Sunday, February 10, 2013

Baada ya Kuijua Njia ya Kweli, Mwana wa Kiongozi wa Hamas Auacha Uislamu na Kumgeukia Yesu KristoMosab Hassan Yousef ni kijana wa kipekee ambaye ana ushuhuda usio wa kawaida. Baba yake ni mmoja wa waliokuwa viongozi wenye ushawishi mkubwa sana ndani ya kundi la kijeshi la Hamas kule Ukanda wa Magharibi (Palestina). Mosab alikulia kwenye familia iliyoshikilia Uislamu kwa nguvu sana.

Akiwa na umri wa zaidi ya miaka 30 sasa [yaani wakati ushuhuda huu ukiandikwa], ni mshirika wa Kanisa la Kikristo, Barabbas Road kule San Diego, Calif. Aliikana imani yake ya Uislamu, akaiacha familia yake kule Ramallah na anatafuta hifadhi ya kisiasa kule Marekani.

Hadithi ya maisha yake inashangaza sana - uwe unakubaliana au hukubaliani na mtazamo wake. Video ifuatayo inaonyesha mahojiano kati ya Mossab na kituo cha FOX News, akieleza yeye mwenyewe namna Muislamu kutoka Ukanda wa Magharibi alivyogeuka na kuwa Mkristo wa Pwani ya Magharibi.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Jonathani Hunt na Mosab Hassan:

Jonathan Hunt: Kwa nini umekuja kubadilika baada ya miaka 25?

Mosab Hassan Yousef: Naamini kuwa zile kuta zote ambazo Uislamu umezijenga kwa miaka 1,400 iliyopita hazipo tena hivi sasa. Lakini wao hawatambui hili. Walizijenga kuta zile na kuwafanya watu wawe wajinga kutokana na hofu. Hawakutaka watu wajadili kitu chochote kuhusiana na hali halisi ya Uislamu; waliwaambia wafuasi wao, ‘Msiulize maswali hayo.’ 

Lakini sasa watu wana vyombo vya habari. Kama baba akimfungia mlango binti yake ili asitoke nje ya nyumba, ataenda kwenye kompyuta yake na kusafiri ulimwenguni kote. Kwa hiyo, watu wanaweza kwa urahisi kupata taarifa na maarifa pale wanapotumia ‘search engines’ mtandaoni. Kwa hiyo kila mtu anaweza kujifunza kuhusu Uislamu na dini zingine – si kwa mtazamo wa Kiislamu bali kwa mitazamo mingine.  

Hivyo, kwa miaka 25 ijayo, hakika hali hii italeta mabadiliko makubwa sana kwenye ulimwengu wa Kiislamu na wa Kiarabu.

Jonathan Hunt: Unazungumza kwa mtazamo wa kipekee, mtu ambaye ulikulia si tu katika familia ya Kiislamu bali pia kama sehemu ya kundi ambalo linaonekana kwa watu wengi duniani kama nguvu kubwa sana ndani ya Uislamu, yaani Hamas. Hali halisi ya Uislamu ikoje? Unasema kuwa watu hawaoni hali halisi; kwani hali halisi ya Uislamu ikoje? 

Mosab Hassan Yousef: Upo ukweli wa aina mbili ambao Waislamu hawauelewi ... naweza kusema ni takribani zaidi ya asilimia 95 ya Waislamu hawaielewi dini yao. Ilikuja kwa lugha kali zaidi ya lugha wanayozungumza, kwa hiyo hawaelewi ... wanategemea tu viongozi wa dini katika kupata maarifa yao kuhusiana na dini hii.

Pili, hawaelewi chochote kuhusiana na dini zingine. Jamii za Kikristo zinaishi katikati ya Waislamu na ni ndogo, ambazo kwao huona ni heri kutozungumza chochote juu ya Yesu ili kuwaambia wengine, maana kufanya hivyo ni hatari kwao. Kwa hiyo, kile Waislamu wanachofahamu kuhusiana na dini zingine duniani ni kutokana na mtazamo wa Kiislamu. Kwa hiyo, hayo mambo mawili ndiyo ambayo watu wengi hawayaelewi.

Kama Waislamu wataanza kuielewa dini yao – jambo la kwanza, dini yao – na kuona jinsi ndani yake kulivyo na mambo mabaya, wataanza kufahamu, hii haiwezekani ... maana watu wengi wacha Mungu hujielekeza kwenye mambo fulani fulani tu ya Uislamu. Wana mambo mengi sana ambayo wanaona fedheha kuyazungumzia.

Jonathan Hunt: Kama yapi?

Mosab Hassan Yousef: Kwa mfano wake za Muhammad. Hutaweza kwenda msikitini na kusikia mtu yeyote akiongelea wake za Muhammad – ambao walikua zaidi ya 50 – na hakuna anayejua hili, kimsingi. Ukiuliza Waislamu wengi, hawajui juu ya ukweli huu.

Kwa hiyo, wanaona fedheha kuzungumzia jambo hili, lakini wanazungumzia juu ya utukufu wa Uislamu, wanazungumzia juu ya ushindi aliopata Muhammad. Kwa hiyo, pale wanapojitazama na kuona kwamba wameshindwa, hawana ufahamu (have ignorance), hawana elimu, hawaiongozi tena dunia kama wanavyotarajiwa kuwa, basi wanawaza kuwa wanatakiwa kurudi kwenye uleule ushindi kwa kufanya yaleyale ambayo alifanya Muhammad, bila kujali kuwa nyakati hizi ni tofauti. Wanasahau kuwa mambo hayo yalitokea miaka 1,400 iliyopita na hayatatokea tena.  

Jonathan Hunt: Je, wanataka kuuharibu Ukristo?

Mosab Hassan Yousef: Uislamu uliuharibu Ukristo tangu mwanzo na Waislamu hawatambui kuwa waliuchoma Ukristo moyoni mwake pale Uislamu uliposema kuwa Yesu hakufa msalabani. Wao wanadhani kuwa wanamheshimu Yesu kwa kusema hivyo.

Kimsingi, Mkristo yeyote anaelewa hili. Lakini Waislamu wanamwambia Yesu, “Hatujali. Wewe haukufa kwa ajili yetu.” Yaani, mtu fulani ametoa maisha yake kwa ajili yako, lakini wewe  unamwambia, “Hukufanya hivyo!”  Hiki kimsingi ndicho wanachofanya Waislamu. Lakini hawaelewi kwamba hili ni jambo la muhimu sana katika Ukristo: yaani msalaba!

Kwa hiyo, hawaelewi. Hawajui kile wanachokifanya. Na hili linaonyesha wazo ovu lililo ndani ya huu Uislamu.

Jonathan Hunt: Ni jambo au mambo gani hasa yaliyokufanya uanze kubadili mawazo yako juu ya Uislamu?

Mosab Hassan Yousef: Tangu nilipokuwa mtoto nilianza kujiuliza maswali magumu sana. Hata familia yangu walikuwa wakisema mara nyingi, ‘Wewe ni mtu mgumu sana na tunapata shida kujibu maswali yako. Kwa nini unauliza maswali mengi namna hiyo?’ Niseme tu wazi  kwamba hivi ndivyo ilivyokuwa kwangu kutokea mwanzo.

Lakini nilihisi kama vile kila mtu – na baba yangu alikuwa ni mfano mzuri kwangu kwa sababu alikuwa ni mtu mwaminifu, mnyenyekevu, na mwenye upendo kwa mama yangu, kwetu; na alitulea kwenye msingi wa kusamehe. Nilidhani kuwa kila mtu katika Uislamu alikuwa hivi.

Nilipofikisha miaka 18, nilikamatwa na Waisraeli na kufungwa gerezani chini ya utawala wa Israeli. Hamas nao walikuwa na udhibiti juu ya watu wao ndani ya magereza yao nami nilishuhudia mateso waliyowapa. Hamas walikuwa wakiwatesa watu vibaya sana, sana. 

Jonathan Hunt: Unamaanisha Hamas wanawatesa washirika wengine kutoka Hamas?

Mosab Hassan Yousef: Viongozi wa Hamas! Viongozi wa Hamas tunaowaona kwenye TV sasa, viongozi wakubwa, ndio wanaohusika kuwatesa washirika wao wenyewe. Hawakunitesa mimi, lakini hilo lilikuwa jambo lililonishtua sana – kuwaona wakiwatesa watu; wakiingiza sindano chini ya kucha za watu, wakichoma moto miili yao ... Na waliua watu wengi sana.

Jonathan Hunt: Kwa nini walikuwa wakiwatesa watu?

Mosab Hassan Yousef: Kwa sababu waliwatuhumu kwamba walikuwa na uhusiano na Israeli na kwamba walikuwa wakishirikiana na Israeli kuupinga utawala wa Hamas ... Kwa hiyo, mamia ya watu walikuwa wahanga wa tuhuma hizi; na mimi nilishuhudia mateso haya kwa takribani mwaka mzima. Kwa hiyo, hilo lilikuwa jambo mojawapo kubwa lililobadili mtazamo wangu katika maisha yangu. Nilianza kufungua macho yangu, lakini cha msingi ni kuwa, nilitambua kuwa kuna Waislamu wazuri na Waislamu wabaya - Waislamu wazuri, kama vile baba yangu, na Waislamu wabaya, kama wale wa Hamas kule gerezani wanaowatesa watu. Hivyo, huo ulikuwa ni mwanzo wa macho yangu kuanza kufunguka wazi.

Jonathan Hunt: Unaongelea kuhusu Waislamu wazuri, kama vile baba yako, lakini bado sasa unaikana imani ya baba yako. Si ungebaki humo kisha na wewe uwe Mwislamu mzuri?

Mosab Hassan Yousef: Sasa, ukweli wenyewe ni huu: Baada ya kujifunza juu ya Ukristo – ambao zamani nilikuwa nina welewa potofu kabisa kuhusiana nao, maana nilijifunza Ukristo kwa mtazamo wa Uislamu, ambao kimsingi Uislamu unakuambia kuwa hakuna jambo la kweli ndani ya Ukristo - na hicho ndicho kilikuwa chanzo pekee cha kile nilichokuwa nakijua kuhusiana na Ukristo.

Nilipoisoma Biblia kwa makini, mstari kwa mstari, nilihakikisha kuwa kile ni kitabu cha Mungu, Neno la Mungu hakika. Kwa hiyo, nilianza kuona mambo kwa namna tofauti, jambo ambalo lilikuwa gumu sana kwangu, yaani kusema kuwa Uislamu hauko sahihi!

Uislamu ni baba yangu. Nilikulia kwa baba huyu – kwa miaka 22 – kisha akaja baba mwingine kwangu na kusema, ‘Samahani, mimi ndio baba yako.’ Na ikawa kwangu kama vile kusema, ‘Unasema nini? Mimi nina baba yangu, yaani Uislamu!’ Na baba wa Ukristo akaniambia, ‘Hapana, mimi ndio baba yako. Nilikuwa gerezani, na huyu (Uislamu) si baba yako.’

Kwa hiyo, kimsingi hiki ndicho kilichotokea. Si rahisi kuamini kuwa huyu (Uislamu) si baba yako tena. Hivyo, ilinibidi nijifunze Uislamu tena kutoka kwenye mtazamo tofauti hadi kuweza kuona makosa yote; makosa makubwa sana na athari zake, si tu kwa Waislamu -  ambapo nilichukia kawaida zake ... Sikupenda taratibu zile zote ambazo zilifanya maisha ya watu kuwa magumu zaidi – lakini pia athari zake kwa wanadamu wote. Kwa wanadamu! Watu wakiuana wenyewe kwa wenyewe kwa jina la Mungu.

Kwa hiyo, kwa kweli nilianza kuona tatizo ndani ya Uislamu, na si kwa Waislamu – siwezi kuwachukia kwa sababu Mungu aliwapenda tangu mwanzo. Na Mungu huwa hatengenezi takataka. Mungu aliumba watu wazuri ambao aliwapenda; lakini wanaumwa; wana mitazamo isiyo sahihi. Siwachukii watu wale tena lakini nawahurumia sana; na njia pekee ya wao kubadilika ni kulijua Neno la Mungu na njia ya kweli ya kufika kwake.

Jonathan Hunt: Hauogopi kwamba kwa kusema mambo haya – na hasa ukitilia maanani ulikotokea kunakofanya maneno yako yawe na uzito zaidi – kwamba kuna hatari ya wewe kuzidisha zaidi ugumu, chuki kati ya Wakristo na Waislamu duniani hivi sasa?

Mosab Hassan Yousef: Hili linaweza kutokea endapo Mkristo ataenda kwao na kuzungumzia hali halisi ya Uislamu. Kwa hiyo, wewe kama Mkristo ukienda kwao na kuwaambia haya, watakwazika mara moja na watakuchukia. Na hili, kwa hakika litaongeza ufa kati ya dini hizi mbili – lakini ni nini kilichofanya mtu kama mimi abadilike?

Miaka kadhaa iliyopita, wakati nikiwa kule, Mungu alifungua macho yangu, na akili yangu pia, na nikafanyika kuwa mtu tofauti kabisa. Kwa hiyo sasa, ninaweza kufanya wajibu huu, wakati ninyi, kama Wakristo, mnaweza kunisaidia kuutekeleza, lakini pengine hamtafanya hivyo. Hivi sasa Waislamu hawana tena udhuru.

Jonathan Hunt: Jambo hili limekuwa gumu kiasi gani kwako kuondoka kwenye familia yako, na kupaacha nyumbani kwenu? Kumekuwa na ugumu gani?

Mosab Hassan Yousef: Kuondoa ngozi yako toka kwenye mifupa, hicho ndicho kilichotokea. Naipenda familia yangu, na wao wananipenda. Na wadogo zangu ni kama watoto wangu. Niliwalea. Kimsingi, ulikuwa ni uamuzi mkubwa kabisa maishani mwangu.

Niliacha kila kitu nyuma, si tu familia yangu. Nilipoamua kuwa Mkristo au dini nyingine yeyote kutoka kwenye Uislamu, unajua si suala tu la kusema, ‘Kwa heri, naondoka.’ Si hivyo hata kidogo. Unakuwa unasema kwa heri kwa utamaduni, ustaarabu, mila, jamii, familia, dini na Mungu – yule ambaye, kwa miaka mingi, ulidhani ndiye Mungu! Kwa hiyo, si rahisi. Ni jambo gumu sana. Watu wengine hudhani kuwa ni jambo rahisi, kana kwamba si kitu kikubwa. Hivi sasa niko hapa Marekani na nina uhuru wangu, jambo ambalo ni zuri sana, lakini wakati huohuo, hakuna kinachoweza kulinganishwa na familia, unajua. Kupoteza familia yako ....!

Jonathan Hunt: Kwani umepoteza familia yako?

Mosab Hassan Yousef: Familia yangu ni ya watu waliosoma, na ilikuwa ni jambo gumu sana kwao. Waliniomba mara nyingi sana, hasa kwa siku mbili za kwanza, kwamba imani yangu hii iwe ni siri yangu na nisiende kuitangaza kwenye vyombo vya habari.

Lakini kwangu ilikuwa ni wajibu wangu mbele za Mungu kutangaza Jina lake na kumsifu duniani kote kwa sababu thawabu yangu ni kuwa hata Yeye atanifanyia vivyo hivyo. Kwa hiyo, nilifanya hivyo, kama wajibu. Sijui ni watu wangapi wanaweza kufanya kile ninachokifanya?  Sijakutana na yeyote.

