Sunday, January 13, 2013

Mwanamke Mwislamu Aliyemkimbilia Yesu Kristo


Hii si picha ya Siti mwenyewe. Ni picha tu kutoka kwenye mtandao.

Ushuhuda wa Siti Zainab

Assalam-mualaikum.

Jina langu ni Siti Zainab. Mimi ni mwanamke wa Kiislamu kutoka Malesia, kusini mashariki mwa Asia.  Nilizaliwa kwenye familia ya Kiislamu, iliyokuwa ikifuata taratibu za Kiislamu kwa nguvu sana. Tokea mwanzo, nilipata elimu ya Kiislamu ambayo ilikuwa imara na ya ndani sana.

Pamoja na elimu yangu ya msingi, nilipelekwa pia kwenye madrasah ya Kiislamu, yaani shule ya dini, na nikaanza kusoma na kukariri Quran tangu mapema; huku nikijifunza maadili na misingi ya Uislamu wa Kisuni, kutoka kwa walimu waliobobea wa Kiislamu. Huko nilijifunza kumwogopa na kumtii Allah s.w.t. na pia kufuata mafundisho na mifano ya Mtume Muhammad (hususani yale yaliyo kwenye Hadithi zinazokubalika). Pia nilikuwa nina uwezo wa kusoma Quran yote, jambo ambalo liliwafurahisha wazazi wangu. Kwa kifupi, nilikuwa nina msingi imara na imani ya ndani ya dini kama Muslimah mwaminifu na aliyejitoa kwa moyo wote.
  
Sikuacha kutekeleza wajibu wangu wa kidini wa kufanya swala (au Namaz) kuswali mara tano kwa siku, na nilifunga siku 30 zilizotakiwa katika mwezi wa Ramadhani – ambao ni mwezi mtukufu katika kalenda ya Kiislamu. Nilitekeleza nguzo zote za imani kwa uaminifu, bila kuambiwa au kukumbushwa na mtu yeyote, hasa na wazazi wangu waliokuwa Waislamu! Kwa kifupi, hakuna mtu aliyenitilia shaka au kuhoji malezi yangu ya kidini na kujitoa  kwangu kama Muslimah (Muislamu mwanamke) ambaye ni mcha Mungu.
  
Hata hivyo, kadiri nilivyoendelea kutekeleza wajibu wangu katika Uislamu, sikuwa nimewahi kuhoji au kutilia shaka umuhimu wa huu ufanyaji wangu wa ibada kwangu. Lakini kadiri muda ulivyoenda, mambo haya yote yalizidi kuonekana ni taratibu tu za kidini na matendo yasiyokuwa na maana ambayo yalipoteza maana na mvuto kwangu! Je, taratibu hizi mazoea haya ndiyo mambo yanayoelezea aina bora kabisa ya uhusiano ambao Mungu/Allah anaweza kujenga kati yake na wanadamu, ambao uko sawa na uhusiano kati ya Bwana na mtumwa?? Pia, ni taratibu ambazo zinafuatwa ili tu mtu aweze kukusanya pointi au maksi ambazo yamkini zitaongeza nafasi yangu ya Allah kuweza kuniingiza Peponi??     

Nikawa na maswali na mashaka mengi, mengi ya namna hiyo ambayo niliyaweka moyoni mwangu wala sikumwambia mtu, maana sikutaka kuumiza hisia za marafiki zangu wa Kiislamu. Pia nilikumbuka jinsi ambavyo nilikemewa kwa nguvu sana na kuzuiwa kuuliza maswali haya ya msingi na walimu wangu wa elimu ya Kiislamu! 

Hata hivyo, maswali haya yaliendelea kuwa ndani ya moyo wangu na mawazo yangu, na yakazidi kuwa na nguvu kadiri nilivyokua kufikia umri wa miaka ya elimu ya sekondari! Nilipokuwa naingia katika utu uzima, taratibu za lazima za Uislamu zilizidi kuwa dhaifu, zilizo tupu na hata matendo mafu. Hazikuwa tena ni za kunifanya nistahili wala kuwa za baraka kama ambavyo maustaadhi na maustaadha (walimu wa dini) wangu walivyojaribu bila mafanikio kutufundisha.

Hiyo haikumaanisha kwamba sikujitahidi kiasi cha kutosha! Kusema kweli nilijitahidi kutafakari mara nyingi na kuelekeza mawazo yangu kwenye mambo mazuri na safi katika kila tendo la ibada. Hata hivyo, ule utambuzi wa jinsi vitendo hivi vya Kiislamu vilivyo vya juujuu na vitupu (shallow and empty) haukuweza kuondoka kwangu! Maswali bado yaliendelea kubakia – je, hii kweli ndiyo njia sahihi na bora zaidi ya wanadamu kuwa na uhusiano na MUNGU?

