Takribani miaka 800 kabla ya Kristo,
Mungu wa Israeli alisema kupitia nabii Yoeli kwamba:
Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa
wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika
siku zile, nitamimina roho yangu.
Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika
dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.
Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja
hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.
Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la
Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako
watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana. (Yoeli 2:28-32).
Jambo hili lilikuja kuanza mara
baada ya Bwana Yesu kufufuka na kupaa kurudi mbinguni, pale Roho Mtakatifu
aliposhuka kwa nguvu siku ya Pentekoste. Biblia inasema:
Hata ilipotimia siku ya
Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi
kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa
wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia
kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu …
(Matendo 2:1-4).
Kwa sababu watu wote walipigwa na mshangao wa kile kilichokuwa
kimetokea, Biblia inasema: Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza
sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu,
lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Sivyo mnavyodhani; watu hawa
hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile
lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu,
nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na
vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. (Matendo 2:14-17). Hicho ndicho
kinachotokea kwenye ulimwengu wa Kiislamu sasa. Si kazi ya mwanadamu, bali ni Roho
Mtakatifu mwenyewe yuko kazini!
Mbingu haziwezi kukaa
kimya siku zote huku zikiona watu wakiwa wamefungiwa nyuma ya malango ya chuma.
Nchi nyingi za Kiislamu ambazo zinaongozwa kwa sheria kali za Kiislamu zinapiga
marufuku kabisa Injili ya Yesu kuhubiriwa kutokana na hofu ya watu kuuacha
Uislamu endapo watajua upendo wa Mwokozi wao aliyewafia msalabani, yaani Yesu
Kristo.
Hata baadhi ya watu ambao
wanajitia nguvu kuingia katika nchi hizo
ili kuwapelekea watu Neno la uzima, wakikamatwa, wanafungwa au wanauawa
– ama kwa kunyongwa, kuchinjwa shingoni, au kwa kupigwa risasi, n.k.
Lakini Neno la Kristo
ambalo halipotei hata nukta moja hadi lote litimie, linasema kwamba: Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa
ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. (Mathayo 24:14).
Dunia hii ni mali ya Yesu.
Wanadamu wote ni mali ya Yesu. Mamlaka yote mbinguni na duniani amepewa Yeye.
Mamlaka haya hayatokani na imani yetu. Tuamini au tusiamini, anayo tu! Ni Yeye
ndiye aliyesema kuwa kabla hajarudi, INJILI NI LAZIMA IHUBIRIWE ULIMWENGUNI
KOTE. Hii ina maana kuwa Injili ni lazima ihubiriwe Irani, Saudi Arabia, Uchina,
Korea Kaskazini, Pakistani, Libya, Algeria, n.k. Huko kote wapo wana wa Ufalme
ambao ni lazima wamkubali Yesu, maanatayari
wana nafasi zao kwa Baba mbinguni.
Wakuu
wa dini na wakuu wa serikali wafanye kila watakalo, lakini Neno la Bwana Muumba
wa mbingu na nchi halitanguki; halijawahi kushindwa na halitashindwa kamwe. Ni lazima
litimie.
Kwa sababu yule azuiaye
ameweka mageti ya chuma na ngome za moto kwenye nchi nyingi ili Injili
isihubiriwe, kuna jambo la ajabu linaloendelea kwenye ulimwengu wa Kiislamu
hivi sasa. Mamilioni ya Waislamu wanakuja kwa Yesu – si kutokana krusedi na
mikutano ya Injili – hapana! Ni kutokana na ndoto na maono kuhusu Mwokozi Yesu
kama ambavyo Bwana aliahidi miaka mingi iliyopita kupitia nabii Yoeli.
