Saturday, February 23, 2013

Bwana Yesu Asema na Miryam wa Saudia Kupitia Ndotoni

Ufuatao ni ushuhuda wa dada aitwaye Miryam, kutoka Saudi Arabia, ambaye Bwana Yesu alisema naye kupitia ndotoni. Matokeo yake, dada Miryam alitoka kwenye Uislamu na sasa anamwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wake.


Katika video ya hapo juu, Miryam anahojiwa na mwendeshaji wa kipindi kiitwacho “God of Mracles” au “Mungu wa Miujiza” kinachorushwa na kituo cha TV cha “Jesus Set Me Free”, au “Yesu aliniweka Huru.”


Fuatana na mtangazaji katika mahojiano haya yenye kuonyesha jinsi Bwana Yesu mwenyewe anavyofanya kazi kwenye nchi za Kiarabu ambazo, wao wanadhani kuwa sheria kali zitazuia Injili ya Bwana kupenya. Hawajui kuwa kuta na ngome walizowafungia watu na kuwanyima uhuru zinabomokabomoka na anayezibomoa ni Bwana mwenyewe kwa namna ambao hawana kamwe nguvu ya kuizuia.

****************

Miryam:
Napenda kukueleza jambo. Kama una mashaka au unaogopa jambo lolote, usimwogope yeyote ila Mungu. Kama una maswali yoyote, mwulize Mungu kwa sababu, kweli kabisa, Yesu ni Mwana wa Mungu.

Mimi binafsi nilimwona. Nilimwomba Mungu anionyeshe ndoto na, ashukuriwe Mungu, ndani ya wiki moja, alinionyesha katika ndoto.

Kama una mashaka, mwulize Mungu naye atakuonyesha. Atakuonyesha kwamba Yesu kweli ni Mwana wa Mungu.

Zaidi ya yote, ziko roho nyingi sana zilizopotea ambazo hazijui cha kufanya kuhusiana na dini yao. Hawapendi mahali pale waliko hivi sasa lakini wanaogopa kubadili dini yao.

Nakutia moyo umwulize tu Mungu. Mwulize Kristo. Atakuja kwako. Atakutokea katika ndoto au kwa njia ya maono. Hii imetokea kwa watu wengi sana.

Mtangazaji:
Kwa namna hii umetii agizo. Hapo tayari umeshahubiri Neno la Mungu. Nimefurahi sana sana. Labda nami niseme kitu kuhusiana na mimi mwenyewe, maana hata mimi nilikuwa Mwislamu. Nilishika sana dini hiyo na nilikuwa nimejitoa kwa moyo wote.

Lakini nilipokuwa na miaka 15 … (Wewe ulikuwa na umri gani Bwana alipokutokea?)

Miryam:
Nilikuwa nina miaka 15 na nilikuwa natazama kipindi kwenye TV kama wanavyofanya watazamaji wetu sasa.

Mtangazaji:
Alikuwapo mwinjilisti mmoja anayeitwa Oral Roberts ambaye alikuwa akihubiri juu ya kufufuka kwa Kristo na kuhusu kifo cha Kristo.

Sikuelewa kile alichokuwa anaongelea lakini, wakati akiendelea kuongea, ghafla, Roho wa Mungu alimiminwa ndani yangu. Sitasema kuwa nilikuwa Mwislamu kisha nikawa Mkristo; bali niseme kuwa nilikuwa mfu na nikafufuliwa pale Roho Mtakatifu alipokuja ndani yangu. Na hiki ndicho kilichowatokea watu wote. Labda walikuwa Wabuddha, au walikuwa hawaamini kabisa kuwapo kwa Mungu. Labda walikuwa Wakristo. Labda walikuwa Wayahudi. Haijalishi ni wa aina gani.

Kabla ya Yesu kuja ndani yetu, kiroho tunakuwa ni wafu. Tunahitaji Roho wa Mungu amiminwe ndani yetu. Na imeandikwa kwenye Biblia kwamba, "Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili" (Yoeli 2:28).