Baada ya kumaliza sekondari ya juu, nilichaguliwa kujiunga na chuo kikuu katika kozi niliyoipenda. Nikiwa chuoni, nilizidisha pia utafutaji wangu wa majibu ya maswali yangu kuhusu maisha na utupu (emptiness) ambao dini ya Kiislamu ilinipa. Nilizidi kusoma zaidi na kufanya utafiti hadi nikagundua kitabu kinachoitwa   Appointment in Jerusalem. Kitabu hiki kimeandikwa na mwanamke Mdenimaki, na kinaelezea kuhusu mashindano makubwa ya ndani yake ya kiroho na juhudi za kutafuta maana na ufahamu na utoshelevu katika dini yake. Nilivutiwa na yaliyomo humo maana kilikuwa kinafanana na mashindano na maswali yaliyokuwa ndani yangu! 

Sikushangaa sana nilipogundua kwamba mwanamke huyu alipata utambuzi kwamba uhusiano wake na Mungu unaweza kuwa wa moja kwa moja na wa hiyari binafsi, bila kupitia kwenye mizunguko ya taratibu za kidini na kufuata hatua fulanifulani ambazo hutakiwi kuzibadilisha hata kidogo. Nilijifunza kwamba wanadamu wanaweza kuwa na uhusiano na Mungu kwa uhuru kabisa hata kwa kuwa na uhusiano binafsi na wa moja kwa moja naye. Yaani, wanadamu wanaweza kuwa na uhusiano na Muumba bila kujisumbua na taratibu za kidini, moja kwa moja, kama vile mtoto anavyokuwa na uhusiano na baba yake! Huu ni uhusiano wa moja kwa moja, wa kibinafsi na wenye nguvu. Kwa hiyo, ina maana kuwa hivi sasa wanadamu wanaweza kumjua Mungu kibinafsi kama ilivyo kwa baba na mwanawe.   

Je, hii inaweza kuwa ndiyo aina ya uhusiano niliokuwa nautafuta kwa muda sasa? Katika madarasa yangu ya chuo kikuu kulikuwa na Wakristo ambao walikuwa ni watu wema na walio tayari kutoa msaada. Hata hivyo, sikujichanganya nao kwa ukaribu, bali niliwatazama kwa mbali tu. Nilikuwa najaribu kuwaza kama imani yao na uhusiano wao na Mungu ulikuwa na mahangaiko sawa na niliyokuwa nayo mimi. Nilijiuliza kama na wao walikuwa na uhusiano usio na maana na usio wa ndani kama ilivyokuwa kwangu nikiwa Muslimah!

Japokuwa Wakristo hawa walikuwa thabiti kiimani, hawakujaribu kunihubiria Ukristo. Ilikuwa ni baada ya miezi kadhaa kupita ndipo nilipouliza kuhusu dini yao na hali yao ya kiroho. Walivutiwa sana kwamba mimi, Mwislamu, nilikuwa nataka kujadili kuhusu dini na wao, Wakristo! Hata hivyo, ninawaheshimu sana kwa kuwa kawakujaribu kunipandikizia dini yao. Kwa upande mwingine, tuliweza kukaa pamoja na kujadili kuhusiana na dini zetu na mashindano yetu ya kiroho kwa uwazi, kama watu walio sawa; kama watu wazima waliokomaa.

Ilikuwa ni kupitia majadiliano na hawa wanafunzi wenzangu wa chuoni ndipo nilipoweza kufahamu vizuri ni nini ambacho mafundisho ya Kikristo yanahusu, na pia ufahamu zaidi juu ya kile kitabu,  Appointment in Jerusalem.

Hata hivyo, kwa miaka yote miwili chuoni, sikufanya lolote kuhusiana na Ukristo. Bado nilikuwa nataka kutafiti zaidi ndani ya dini yangu ya Kiislamu juu ya uhusiano wa kweli kati ya Mungu na wanadamu, na kulinganisha hayo na mafundisho ya Injili. Katika miaka ile miwili, wale marafiki zangu Wakristo walikuwa wavumilivu sana kwangu na maswali yangu. Wakati mwingine maswali yangu yalikuwa ya kijinga na yasiyo na uzito; wakati mwingine yalikuwa magumu! Lakini nilivutiwa sana na uungwana, upole na unyofu wa Wakristo.

Baada ya miaka miwili, niliamua hatimaye kukumbatia na kukubali mafundisho ya kweli na ujumbe wa Injili ya Yesu Kristo. Tangu wakati ule, maisha yangu ya maombi, kuabudu, kufunga na kutenda matendo mema yamekuwa bora sana na yaliyobarikiwa na Mungu mwenyezi. Nimeshatambua kwamba mwanadamu hajaumbwa ili awe kama roboti; hajaumbwa ili uhusiano wake na Mungu/Allah uwe kama wa bwana na mtumwa!!

Kwa upande mwingine, ujumbe wa Injili takatifu ya Yesu Kristo unasema kwamba watu wote wanaopokea Njia, Kweli ya Mungu, watapewa uhusiano mpya kabisa na Mungu, na haki ya kuitwa wana wa Mungu, kama ilivyoandikwa kwenye Maandiko Matakatifu na kufundishwa na Sayidina Isa A.M. mwenyewe:

Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. (Yohana 1:12-13).