Wakati watawala na polisi
wao na magereza yao wakiwa wanazuia Injili kuhubiriwa, Bwana anawatembelea watu
wake kupitia ndoto na maono. Makundi kwa makundi ya watu kwenye ulimwengu wa Kiislamu
wanamwona Mwokozi kupitia ndoto na maono. Kupitia njia hizo, Bwana
anajidhihirisha kwao, anasema nao, na matokeo yake wanampokea kama Bwana na
Mwokozi wao PEKEE maana, zaidi ya jina la Yesu: hakuna
wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya
mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. (matendo 4:12).
Enyi watawala mnaowafungia
watu makongwa ya udini mtafanya nini sasa? Ninyi mnaowazuia watu wa Mungu
kupokea uzima, si kwa sababu mnawatakia mema, bali ili tu muweze kulinda
heshima za dini zenu, mtafanya nini sasa? Mtawekaje askari walinzi ndotoni
sasa?
Hebu sikiliza ushuhuda kwenye
video hapo juu ambao ni mmoja kati ya nyingi ambazo nitakuletea. Video hii
inaonyesha kazi hiyo ya ajabu anayofanya Roho Mtakatifu kwenye ulimwengu wa
Kiislamu hivi sasa.
Kwa kweli ndugu zangu
Waislamu amkeni. Acheni kupenda dini kuliko kumpenda Mungu. Ukipenda dini,
utaanza kulinda dini. Lakini ukimpenda Mungu, utalindwa na Yeye.
Video hiyo inaonyesha waumini
wa Kikristo kule Kurdistan, Iraki ambao mwanzoni walikuwa Waislamu. Humo kuna
wengi wanaoongea, akiwamo msimuliaji. Lakini mimi nitajikita zaidi kwenye maneno
ya Wakurdistani wenyewe.
Mchungaji Zagros (mwenye
nywele zilizochongoka mbele) anasema, “Biblia inatufanya tuamini kama kwamba
Kitabu cha Matendo ya Mitume kitajirudia hapa Kurdistan.”
Baadaye anaendelea kusema,
“Zamani nilikuwa mmoja wao kabla ya kuamini ujumbe kwamba ninatakiwa kuwaua
wengine. Wakati mwingine nilitamani hata kumuua mke wangu kwa vile tu hajafunika
kichwa chake. Lakini nilipoyapata maisha yangu ndani ya Yesu, kitabu cha
Mathayo kinaniambia niwapende maadui zangu.”
Ukiendelea kusikiliza,
hatimaye anaonekana dada mmoja anayesema, “Nina furaha sana kwa kuwa Yesu
alikuja kugonga kwenye mlango wa moyo wangu. Ndipo nilipomjua Mungu wa kweli
katika namna ya kweli ya maisha.”
Halafu anafuata baba
mwingine mwenye kipara. Anasema, “Kabla sijawa muumini, siku zote nilihisi kuwa
kuna kitu kimekosekana kwenye maisha yangu kana kwamba nimepoteza kitu. Hisia hizo
ziliniandama kila wakati. Sasa hivi, baada ya kuwa mwamini, hisia hizo hazipo
tena. Ninajua kuwa nimeshapata kile ambacho kilikuwa kinakosekana kwenye maisha
yangu.”
Ndugu yangu uliye
Mwislamu, je, wewe hufuatwi na hisia za namna hiyo? Je, si kweli kwamba kila
wakati unajitahidi kumridhisha Mungu wako kwa mambo mengi kwa sababu ya ile
hofu ya kutupwa jehanamu? Lakini si kweli kwamba hata ukijitahidi vipi bado
unakuta hiyo hali ya kuhukumiwa inakuwapo moyoni? Kwa Yesu hakuna mambo kama
hayo? Njoo upate amani ya kweli na wokovu wa kweli.
Kisha kwenye video anafuata
bwana mwingine anayesema, “Watu wengi wanaona maono kuhusu Yesu; hata kama
walikuwa hawajui chochote kuhusiana na Biblia au Agano Jipya au Kanisa. Wanamwona
tu Yesu kwenye ndoto.”