Wawe ni watu kutoka Amerika, watu kutoka Palestina, watu kutoka Saudi Arabia, watu kutoka Misri, watu kutoka India, watu kutoka Afrika. Watu kutoka duniani kote! Mungu anamimina Roho wake juu yao. Kweli leo umeipa furaha mioyo yetu kutokana na ushuhuda wako mzuri. 

Ulikuwa pia na ndoto zingine kutoka kwa Bwana. Unaweza kunieleza juu ya ndoto mojawapo uliyopata kutoka kwa Bwana?

Miryam:
Niliota ndoto ambapo nilimwona Yesu. Na katika ndoto hii, kulikuwa na maneno kutoka kwenye Biblia kabla ya mimi kusoma Biblia. Niliyasikia ili watu waweze kujua kuwa ndoto ile ilikuwa inatoka kwa Mungu. 

Ndoto ilionyesha siku ya kiama na nilikuwa ninajaribu kuwahubiria watu Injili. Walikuwapo watu ambao walikuwa hawataki kukubali kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu. 

Mtangazaji:
Na hii ilikuwa ni katika ndoto?

Miryam:
Ndiyo. Nilikuwa ninajaribu kuhubiri Neno na kuwaambia baadhi ya maneno kutoka kwenye Biblia. Niliinua macho yangu na kumwona Yesu akija kutokea mawinguni. Alikuwa na umbo kubwa sana. Sote tunajua jinsi mbingu zilivyo nyeupe. Lakini mng’ao wa Yesu ni tofauti kabisa na mng’ao wa mbingu au wa kitu kingine chochote tulichowahi kukiona.

Ndiyo. Hiki ndicho nilichoona. Nilimtazama na nikajisikia amani kubwa sana. Japokuwa ulikuwa ni wakati wa kuogofya, lakini mimi nilijisikia amani sana. Kisha nikawaonya watu nikisema, “Huyu Ndiye niliyekuwa nawaambia habari zake.” Na wote wakamwona.  

Nusu yao walimkubali na nusu yao walimkataa. Huu ndio ukweli wa ulimwengu huu kwamba, wako watu ambao hawatamkubali Yeye.

Hata kama wangemwona Yesu mwenyewe, bado …. Ndani yao wamekufa. Huu ndio ukweli katika ulimwengu huu. Lakini ashukuriwe Mungu kwamba nusu ya watu, pale walipomwona, walimkubali. 

Alikuwa akishuka siku ya hukumu na alikuwa akishuka hadi Israeli. Hii ndiyo ndoto ya mwisho niliyoota kuhusiana na Yesu. Lakini iliyabadili maisha yangu.

Mtangazaji:
Watu walichukuliaje maisha yako? Je, kuna watu ambao walifahamu imani yako? Na je, waliitikiaje jambo hilo? Yaani waliitikiaje juu ya uamuzi wako wa kumfuata Kristo?

Miryam:
Una maanisha Waarabu?

Mtangazaji:
Ndiyo, Waarabu …..

Miryam:
Kusema kweli kabisa, Waarabu wameheshimu uamuzi wangu. Hawakubaliani na mimi … lakini kila mmoja anaweza kufanya kile ambacho anaamini ndicho Mungu anachotaka.

Namshukuru Mungu kwa sababu amenisaidia sana kufanya mambo yawe rahisi kwangu. Sijakutana na tatizo kubwa. 

Kwa wengine, wanafurahi kuona miujiza na kuona Saudia ikimuijia Yesu. Yesu anatufundisha kuishi na watu wote kwa amani.

Mtangazaji:
Imeandikwa kwamba, "Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote" (Warumi 12:18). Mungu hapendi tuishi wakati wote tukiwa na matatizo, hasira na uadui na watu wengine. Imeandikwa kwamba haya ndiyo mapenzi ya Mungu. Kwa hiyo nafurahi kwamba umepata kibali miongoni mwa watu, hata Waarabu kuhusiana na imani yako. Je, sasa hivi unaenda kanisani?


