anang’ang’ania boksi. Dini au kanisa ni boksi la kubebea Kweli ya Mungu. Kweli ndiyo zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu. Na Kweli ni Yesu (Yohana 14:6).

Nikirudi sasa kwenye hoja yako Ibra, ni wapi ambako nimesema kuwa Yesu si Mungu? Yesu ni Mungu kabisa kabisa aliyeumba mbingu na nchi na vitu vyote. Isaya alipotabiri miaka mingi nyuma kuhusiana na kuzaliwa kwa Yesu Kristo, anasema hivi: Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. (Isaya 9:6).

Yesu ni mtoto (Mwana wa Mungu) na ni Baba (yaani Mungu Baba). Kwa hiyo, hakuna mahali ambapo mimi nimesema kuwa Yesu si Mungu. Najua kuwa, kama nilivyosema kwenye jibu jingine, ninyi Waislamu mnachukua tabia za kibinadamu kisha mnamtwika Mungu tabia hizo, halafu mnatengeneza majibu kutokana na tabia hizo mlizompa. Mathalani, kwa kuwa mwanadamu hawezi kuwa baba na mwana, au hawezi kuwa hapa na kule kwa wakati mmoja, basi mnahitimisha kuwa hata Mungu naye hawezi kufanya hivyo. Kwa hiyo Ibra ndugu yangu, Yesu ni Mungu wala katika hili sina konakona hata kidogo. Sijasema kokote kwamba Yesu si Mungu.


Ibra anasema:

Mr.James unaposema Mungu wa biblia anaitwa yehova au yesu au roho mtakatifu inamaanisha ni kitu kimoja hiko hiko. Acha kuwa na kauli mbili mbili, thibitisha kitu, watu wakuelewe ili waweze kufaidika na kile unachokifundisha. Usiwe mjanja mjanja, mungu kaua unasema yesu sio mungu ni mtume tu. Mungu kaleta upendo, unasema yesu mungu, nikuelewe vipi? Mr.James, mistari ya biblia niliyokutolea nimekuthibitishia kwamba, Mungu pekee ndio mwenye uwezo wa kuua. Kwa nini ushangae kuuwawa kwa watu kwenye islam na haushangai kwenye biblia? Kuua kwa Yesu au Kutokuua, kukata viungo vya wanadamu ndani ya biblia, haimaanishi hukumu hiyo haikuwepo kwa sababu hata muhammad hajawai kuua bila agizo la mungu kwa wanadamu inasema hivyo.

Ibra, kuhusu Mungu kuua, unajua fika kuwa mimi sijakukatalia. Kimsingi, nimekupa hata andiko linalokubaliana na jambo hilo. Mungu anasema katika Biblia: Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; naua mimi, nahuisha mimi, nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu (Kumbukumbu 32:39).

Ila kuhusu Yesu kuwa mtume tu, hapo sasa unanisingizia rafiki. Hilo si neno ninaloweza kusema mimi kamwe!

Ni kweli kabisa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ni Mungu huyohuyo mmoja. Lakini kumbuka kwamba, kulingana na Quran, inaonekana kuwa Mungu anajidhihirisha katika nafsi moja tu. Bali kulingana na Biblia, Mungu anajihidhirisha katika nafsi tatu.

Na nilichosema ni kuwa, alipojidhihirisha katika nafsi ya pili, yaani kama Mwana, hakuna sehemu hata moja ambapo anaagiza mwanadamu amuue mwanadamu mwenzake. Sababu yake ni rahisi tu – wewe unamuua mwenzako kwa sababu ametenda dhambi ya wizi, uzinzi, n.k. Basi, ukishamaliza kumuua, na wewe tega shingo yako uuawe maana, bila shaka, unazo dhambi za kwako pia, hata kama si sawa na za yule unayemuua.

Na sababu ya hali kuwa hivi, nikakwambia, Mungu ameweka maisha yetu katika hatua. Kwanza, kilikuwa ni kipindi kabla ya sheria (torati), ambapo watu walitenda dhambi lakini hawakujua kuwa ni dhambi, maana hakukuwa na sheria. Pili, ni kipindi cha wakati wa sheria (torati) ambacho lengo lake HASA si kumfanya mwanadamu awe mtakatifu, bali ni kumwonyesha jinsi alivyopungua mbele ya utakatifu wa Mungu; na jinsi ambavyo anahitaji msaada wa Mungu ili kutoka kwenye uchafu na utumwa wa dhambi na kuingia kwenye utakatifu. Kazi hii ya kusafisha mioyo ni kazi anayoweza kuifanya Mungu peke yake.

Ndiyo maana andiko nililonukuu hapo juu linasema: naua mimi, nahuisha mimi, nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu.

Hakuna wokovu kwa juhudi za kibinadamu. Ukijidanganya kwamba wewe utashika sheria za Mungu ZOTE ili uokoke, kwa hiyo bidii yako, umepotea! Hauponi katu!

Ngoja nikupe mfano. Mzee Musa ni hakimu wa mahakama. Mtoto wake anaitwa Samweli. Samweli aliiba, akakamatwa na kushitakiwa. Kesi ilisimamiwa na hakimu Musa. Samweli alifungwa miaka 7 gerezani. Je, Samweli akiulizwa, ‘Umehukumiwa na nani?’ anatakiwa atoe jibu lipi sahihi kati ya haya?  A). Nimehukumiwa na baba. B). Nimehukumiwa na hakimu wa mahakama. C). Nimehukumiwa na Mzee Musa.

Bila shaka jibu sahihi ni B. Lakini kwa nini lisiwe A au C wakati hakimu wa mahakama ni baba na ni Mzee Musa? Ni suala la mandhari husika; ni suala la muktadha; ni suala la nafasi husika; ni suala la majira na nyakati. Wakati anapokuwa nyumbani ni baba yake; lakini akiwa mahakamani si baba yake, bali ni hakimu wa mahakama. Sasa wewe ukiniambia kwamba, “Hapana. Acha ujanjaujanja. Kuwa wazi. Mara useme ni baba, mara useme ni hakimu, mara useme ni Musa. Tukueleweje?” Hapo unategemea nikuambieje, Ibra? Siwezi kukuambia jambo tofauti na hali halisi. Wewe unataka jibu lifanane na mtazamo wa Quran. Lakini hiyo siyo hali halisi. Hiyo siyo Kweli.

Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo anadhihirika katika nafsi tofauti kutegemea na nafasi gani unayoongelea. Katika nafasi ya kutamka wakati wa uumbaji, kwa mfano, hapo alikuwa Baba. Katika nafasi ya kuwa Mkombozi wa wanadamu, hapo alikuwa Yesu (au Mwana). Na katika nafasi yake sasa hivi duniani, Yeye ni Roho Mtakatifu. Lakini ni Mungu yuleyule. Ni Mzee Musa yuleyule; ni hakimu wa mahakama yuleyule; ni baba yuleyule.

Ndiyo maana nikasema, akiwa kama Mwana, yaani Yesu Kristo, hajawahi hata mara moja kuagiza mwanadamu mmoja amuue mwanadamu mwingine. Kipindi hicho cha kuua watenda dhambi kwa kuwapiga mawe, n.k. kilikuwapo, lakini kilishapita. 


Ibra unasema:
Yesu hakuja kuzifuta sheria bali kutumikia. James, mi nina wasiwasi juu ya imani yenu nyie wakristo mnamfuata nani? Na kama mnamfuata yesu, mbona hamwenendi katika njia zake?

Ibra, sisi tunamfuata Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo, maana Yakobo alikuwa na wana wa kiume kumi na mbili. Na mmoja wao alikuwa Yuda. Na kupitia Yuda, alizaliwa Yesu.


Ibra unasema:

Matayo 5:17-20
17 Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.
18 Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie.
19 Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
20 Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

Sijui unaelewa nini ndugu yangu Ibra kuhusiana na maandiko hayo katika Mathayo 5:17-20? Hata hivyo, kutokana na mtiririko wa mawazo yako yote, bila shaka unalenga kuonyesha kuwa tunatakiwa kuishi kadiri ya torati isemavyo. Na mantiki yako ni kwamba Quran, kwa kuwa inasisitiza sana mambo ya sheria zilizo katika torati, basi hiyo ndiyo yenye ujumbe sahihi, au siyo?

Lakini, kama kawaida, tuangalie maandiko kwa ukaribu na kwa makini. Bwana Yesu hasemi kuwa alikuja kuishi sawasawa na torati isemavyo neno kwa neno (literally). Mstari wa 18 unasema: Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie.

Maana ya aya hii ni kwamba, tangu zamani, torati ilikuwa ina madai kadhaa juu ya wale walioletewa. Kwa kuwa torati waliletewa wenye dhambi – yaani wanadamu wote – maana imeandikwa:

… sheria haimhusu mtu wa haki, bali waasi, na wasio wataratibu, na makafiri, na wenye dhambi, na wanajisi, na wasiomcha Mungu, na wapigao baba zao, na wapigao mama zao, na wauaji, na wazinifu, na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo; na likiwapo neno lo lote linginelo lisilopatana na mafundisho yenye uzima (1 Tomotheo 1:9-10).


Na madai yote ya torati yanajumuika kwenye neno hili: Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. (Warumi 6:23).


Maana yake ni kwamba, kwa kuwa wanadamu wote ni wenye dhambi (jambo hili ninalisema tena na tena maana ni muhimu sana kulielewa, si tu kwa sababu maandiko yanasema hivyo, lakini pia unaweza kujipima wewe binafsi na utaujua ukweli).


Na kwa sababu torati ni ya kutoka kwa Mungu, ili uweze kuokoka ni lazima uitimize, si kwa asilimia 95 au hata kwa 99, bali kwa asilimia 100 – kama ukiweza! Maana imeandikwa: Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo. (Warumi 10:5). Ukiweza kuitimiza, unaingia mbinguni moja kwa moja, bila shaka yoyote. Lakini ukitenda dhambi mia, mshahara wa dhambi ni mauti! Ukitenda dhambi moja, mshahara wa dhambi ni mauti!


Sasa, kwa kuwa dhambi mwisho wake ni mauti, ina maana kuwa wanadamu wote tulitakiwa kuishia jehanamu. Lakini tangu mwanzo Mungu alishaahidi ukombozi kwa mwanadamu. Unaweza kusoma HAPA.


Ndipo sasa Bwana Yesu anasema kwenye mstari wa 17: Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, ... Maana ya neno ‘tangua’ kulingana na Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI, 1981) ni ‘vunja kanuni au maafikiano, batilisha.’ Kwa maneno mengine, anachosema Bwana hapa ni kuwa, msidhani nimekuja kubatilisha yale ambayo torati inayataka; au sikuja kuwaambia kwamba achaneni na torati mfuate mambo mapya mengine. Hapana! Badala yake anamalizia kwa kusema: bali kutimiliza.


Nimekuambia hapo juu kuwa torati ilikuwa na madai mengi dhidi ya wenye dhambi kama wanataka kuokolewa na mauti ya jehanamu. Kwa maana nyingine ni kuwa torati ilikuwa ni hukumu juu ya kila mwanadamu kwa kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuitimiza. Torati ilikuwa inasema juu ya kila mwanadamu, “Huyu amevunja sheria hii na hii na hii. Hawezi kuruhusiwa kwenda mbinguni. Anatakiwa kutupwa jehanamu.”


Sasa, hapa Bwana Yesu anasema: Nimekuja kuyatimiza au kuyalipa au kuyatekeleza masharti na madai hayo ili pale ambapo torati ilikuwa ina madai dhidi ya wenye dhambi, yaani wanadamu wote, kusiwepo madai tena; maana mimi ninawapenda hawa wanadamu; sitaki waangamie!!