Kwa hiyo, ilibidi niwe jasiri katika hilo. Hilo lilikuwa ni changamoto kubwa sana. Huo ulikuwa ni uamuzi mgumu sana maishani mwangu na sikuuchukua ili tu kujifurahisha. Sikuuchukua kwa ajili ya jambo lolote katika ulimwengu huu. Niliuchukua kwa sababu moja tu: Niliamini katika uamuzi huo. Watu wanateseka kila siku kutokana na mitazamo mibaya. Ninaweza kuwasaidia kutoka kwenye duru (circle) hii isiyo na mwisho ... duru ambayo ibilisi amewategea.

Jonathan Hunt: Umeshazungumza na baba yako hivi karibuni?

Mosab Hassan Yousef: Hakuna uwezekano wa kuzungumza na baba yangu kwa vile yuko gerezani hivi sasa na kule hakuna simu za kumwezesha kuzungumza nami.

Jonathan Hunt: Je, wanafamilia wengine wameshakuambia jinsi alivyochukulia suala lako?

Mosab Hassan Yousef: Walishaenda kumtembelea mara kwa mara. Hadi sasa, sifahamu kwa hakika anavyolichukulia lakini ninaamini anahuzunishwa sana na uamuzi kama huu. Lakini wakati huohuo, atakuja kuelewa, maana ananifahamu mimi na anajua kuwa huwa sifanyi uamuzi wowote bila kuuamini kwa nguvu kabisa.

Jonathan Hunt: Je, suala hili linafanya maisha yake miongoni mwa washirika wenzake wa Hamas kuwa magumu zaidi?

Mosab Hassan Yousef: Bila shaka. Familia yangu, akiwamo baba yangu, iliwabidi kubeba msalaba huu pamoja nami na ninamwomba Mungu – ninaomba kwa ajili ya baba yangu. Kaka zangu wote na dada zangu wote hapa kanisani, huwa tunawaombea kila wakati – ili Mungu afungue macho yao, akili zao, ili waje kwa Kristo; na pia awabariki maana iliwalazimu kubeba msalaba huu pamoja nami. 

Jonathan Hunt: Hebu nieleze kuhusu Hamas na jinsi inavyofanya kazi. Je, Hamas ni kundi la kidini kabisa kwa jinsi unavyoliona, na hapo ndipo kosa lake liliko, au ni mahali pengine ndiko kwenye shida? Au Hamas ni kundi zuri tu? Hamas ikoje kwako wewe?  

Mosab Hassan Yousef: Kama tukiongelea kuhusu watu, kuna watu wazuri kila mahali. Kila mahali. Yaani, watu wazuri ambao Mungu aliwaumba.

Je, wanafanya mambo yao wenyewe? Ndiyo, wanafanya? Nawafahamu watu wanaounga mkono Hamas lakini hawashiriki kwenye vitendo vya kigaidi, kwa mfano ... Wao wanafuata Hamas kwa sababu wanampenda Mungu na wanadhani kuwa Hamas inamwakilisha Mungu. Hawana ufahamu; hawamjui Mungu wa kweli na hawajawahi kujifunza kuhusu Ukristo. Lakini Hamas, kama mwakilishi wa Uislamu, ni tatizo kubwa.

Tatizo si Hamas; tatizo si watu. Mzizi wa tatizo ni Uislamu wenyewe kama itikadi. Na kuhusu Hamas kama kikundi, ni wazi, uongozi wa Hamas, akiwamo baba yangu, wanawajibika. Wanawajibika kwa vurugu zote zilizotokana na kundi hilo. Najua kuwa wanazielezea kuwa ni matokeo ya vitendo vya Israeli, lakini bado, wao ni sehemu yake na walikuwa wakifanya maamuzi katika operesheni hizo dhidi ya Israeli; maamuzi ambayo yalisababisha kufa kwa raia wengi.