Miryam:
Ninashiriki kwa siku nne kwa wiki. Tunaenda Jumapili kwa ajili ya ibada ya kawaida. Jumatatu, Jumanne na Alhamisi.

Tunaenda pia kule nje kujaribu kuwaleta watu ambao hawamwamini Yesu. Na tunaomba. Na kuna waimbaji ambao huja na kuimba nyimbo za kuabudu. Na tunawasaidia wale ambao wanataka kumpokea Yesu lakini hawajui wafanyeje.

Mtangazaji:
kusema kweli tunamshukuru Mungu kwa ajili ya utii wako kwa agizo lake ulilopokea kutoka kwake. Umetukumbusha kwamba Mungu yu hai na anawapenda watu wote.

Biblia inasema kwamba, "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."


Labda kuna watazamaji wetu. Ningependa kuwatia moyo leo. Kama ilivyo kwa dada yetu hapa. Labda una mashaka. Labda una njaa au kiu ya kiroho. Labda unatamani kwamba Mungu angekuja na kuijaza hii kiu iliyo ndani yako.

Nakushauri ufanye kama alivyofanya dada yetu Miryam. Mwambie Mungu, “Ewe Mungu, kama Yesu ni Mwanao; kama Yesu alikuja na kufa msalabani kwa ajili yangu, nipe uthibitisho. Nithibitishie pendo lako. Hebu niwezeshe kulijua pendo lako. Bwana ninaomba uijaze kiu hii iliyo ndani yangu.”

Mungu wetu yu hai na yuko na wewe hivi sasa. Na anakupenda kwa upendo usio na mwisho. 

Nawashukuru watazamaji wetu kwa kuwapo kwenu kwenye jambo hili maalum katika kipindi cha “Mungu wa Miujiza” kinachorushwa na kituo cha “Jesus Set Me Free”, yaani “Yesu Aliniweka Huru.”  

**************

Haya ndugu msomaji wa blog hii. Umemsikia dada Miryam. Watu wanazidi kumkimbilia Bwana Yesu. Usiachwe nyuma. Tafakari mambo haya.

Mara nyingi huwa ninasema, dini ni mzigo. Iwe ni ya Kikristo au ni dini nyingine yeyote. Tunachohitaji ni uhusiano wa kibinafsi na Mungu aliye hai, katika Yesu Kristo. Ukiwa na Yesu ndipo hata dini inakuwa na maana. Lakini ukiwa na dini bila Yesu kuwa Mwokozi wako binafsi, unakuwa kwenye matatizo. [Tunaposema Mwokozi binafsi maana yake rahisi ni kwamba, ni Yule ambaye kila wakati, kila mahali, unasema naye juu ya kila jambo. Ukiwa na shida unamwambia. Ukipata kitu unamshukuru – katika hali ya kawaida kabisa. Si lazima kwanza ukae mkao fulani na kuweka uso au mikono kwa namna fulani. Huyu ni Baba yetu; ni Rafiki yetu.]

Bwana Yesu hajawahi kusema kuwa tunatakiwa kuwa Wakristo au watu wa dini fulani ili tuweze kwenda mbinguni. Alisema, "Mwayachunguza maandiko [yaani ya Biblia], kwa sababu mnadhani ya kwamba ninyi mnao uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima" (Yohana 5:39-40). !

Mungu wangu! Yaani kumbe hata Biblia japo yenyewe ni Neno la Mungu, lakini bila Mungu mwenyewe inabaki kuwa ni andiko tu la kwenye karatasi ambalo halimfaidii mtu kitu. Ni lazima Mungu mwenyewe awe ndani yako ndipo Neno lake nalo linakuwa hai! Haleluya!

Njoo kwa Yesu sasa upate uzima wa milele.

No comments:

Post a Comment