Kama James anadaiwa shilingi laki moja na Ali na yeye ni hohehahe kabisa hawezi kulipa hata elfu tano, halafu Ali akasema, "James, usiwe na wasiwasi nimekusamehe deni lako," hapo Ali anakuwa ametangua deni hilo. Lakini kama atatokea Musa akasema, "Ali chukua laki moja hii hapa kwa ajili ya deni la James," Musa hajabatilisha, bali ametimiliza kile kilichokuwa kinadaiwa.

Lakini utamfikiriaje James kama baada ya Musa kulipa deni, yeye atasema, "Amelipa wapi bwana. Mimi nitahangaika mwenyewe"? Bila shaka kila mtu atajiuliza iwapo huyu James anajipenda au la. 

Hiki ndicho ambacho Mwokozi Yesu amefanya. Badala ya kusema tu kwamba, "Wanadamu wametenda dhambi kwa hiyo wasamehe tu," aliamua kuja kutimiliza kila dai ambalo torati ilikuwa nalo juu ya mwanadamu huyu mwenye dhambi; ambaye hana hata chembe ya uwezo wa kuishi sawasawa na torati yote. Lakini Ibra na Waislamu wenzako mnasema, "Hamna bwana, tutahangaika wenyewe hivyohivyo." Ajabu ee? Unakataa uhuru, unachagua utumwa!!!!  Haya.

Ninyi ndugu zangu Waislamu, kama kawaida, kwa kuwa lengo lenu hasa si kuitafuta kweli, bali ni kutafuta kuhalalisha Quran, basi mnasaka namna ya kuifanya Biblia iendane na kile Quran inachosema. Kwa hiyo, ninyi mnadhani kuwa hapa Bwana Yesu anaongelea mambo yenu yaleee ya kunawanawa, kufuga ndevu, kupiga watu mawe, n.k. ambayo yamo kwenye torati. Mafarisayo nao walikuwa wanasisitiza hayo hayo. Walikuwa wanasema kuwa ukitaka kwenda mbinguni, basi ni lazima uishi (literally) kama torati isemavyo.

Hivi ndivyo Neno la Bwana lisemavyo kama nilivyokunukulia hapo juu: Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo. (Warumi 10:5).  Yaani haki ya kuitwa mwana au mtakatifu wa Mungu; haki ya kuingia peponi; haki ya kupona jehanamu inatokana na kuishi sawasawa na torati kwa asilimia 100 – kama ukiweza! Kama ukiweza!


Nimalizie basi na mstari wa 20. Bwana Yesu akasema kwa wale ambao wako tayari kuishi kwa utimilifu wa torati unaopatikana ndani yake Yeye Yesu kwamba: Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Haki ya waandishi na mafarisayo ni ipi? Ni hiyo ya kutaka kutimiza torati inayotajwa kwenye Warumi 10:5. Ni ile haki iliyo ndani ya Quran pia.


Sasa, haki ya wafuasi wa Yesu itazidi namna gani haki ya mafarisayo? Bwana Yesu, kwa kuwa Yeye ni Mungu, aliishi hapa duniani bila kutenda dhambi yoyote. [… bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi (Waebrania 4:15).] Hivyo, torati haikuwa na hukumu wala madai yoyote juu yake. Lakini badala yake, Yeye alibeba hukumu yote ya torati dhidi ya wanadamu wote – yaani ile isemayo: Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Kisha akauawa kama torati inavyodai. Hapo akawa, hajaitangua, bali ameitimiza torati. Yaani, aliipatia kile ilichokitaka.


Mimi sasa, na wewe, na mwanadamu mwingine yeyote, badala ya kujidai kwamba tuna uwezo wa kuitimiza torati, tunachotakiwa kufanya ni kuamini TU kwamba Yesu alibeba dhambi zangu, alikufa kwa niaba yangu, alifufuka kwa ajili yangu, ninampokea kwa imani kama Bwana wangu na Mwokozi wangu. Simple! Thank you Jesus!!!!!!


… kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu (Warumi 3:20-24)


Torati ni mzigo wa mawe usiobebeka kwa mwanadamu. Sasa ametokea mtu kwa upendo wake ameamua kubeba mzigo huo kwa niaba yako. Lakini wewe bado unang’ang’ania kusema, “Niacheni. Nitaubeba tu,” wakati huwezi. Hicho ni kiburi mbele za Mungu. Unadhani utaweza kununua pepo kwa bidii yako?


Tofauti kubwa kati ya Biblia na Quran ni hii: Kulingana na Biblia, mwanadamu anaokolewa kutokana na kile ambacho Bwana kwa upendo wake, amefanya kwa ajili yetu. Kulingana na Quran, mwanadamu anaokolewa kutokana na kile ambacho anamfanyia Mungu wa Quran (ambacho of course, hamkiwezi, na mnajua fika kwamba hamjaweza, hamuwezi na hamtaweza).

Mungu wa Biblia ni Baba anayetoa na kutoa na kutoa; lakini Mungu wa Quran ni Baba anayedai na kudai na kudai.

Tafakari.

Hoji mambo.

Jipime.

Chukua hatua. 


Asante tena Ibra. Bwana Yesu akubariki. Naamini utafika wakati ambapo pazia litaondoka na kila kitu kitaonekana wazi.

Bado sijamaliza kujibu swali lako kuhusiana na Yeremia 8:8. Nitakujibu katika sehemu ya 2 ya makala haya.


*******************


Lakini pia, bado nasubiri kwa hamu majibu ya maswali yangu ambayo nimeyauliza HAPA na nilikuomba Ibra unijibu lakini haujafanya hivyo. Natumaini unayafanyia kazi.

4 comments:

 1. Mr. james, kabla ya kuendelea na mjadala wetu, ningependa kukushauri ya kwamba, ule ukurasa wenye mada tunayotolea maoni, usibadilishe na kutengeneza kitu kingine kwa sababu wale wanaofuatilia majadiliano yetu watashindwa kupata ukweli wa mambo. Tafadhali sana Mr!
  Mr.James, mi naona sasa nikubaliane na wewe ya kwamba kuna mungu wa biblia na mungu wa qur'an.
  Sasa mungu wa biblia, kwa mujibu wa maandiko yaliyotolewa, kwenye kurasa za nyuma, inaonyesha ametoa maagizo ya kuwauwa binadam na pia mungu wa qur'an, ametoa maagizo ya watu kuhukumiwa kwa kifo na mambo mengine (kama vile, kukatwa viungo kwa yale makosa madogo madogo) je, huoni kama miungu hii inafanana kwa tendo hili?

  Kwa nini wewe unaegemea sana upande wa qur'an kwamba ndio yenye makosa?
  Mr.James, katika mafundisho yako yote, yana misingi ya kibinadamu sio ya mungu. Kama unakumbuka niliwahi kukuonya juu ya maneno ya binadamu kupitia Yeremia 23:14-16 (14 Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.
  15 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.
  16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.)
  Natoa madai haya kwa sababu, uaminifu wako wote ambao ni tegemezi, unatokana na maneno ya Paulo na unaachana na maneno ya yesu aliyofunuliwa na mungu.
  Mimi nimejaribu sana kutoa ushahidi wa kile ninachodai kwa maandiko, lakini wewe unakuja kwa kupinga kutumia maneno ya wanadamu ambae mungu anakataa.
  Nikakupa pia Mithali 30: 5 (Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.
  6 Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.)
  Kwa madai ya andiko hili nemeona kwa watu hawa wawili ( Yakobo ndugu yake Yesu na Paulo ambaye amewahi kushirikiana na shetani katika kuwajuza watu wamjue mungu) kama ifuatavyo:
  warumi 3:28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
  Hapa paulo anadhihirisha hivyo.
  Yakobo 2:14-26 14 Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa?
  15 Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki,
  16 na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?
  17 Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.
  18 Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
  19 Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.
  20 Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?
  21 Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu?
  22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.
  23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.
  24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.
  25 Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?
  26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo mekufa

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ibra asante kwa ushauri juu ya kutobadilisha ukurasa wenye makala ambayo ndiyo tunaitolea maoni. Nimekubaliana nawe juu ya hilo. Hata kama nitaandika kitu kutokana na mijadala hii, hicho kitakuwa ni cha jumla tu lakini majibu ya hoja yatakuwa ndani ya makala inayohusika.

   Kwamba unakubaliana na mimi kuwa kuna Mungu wa Biblia na Mungu wa Quran, naamini huo ni mtazamo sahihi kabisa maana haiwezekani kusema kuwa vitabu hivi vinatokana na Mungu mmoja ukivitazama kwa ujumla wake – licha ya kufanana hapa na pale.
   Nikikunukuu maneno yako, unasema kwamba, “Sasa mungu wa biblia, kwa mujibu wa maandiko yaliyotolewa, kwenye kurasa za nyuma, inaonyesha ametoa maagizo ya kuwauwa binadam na pia mungu wa qur'an, ametoa maagizo ya watu kuhukumiwa kwa kifo na mambo mengine (kama vile, kukatwa viungo kwa yale makosa madogo madogo) je, huoni kama miungu hii inafanana kwa tendo hili?”
   Ibra, nakubaliana kabisa na wewe juu ya hili.
   Lakini umeniuliza kwamba: “Kwa nini wewe(yaani mimi) unaegemea sana upande wa qur'an kwamba ndio yenye makosa?”
   Rafiki yangu Ibra, ambacho nimekuwa nikisema mara zote ni kuwa, Mungu wa Biblia ana ratiba ambayo inatokea zamani kabla ya torati kuletwa, ikapita kipindi cha torati, na sasa iko kwenye kipindi ambacho kinaitwa cha neema. Kipindi cha torati kilikuwa cha kuhukumu dhambi papo kwa hapo. Lakini kipindi cha neema ni kipindi kinachodhihirisha huruma, upendo, uvumilivu na rehema za Mungu. Torati ililetwa kupitia Musa kwenye Mlima Sinai. Lakini hivi ndivyo humohumo kwenye torati Mungu anamwambia Musa kuwa: Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. (Kumbukumbu 18:18). Nabii huyu ni Yesu kama ambavyo nimeeleza wazi kwenye makala yangu yenye kichwa: Je, Muhammad Ametabiriwa Kwenye Biblia – Sehemu ya 2.
   Kwa kuwa unataka kuonyesha kana kwamba Mungu wa Biblia aliyeamuru kuuawa kwa wanadamu wenye dhambi ndiye huyohuyo Mungu wa Quran anayeamuru wenye dhambi wauawe, basi inabidi uamini kila anachokisema. Usiishie tu kuchukua yale unayoyataka tu wewe. Chukua yale anayoyataka Yeye.

   Sasa huyu Mungu wa Biblia aliyefanya agano na Israeli na kuwapatia torati, kwa kuwa Yeye ni Mungu mwenye ratiba inayofuata majira na nyakati, alikuja kusema kupitia nabii Yeremia, maneno yafuatayo:
   Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena. (Yeremia 31:31-34).

   Hapo ilikuwa ni miaka mingi kabla ya kuja kuja kwa Bwana Yesu. Bwana Yesu alipokuja sasa, hivi ndivyo alivyosema pale alipokuwa kwenye karamu yake ya mwisho na mitume wake kabla tu ya kuondoka duniani na kurudi mbinguni:
   Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. (Mathayo 26:27-28).

   Yohana anafafanua zaidi kwa kusema: Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo (Yohana 1:17).

   Kwa hiyo rafiki yangu, Ibra, Quran ina makosa kwa sababu iko nyuma ya wakati wa Mungu. Haitambui kuwa Mungu alishatoka kule siku nyingi.

   Delete
  2. Ibra umerudia tena kwa mara nyingine kunikumbusha juu ya maonyo uliyonipa kwamba nisiwe nabii wa Uongo. Na kati ya maandiko uliyoninukulia ni [ambacho ni kitu cha ajabu sana] ni Yeremia huyohuyo ambaye hapo tu juu nimekuonyesha akizungumzia kuhusu agano jingine tofauti na lile la Musa. Na umenukuu Yeremia 23:14-16. Na mstari wa 16 unasema kwamba: Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.
   Sasa, kati ya mimi na Muhammad, ni nani nabii wa uongo? Maana umemnukuu Yeremia; na Yeremia anasema kuwa kutakuwa na agano jingine. Na mimi ninakubaliana na Yeremia kwa kukuonyesha jinsi ambavyo agano limekuwa si la kukata watu mikono na shingo bali ni la kurehemu na kusamehe kupitia Yesu Kristo. Sasa je, Muhammad anakubaliana na hicho anachosema Yeremia? Bila shaka hakubaliani. Sasa kati ya yeye na mimi, yupi ni nabii wa uongo?
   Huoni kwamba hilo onyo ulilonipatia mimi linakugeukia wewe?
   ……………………………………….
   Pia unasema kuwa uaminifu wangu wote unategemea maneno ya kibinadamu ambayo wewe unamaanisha kuwa ni maneno ya Paulo. Si kweli. Mimi nategemea Neno la Mungu. Hakuna jambo lolote ambalo Paulo amewahi kusema lililo kinyume na maagizo ya Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Kila kitu anachosema kinaendana sawasawa na mtiririko wa majira na nyakati za Yehova. Kwa kuwa unatoa maneno ya jumla sana, nitaweza kukupa ushahidi kama ukinionyesha mfano ‘specific’ juu ya kile unachoita ni maneno ya kibinadamu ya Paulo.

   Delete
  3. Jambo jingine uliloongelea Ibra ni kile ambacho wewe unadhani ni mkanganyiko kati ya Paulo na Yakobo.
   Paulo anasema: Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria. (Warumi 3:28). Na Yakobo anasema katika Yakobo 2:14-26 kuwa imani pasipo matendo haina faida.
   Bila shaka hapa wewe unavutiwa na Yakobo kwa sababu unadhani kuwa anakubaliana na Quran. Lakini hebu sikiliza Ibra.
   Paulo anazungumzia juu ya kupewa haki ya kuwa mtakatifu wa Mungu; haki ya kuingia mbinguni; haki ya kuokolewa. Kwenye makala ya jana niliongelea sana jambo hili, japo haikuwa kwa mtazamo wa kujibu swali hili.
   Tunapoongelea kuhusu kuokoka na kwenda mbinguni, Uislamu unafundisha kuwa mwanadamu atende matendo mema mengi kadiri iwezekanavyo kwa sababu eti, Mungu atakuwa na mizani siku hiyo. Matendo yako mema yakiwa mazito kuliko yale mabaya, basi unaingia mbinguni. Lakini mabaya yakiwa mazito zaidi, basi moto wa jehanamu ni wako.
   Sasa, Paulo anaongelea jambo linalohusiana na hilo. Wayahudi washika torati nao walidhani kuwa mwanadamu anaokolewa kwa njia ya kutenda matendo mema kama anavyowafundisha Muhammad. Na kama hivyo ndivyo ambavyo ingekuwa, basi Yesu alipoteza tu muda wake kuja kutoa uhai wake [Hapa naongelea Yesu aliyezaliwa kwenye hori la ng’ombe ambaye alikufa; siongelei Isa aliyezaliwa chini ya mtende ambaye hakufa].
   Ndipo sasa Paulo anasema kwamba, kama wewe unadhani kuwa matendo yako mema yatakuokoa, basi jua kuwa umepotea tayari.
   Lakini Yakobo anaongelea juu ya mtu ambaye tayari ameshapokea wokovu wa Bwana Yesu kwa imani jinsi anavyotakiwa kudhihirisha hiyo imani yake katika maisha ya kila siku. Matendo anayoongelea Yakobo si kwa ajili ya KUPATA WOKOVU, bali ni kwa ajili ya KUUDHIHIRISHA. Ni matendo ya mtu ambaye TAYARI anayo imani ile ambayo Paulo ameitaja. Ndiyo maana anasema kuwa: … imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. (Yak 2:17). Yaani imani tayari ipo. Matendo yanaifanya iwe hai.SIO kwamba matendo yanakufanya upate nafasi mbinguni. Hapana!

   Delete