Jonathan Hunt: Unadhani Israeli haistahili lawama katika mgogoro huu?

Mosab Hassan Yousef: Kukalia ardhi ya watu wengine si vizuri. Siwezi kusema Israeli — Siko kinyume na taifa lolote. Hatuwezi kusema ni Waisraeli; hatuwezi kusema ni Wapalestina. Tunaongea juu ya mitazamo. Israeli ina haki ya kujilinda; hakuna anayeweza kubisha juu ya hili. Lakini wakati mwingine wanatumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya raia. Wakati mwingine raia waliuawa kwa sababu tu wale askari hawakuwajibika  ipasavyo; namna wanavyowatendea watu kwenye vituo vya ukaguzi.

Ujumbe wangu hata kwa askari wa Israeli: angalau muwatendee watu kwa utu kwenye hivyo vituo vya ukaguzi. Si lazima muonekane wabaya kiasi hicho; na hii haihusiani na mataifa; ni suala la mitazamo mibaya kwa pande zote; na njia pekee ya haya mataifa mawili kutoka kwenye duru hii isiyo na mwisho ni kujua kanuni ambazo Yesu alizileta hapa duniani: neema, upendo, kusameheana. Bila hizi, hawataweza kamwe kupiga hatua, au kuvunja duru hii [ya uhasama] isiyo na mwisho.  

Jonathan Hunt: Umeona baba yako amefungwa jela. Wewe mwenyewe ulishakuwa gerezani. Umeona Hamas wakifanya vitendo vya kigaidi dhidi ya Israeli, lakini bado unasema kila mmoja anatakiwa kuvuka juu ya hapo?

Mosab Hassan Yousef: Bila shaka. Hili ni suala tu la uchaguzi. Hakuna mtu mwenye nguvu za kimiujiza zinazoweza kufanya kitu kwa ajili ya Mashariki ya Kati. Hakuna hata mmoja. Unaweza kumwuliza mwanasiasa yeyote hapa Marekani; unaweza kumwuliza mwanasiasa yeyote wa Palestina au wa Kiarabu, viongozi wa Israeli; hakuna hata mmoja, hakuna anayeweza kufanya lolote. Hata kama wanaamini katika amani sasa hivi, wao ni sehemu ya suala hili.

Hawawezi. Hata kama ukipata mtu jasiri, kama vile Rabin, ambaye aliitwa na Waisraeli kufanya amani na Wapalestina na kuwapatia nchi yao, hakuna, hata kama utatafuta kiongozi mwenye nguvu, hawawezi kufanya lolote katika jambo hili. Huwezi kuilazimisha nchi iliyo huru kuipatia uhuru nchi nyingine, na hasa kama hiyo nchi nyingine inataka kuiharibu nchi inayotoa uhuru.

Kila mmoja ameumizwa. Askari wa Israeli wamepoteza marafiki zao; Wapalestina wamepoteza watoto wao, baba zao. Bado wako watu wengi kwenye magereza, na watu wengine wengi wameuawa. Maelfu. Kwa hiyo, kila mmoja hatasahau hali hii. Kama wanataka kuendelea kukumbuka ya nyuma, kamwe hawataweza kutoka kwenye duru hii. Njia pekee ya kuanza ni kusonga tu mbele. Walizaliwa ndani ya Palestina inayokaliwa.   

Vizazi viwili vya mwisho, hawakuwa na la kufanya. Kizazi kipya cha Israeli – tukiachilia mbali kwamba kuwapo kwa Israeli ni halali au si halali, je, watu wale waliozaliwa Israeli wana hatia gani wakati hawana kwingine kwa kwenda? Hivi sasa hiyo ndiyo nchi yao. Hivyo ndivyo wanavyoiona. Na wataendelea kuilinda na kumpinga yeyote aliye kinyume nao. Watasema, ‘Ondoka kwenye ardhi hii!’ Kwa hiyo, njia pekee ni kwa mataifa yote mawili kuanza kuelewa neema, upendo na msamaha wa Mungu, ili waweze kutoka kwenye mgogoro huu.

Jonathan Hunt: Je, unaamini kuwa Israeli itafikia kuwa na amani na Hamas?

Mosab Hassan Yousef: Hakuna uwezekano huo. Je, moto unaweza kukaa pamoja na maji? Haiwezekani. Hamas inaweza kucheza mchezo wa siasa kwa miaka 10, miaka 15, lakini muulize kiongozi yeyote wa Hamas kwamba, baada ya hapo nini kinafuata? Je, mtaendelea kukaa pamoja na Israeli daima? Jibu litakuwa ni hapana ... labda kama [Hamas] watataka kwenda kinyume na Quran. Lakini huo ndio mtazamo wao na wao hawatakaa waseme, ‘Hatutaufuata.’ Kwa hiyo, hakuna uwezekano. Si suala la Israeli; si suala la Hamas. Ni suala la mitazamo ya pande zote mbili. Hakuna uwezekano.

Jonathan Hunt: Hauogopi kwamba kuna mtu atajaribu kukuua kwa kusema mambo haya – jambo ambalo linakubaliwa na Quran?

Mosab Hassan Yousef: Watatakiwa waue kwanza mawazo yangu, maana tayari nimeshayatoa. Sasa, watayauaje? Watauaje mtazamo nilio nao? Wanaweza kuua mwili wangu, lakini hawawezi kuua roho yangu.  

Jonathan Hunt: Ina maana haugopi?

Mosab Hassan Yousef: Kama mwanadamu, unajua, naweza kuwa jasiri sasa. Sifikirii juu ya hilo sasa na ninahisi kwamba Mungu yuko upande wangu. Lakini kama hii itakuwa ndiyo changamoto yangu, basi namwomba Mungu anipe nguvu zaidi.

Jonathan Hunt: Umewahi kutishiwa maisha?

Mosab Hassan Yousef: Hapana. Kusema kweli, Waislamu walio wengi, na viongozi wa Kiislamu wa hapa Marekani na Ulaya wanajaribu kunipata. Wanawasiliana na familia yangu, mama yangu, na kuomba kupatiwa mawasiliano yangu. Wanamwambia, ‘Tunataka kumsaidia.’

Jonathan Hunt: Wanadhani unahitaji msaada?

Mosab Hassan Yousef: Ndiyo. Wanadhani Wakristo walitumia tu shida zangu ili kunipata, na hii si kweli hata kidogo. Nimekuwa Mkristo kwa muda mrefu kabla wao hawajajua, au mtu yeyote kujua. Nampenda Yesu. Nimeshamfuata kwa miaka mingi sasa. Kwa muda mwingi, halikuwa jambo la siri. Na safari hii nimefanya hivi kwa ajili ya utukufu wa Jina la Mungu na kumletea sifa Yeye.

Hapa hawapingani na Mwislamu wa kawaida. Wanajua kuwa mimi nimesoma. Wanajua kuwa nimejifunza kuhusu Uislamu na Ukristo. Pale nilipofanya uamuzi wangu, sikufanya hivyo labda kwa kuwa kuna mtu alifanya miujiza yake kwangu au kunishawishi. Ulikuwa ni uamuzi wangu peke yangu.

Jonathan Hunt: Huwa unaikumbuka Ramallah?

Mosab Hassan Yousef: Kabisa. Umeshafika kule na unajua jinsi ilivyo nchi nzuri. Ni nchi nzuri sana, sana. Ni sehemu ndogo sana lakini ina kila kitu – hii ndiyo sababu watu wanapigana kwa ajili ya kipande hicho kidogo cha ardhi. Kusema kweli naikumbuka sana Ramallah. Yerusalemu. Mji wa Zamani.

Jonathan Hunt: Je, unaamini kuna siku utakwenda tena kule?

Mosab Hassan Yousef: Nadhani mimi ni wa kule, na naamini ipo siku nitakwenda kule, hata kama iweje. Kama wanataka kuniua, watafanya kila wawezalo ili kufanya hivyo. Nina familia yangu pale. Wananipenda. Na sasa wananiunga mkono kikamilifu juu ya maamuzi yangu. Labda hawataki niongee kwenye vyombo vya habari lakini wanaamini kuwa nilifanya uamuzi ambao ninauamini kikamilifu. Kwa hiyo, wananiunga mkono. Ninawapenda familia yangu. Nitarudi tena huko siku moja. Naupenda mji wangu.

Jonathan Hunt: Unadhani kuna siku utaenda Mashariki ya Kati huku kukiwa na amani?

Mosab Hassan Yousef: Kutakuwa na amani kwa asilimia 100 pale Yesu atakaporudi; pale atakapomhukumu kila mmoja. Ufalme wake utadumu kwa maiaka 1,000 na kutakuwa na amani kamili; na utakuwa ni ufalme wa Mungu.

Jonathan Hunt: Upi ni ujumbe wako wa msingi kwa Mwislamu yeyote anayekusikiliza hivi sasa?

Mosab Hassan Yousef: Ujumbe wangu kwao, kwanza kabisa, wafungue akili zao. Walizaliwa kwenye familia za Kiislamu – hivi ndivyo walivyojikuta ni Waislamu na hii ni kama ... dini nyingine yeyote, kama ilivyo kukulia kwenye familia ya Kikristo, au kukulia kwenye familia ya Kiyahudi.

Kwa hiyo, ninachotaka kusema hapa ni kuwa, watu hawa wafungue macho yao, akili zao, na kuanza kuelewa na kupiga picha kana kwamba wasingezaliwa kwenye familia za Kiislamu; kisha watumie ufahamu wao.

Kwa nini Mungu aliwapa akili? Wafungue mioyo yao. Wasome Biblia. Wajifunze juu ya dini yao. Nataka kufungua mlango kwa ajili yao. Nataka wawe huru. Watakutana na maisha mazuri hapa duniani kwa kumfuata tu Mungu – na pia watapata uhakika juu ya maisha yale yajayo. 


Mosab Hassan Yousef

******************

Waweza pia kuusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza kwa kubofya HAPA.

******************

Ndugu yangu uliyesoma ushuhuda huu, yapo mambo mengi ambayo tuliaminishwa tangu utoto wetu. Lakini asilimia karibia mia moja ya sababu za sisi kuyafuata zinatokana na hukohuko kuaminishwa. Kwa maana nyngine, hatuna sababu zinazotokana na uchunguzi wetu binafsi, ambazo tunaweza kweli kusema, “Hili nimelichunguza kikamilisu na kuona kuwa liko kweli.” Je, uko tayari kutikiswa hadi kwenye mizizi ya imani yako ya tangu kuzaliwa kwako endapo utakutana na kweli halisi iliyo tofauti na hayo uliyoaminishwa? Hii ni changamoto kubwa kwako. Maadamu u hai, bado unayo nafasi ya kuchunguza upande wa pili ambao uliambiwa kuwa haukufai. 

Yesu Kristo anazidi kuthibitisha tena na tena kuwa Yeye ndiye Mwokozi wa ulimwengu wote; wa wanadamu wote. Ni Yeye peke yake ndiye  Njia, Kweli na Uzima wa milele.
Tafakari.
Chunguza.
Jihoji.
Chukua hatua.

Tafadhali andika maoni yako hapa chini; au pia waweza kuniandikia mimi (blogger) chochote kuhusiana na ulichosoma hapa au kwingineko ili tuzidi kuelimishana kungali mchana; maana usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. Andika kupitia: ijuekweli77@yahoo.co.uk
Bwana Yesu akubariki.  
No comments:

Post a Comment