Kisha Mchungaji Zagros
anarudi tena na kusema, “Nilimwona Yesu kwenye ndoto mwaka 1999. Hakuniacha peke
yangu. Alikuja tena. Alisema, ‘Nakupenda na ninataka uokoke.’”
Mchungaji Zagros anaendelea
kusema, “Nataka kuuambia ulimwengu. Pokeeni upendo wa Mungu. Inaweza ikawa sasa
au baadaye, lakini kila mmoja atakuja kupiga magoti mbele za Mungu. Ni bora
kufanya hivyo sasa.”
Ndugu uliye Mwislamu, Yesu
alikuja kwa ajili ya ulimwengu wote. Yesu hakuja kwa ajili ya Wakristo kama
wengi wanavyodhani. Njoo kwa Yesu sasa upige magoti kwake maana Yeye ndiye
Mungu wako aliyekuumba na kukufia msalabani kama sadaka ya dhambi zako na za
ulimwengu wote. Unaweza kukataa kupiga magoti sasa kwa sababu huu ni wakati
ambao tumepewa uhuru wa kuchagua. Lakini siku inakuja ambapo uhuru huo
utaondolewa. Na hapo utapiga magoti tu! Ili si kwa kupenda, bali ni kwa lazima na
baada ya hapo itafuata hukumu. Lakini nikuhakikishie kabisa kwamba Yesu
anakupenda mno mno. Hata sasa analia kwa ajili yako. Anasikitikita kwa jinsi
ambavyo hutaki wokovu wa bure na unakoelekea ni kubaya sana. Njoo leo!
Umeshaambiwa kuwa Yesu si
Mungu, sawa; Yesu hakufa, sawa; Yesu ni mtume tu, sawa. Basi ninakupa
changamoto. Najua unataka kwenda mbinguni. Pia najua kuwa kama ningekuwa na
namna ya kukuonyesha kwa uhakika kabisa jinsi ambavyo Yesu ni Mungu, nina
uhakika kuwa baada ya hapo, ungesema moja kwa moja, “Bwana Yesu nakupa moyo
wangu.”
Si kwamba unamkataa Yesu
kwa kuwa hutaki kwenda mbinguni, la hasha. Ila unamkataa Yesu kwa kuwa unaamini
kabisa moyoni mwako kwamba hapo uliko, uko sahihi.
Basi ninakupa changamoto
hii: MWITE YESU KWA MOYO WAKO WOTE NA UMWAMBIE KUWA AJIDHIHIRISHE KWAKO YEYE
MWENYEWE!!
Kwani kuna ubaya gani? Huyo
si ni binadamu tu kama unavyoamini? Kama ungekuwa unaamini kwamba Yesu ni jini,
basi ungeweza kuniambia, ‘Sitamwita kwa kuwa atanidhuru.’ Lakini kwa vile
unaamini kuwa Yeye ni mwanadamu tu; ni mtume tu, bila shaka hata akija,
hatakudhuru kwa lolote. Basi mwite leo!!! Mwambie, “Yesu njoo ujidhihirishe
kwangu.”
Roho Mtakatifu yuko kazini
katika nyakati hizi za jioni ya ulimwengu huu; wakati ambapo tunamalizia majira
na nyakati za ulimwengu huu. Mungu akubariki sana.
**********
Hata wewe uliye Mkristo
lakini hutaki kupokea wokovu kwa sababu unasema, “Mimi sitaki kuitwa mlokole.” Ndugu
yangu, dini– iwe ni Ukristo, Uislamu au dini nyingine yoyote – haina faida
yoyote kwa mwanadamu. Yesu hakuja kuleta dini. Dini zilikuwapo tangu maelfu ya
miaka kabla ya kuja kwa Yesu. Yesu alikuja kuleta WOKOVU kwa njia ya kujitoa
sadaka ili, kwa imani na utii wetu kwa neno lake, tumpokee YEYE na si dini;
maana Yesu ni NJIA, KWELI na UZIMA. Okoka leo!
No comments:
Post a Comment