Baada ya kubarikiwa na Bwana, kama mwanawe, maisha yangu yalianza kubadilika na kuwa bora. Watu wa familia yetu waligundua mara moja kwamba kuna jambo la tofauti. Hatimaye baadaye wakaja kujua juu ya imani yangu ya Kikristo na kwamba mimi ni mfuasi wa Yesu Kristo kama inavyofundishwa kwenye Injili. Hapo ilikuwa hali ngumu kidogo kwao kunikubali mimi kama mfuasi wa Yesu Kristo – Uislamu ni dini isiyo na uvumilivu hata kidogo kwa wafuasi wake wanaoikana. Nakumbuka nilipita kipindi cha majaribu na vikwazo vizito kwenye wakati huo wa maisha yangu.

Licha ya hayo yote, Bwana Mungu alinipa nguvu na uvumilivu wa kutosha kustahimili na kupita kwenye mwitikio wa mwanzo wa familia yangu uliokuwa na tamuchungu. Niliamini kikamilifu ukweli kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wangu, Neno lililo hai la Mungu (Logos kwa Kigiriki, Kalimatullah kwa Kiarabu; linganisha na Yohana 1:1-5, AQ Surah 3/45, 4/171) maishani mwangu.

Nafikiri hawajui maana hasa ya kuwa mfuasi wa Yesu Kristo ni nini. Quran haina maelezo kamili ya maisha na huduma ya Sayidina Isa Al-Masih, yaani Yesu Masihi. Lakini Injili zilizo kwenye Agano Jipya zina maelezo kamili na ya kina juu ya kila kitu cha muhimu ambacho Sayidina Isa A.M. aliwahi kusema na kutenda!  

Leo, Mungu asifiwe, Alhamdulillah, hali katika familia yangu imekuwa bora zaidi. Cha muhimu zaidi ni kwamba, hivi sasa ninao uhakika wa uhusiano wa kweli na wenye nguvu na Mungu mwenye upendo, kuliko ilivyokuwa zamani, ambapo matendo yangu mema, au amal saleh hayakuwa yanatosha kunihakikishia mimi uhusiano mzuri na unaokubalika na Allah, pamoja na kwamba nilijitahidi sana kuwa Muslimah bora na mwema. Hakuna Mwislamu anayejua kamwe au aliye na uhakika juu na nini na lini atafanya kiwe kinatosheleza kabisa kumfanya Mungu wa Uislamu aridhike!

Sasa, nikiwa kama mfuasi na mwamini wa Yesu Kristo na Wokovu wake, ninao uhusiano na Mungu ambao umebarikiwa sana na bora sana kuliko ule wa mtumwa na bwana wake kama Uislamu unavyofundisha, maana, kama mtumwa, hatuna uhakika kama bwana wetu ameridhika na huduma au unyenyekevu wetu!  

Leo, nikiwa mwana wa Mungu, ninao ujasiri na uhakika wa milele kuhusiana na uhusiano wangu na Mungu, unaotokana na zawadi ya upendo ya Mwokozi wangu Sayidina Isa, ambaye alitoa kiffarat [dhabihu ya ondoleo la dhambi] timilifu kwa niaba yangu. Hivi sasa, Roho wa Mungu Mwenyewe amemimina kila baraka njema na ya ajabu ya rohoni kwenye maisha yangu kutoka kwenye utajiri wake, nikiwa kama mwana wake na pia mtumishi wake.

Ningependa kukualika uje uponywe kutokana na hali yako ya kutokuwa na uhakika wa kiroho, kuchanganyikiwa na kukosa uhakika wa milele kuhusiana na maisha yako baada ya dunia hii (Akhirat), na uje na kupata na kujua wewe binafsi baraka za kiroho zisizo na mfano ambazo Mungu aliye hai atakupatia. Mimi mwenyewe sijajuta hata kidogo kutokana na uamuzi niliofanya, wa kufuata na kubakia mwaminifu kwa Neno la Mungu lililo hai, yaani  Sayidina Isa, Masihi, kwa leo na hata kwa kesho.

Ni mimi rafiki yako, Zainab.

*******************

Ndugu yangu msomaji, umemsikia Zainab na umeona mapito yake. Nina uhakika hata wewe unayo maswali mengi kuhusiana na dini na Mungu na maisha ya peponi.

Siku utakapoamua kufikiri na kutafakari kama mtu binafsi atakayeenda kusimama kibinafsi mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu; na siku utakapoacha kujidanganya kwamba matendo yako mema yatakupatia nafasi mbinguni wakati unajua fika kwamba moyo wako umejaa ukengeufu; hapo ndipo utakapoanza kuitafuta kweli ya uzima wa milele.

Kweli ina gharama. Na gharama moja kubwa ni kwamba itatikisa kabisa maisha yako na kung’oa mambo ambayo umeyahangaikia maisha yako yote ili isimame yenyewe ndani ya maisha yako.

Yesu Kristo ndiye KWELI! Imeandikwa: Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. (Yohana 14:6).

Tafakari.
Hoji.
Amua.

Unaweza pia kusoma ushuhuda huu kwa lugha ya Kiingereza ambao ndio umezaa tafsiri hii ya Kiswahili. Tafadhali bofya HAPA.

Waweza kuniandikia maoni yako pia kupitia: ijuekweli77@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment