Thursday, July 11, 2013

Kufa kwa Yesu Kristo Maana Yake Nini?
Utakatifu

Mungu ni mtakatifu. Kutenda dhambi ni kukosa utii kwa Mungu. Mungu anasema kwenye Neno lake: Basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu. (Walawi 11:45).

Pia imeandikwa: Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu (1 Petro 1:15).

Kwa kifupi, kuwa mtakatifu maana yake ni kutokuwa na dhambi yoyote. Mungu kamwe hawezi kufumbia macho dhambi hata iwe ni moja. Kamwe! Hafumbii macho hata zile dhambi ambazo sisi tunaziona ni ndogo sana.


Hata kama mtu angeishi maisha ‘safi kabisa’ kisha akaja akatenda dhambi moja tu ‘ndogo’ kabla ya kufa, mtu huyo ataingia kwenye jehanamu ya moto kwa sababu sheria ya Mungu inasema kuwa mshahara wa dhambi ni mauti – haisemi mshahara wa dhambi nyingi; inasema tu mshahara wa dhambi!

Tumeitwa kuishi maisha matakatifu, yasiyo na dhambi mbele za Mungu Aliye Mtakatifu ili aweze kutupokea kwenye mikono yake mitakatifu.

Hali ya Dhambi ya Mwanadamu

Utakatifu kamwe si kujaribu au kujitahidi kufanya mambo mema maishani mwetu. Ni zaidi ya hapo. Bwana anasema kuhusu sisi: Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi (Isaya 64: 6). Vilevile anasema kwa msisitizo kuwa: Hakuna mwenye haki hata mmoja. (Warumi 3:10). 

Tunafahamu kuwa maziwa yaliyochemshwa ni salama. Lakini, utafanyaje endapo mtu atayachemsha kisha akakuwekea kwenye kikombe kichafu? Je, huko kuchemshwa kutakuwa bado na maana yoyote? Kwa hakika, ingawaje yatakuwa yamechemshwa, utakataa kuyanywa.

Hivyo ndivyo Mungu anavyotuona tunapojaribu kufanya matendo mema lakini si kulingana na sheria yake. Matendo mema ni mazuri kama ilivyo kwa maziwa yaliyochemshwa. Lakini sisi ni kama vikombe vichafu ambavyo vinayachafua na kuyafanya yapoteze uzuri wake mbele za Bwana.

Kwa asili, moyo wa mwanadamu si safi; kwa hiyo, kile kinachotoka humo nacho kinakuwa si safi. Japokuwa kwa nje matendo yetu yanaweza kuonekana mema mbele za watu wengine, kamwe hayawezi kufikia viwango vya Mungu.

Bwana anasema: Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano (au sahani), na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.  (Mathayo 23:25-26). Mwonekano wa kuvutia wa Mafarisayo ulikuwa machukizo mbele za Mungu kwa kuwa cha maana kwa Mungu ni kile kilichomo moyoni mwa mtu, yaani nia yake.

Baada ya anguko, Adamu na Eva walipoteza utakatifu wa Mungu ambao uliwafunika, halafu badala yake wakafunikwa na kifuniko cha asili ya dhambi.  Hawakutenda dhambi nyingi. Ilikuwa ni dhambi moja tu! Walikula tunda walilokatazwa.

Biblia inasema: Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. (Mwanzo 3: 6).

Huu ulikuwa uchafu uliotosha kumtenga mwanadamu na Muumba wake. Vinginevyo walitakiwa wajisafishe hadi uchafu huo utoke kabisa. Tayari kulikuwa na bonde kubwa sana lililomtenga mwanadamu mdhambi na Mungu aliye Mtakatifu milele.

Hata kama Adamu na Eva wangekuwa tayari kutoa sadaka kwa ajili ya dhambi yao, wangewezaje? Wakiwa tayari ni wenye dhambi (vikombe vichafu), ilikuwa haiwezekani tena kamwe kumtolea Mungu sadaka inayokubalika. Mungu Mtakatifu hawezi kukubali kitu kutoka kwa mtu aliye mchafu. Bwana anasema:  Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye. (Ayubu 14:4).

Vilevile anasema: Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu? Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake; punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? (Yeremia 2:21-24).

Ndiyo, Adamu aliumbwa akiwa mtakatifu, lakini aligeuka kuwa mchafu. Juhudi zozote ambazo angefanya za kujisafisha zingekuwa ni kazi bure. Kama ilivyo kwa punda, asili yake sasa ilikuwa tofauti isiyoweza kamwe kuendana na utakatifu wa Mungu. Alishajiharibu. Punda hata akijitahidi vipi, kamwe hawezi kugeuka kuwa ng’ombe au mnyama mwingine yeyote.

Mungu alipomzuia Adamu kula matunda, alisema: usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. (Mwanzo 2: 17). Sheria ya Mungu inasema: Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23).

Je, Tunaweza Kujibadili?

Kama tukijikagua wenyewe kwa uaminifu kabisa, tutagundua kuwa sisi ni watenda dhambi kwa asili. Tunafahamu kabisa kuwa hasira, uchoyo, wizi, kukosa uaminifu, chuki, kutamani, uongo, n.k. ni mambo maovu; na kipimo kinachoonyesha wazi kuwa ni mambo maovu ni kuwa sisi wenyewe hatupendi mtu atutendee mambo hayo. Lakini  ajabu ni kuwa sisi wenyewe tuko hivyo.

Tunatafunwa na hatia ndani yetu kutokana na kuwa hivyo. Kwa ndani, tunatamani kuwa watu bora zaidi, lakini tunakuta kuwa haiwezekani kubadili hiyo asili yetu. Na hivyo ndivyo inavyotakiwa tuwe. Yaani tunatakiwa kushindwa!

Hata pale tunapojaribu kuwa wema mbele za watu wengine, baada ya muda mfupi tunajikuta tumekwama tu. Jitihada zetu kamwe hazitaweza kufanikiwa! Sisi ni wa kushindwa tu! Bwana anatupa changamoto kwa kusema: Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; nimetakasika dhambi zangu? (Mithali 20:9).  Kwa sababu ya dhambi, mwanadamu alikuwa amepotea milele.

Kama Adamu na Eva wangezaa watoto kabla ya kuanguka dhambini,watoto wao wangekuwa wamezaliwa chini ya utakatifu. Lakini sasa walizaa watoto baada ya uasi. Hivyo, watoto hao walikuwa wamezaliwa chini ya dhambi. (yaani, tayari dhambi ilikuwa ulimwenguni). Sisi ni watoto wao. Imeandikwa: Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. (Warumi 5:12).

Kwa kifupi, wanadamu wote walikuwa sasa wanaelekea kwenye upotevu wa milele; maana mbingu haina nafasi kwa watu wenye dhambi. Mbingu ni makao ya Mungu Mtakatifu na yeyote mwingine aliye mtakatifu kama Mungu. Imeandikwa: Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27).

Kumbuka kwamba, Mungu ni mkamilifu. Mungu kamwe huwa hakosei kitu chochote. Yeye ana nguvu zote na anajua yote. Kutokana na nguvu zake na kujua yote, hataruhusu kamwe hata dhambi moja ‘ndogo’ iingie kwenye mbingu zake zilizo kamilifu.  Ametuumba hivi tulivyo ili tumtegemee yeye peke yake kwa asilimia zote. Yesu anasema: Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. (Yohana 15:5-6).

Hebu nisisitize tena kwamba, kwa Mungu, mtu anapotenda dhambi, hakuna jingine kwake zaidi ya kuingia kwenye mauti, yaani kutengwa na Mungu milele.

Dhabihu kwa Ajili ya Kusamehewa Dhambi

Mungu anampenda mwanadamu mwenye dhambi (hii ni sawa na kusema, anatupenda sote; maana sote tu wadhambi). Lakini hawezi kuvumilia dhambi. Kwa vile mwanadamu ametenda dhambi, basi mwanadamu alitakiwa afanye jambo kuhusiana na hali yake ya dhambi ili aweze kutoka kwenye mauti ambayo sasa alishaingia.

Sheria ya Mungu inasema: na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo (Waebrania 9:22). Vilevile imeandikwa: Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu. (Walawi 17:11). Hii ina maana kuwa, dhambi inaweza kulipwa kwa kumwaga damu tu. Lakini kwa kuwa tumeona kwamba damu ya mwanadamu imechafuliwa na dhambi, basi haiwezi kukubalika kuwa sadaka kwa ajili ya ondoleo la dhambi.

Sababu ya damu ya mwanadamu kutokubalika ni kwamba sheria ya kumwaga damu inasema: Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa  BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu. Ng’ombe au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa ya kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa. Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu. Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu. (Walawi 22: 22-25).

Mwanadamu alishatiwa mawaa na dhambi. Hata kama tukidhani kwamba tunaweza kufanya matendo mema au hata kujitoa wenyewe tufe ili Munngu atusamehe dhambi zetu, tutakuwa tunapoteza tu muda na roho zetu. Ilikuwa ni lazima damu imwagwe kutoka kwa mnyama mkamilifu ambaye hakuwa na mawaa hata kidogo. Kama wanyama walikuwa na dosari yoyote, Mungu anasema kuwa wanyama wanaotolewa kuwa sadaka hawatakubaliwa kwa ajili yenu.

Sasa unaweza hata kuelewa kile ambacho Yesu alimaanisha pale aliposema: Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la sikuja kuitangua, bali kuitimiliza. (Mathayo 5:17).  Alimaanisha kuwa, kama masharti ya Mungu hayatatimizwa (kuhusiana na dhambi kwa upande wetu), hakuna roho hata moja ambayo ingekwepa jehanamu ya moto. Kwa nini? Kwa sababu KAMWE Mungu hatafumbia macho dhambi hata iwe ni moja tu. Kila dhambi inahukumiwa kwa kifo. Sharti hilo ni lazima litimilizwe. Yesu alikuja ili kutimiliza hitaji hilo la sheria kwa kuwa mwanadamu hana kabisa uwezo wa kulitimiza!

Vilevile, ina maana kuwa kwa vile sheria inadai mwana-kondoo MKAMILIFU, yeye ndiye alikuja kutimiliza hitaji hilo.

Tunaweza vilevile kuelewa pale sheria ya Bwana inaposema: na atakayempiga mnyama hadi akafa atalipa; uhai kwa uhai. Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vilevile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vilevile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo. Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa. Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. (Walawi 24: 18-22).

Kwa hiyo, unapotenda dhambi, unakuwa na hatia ya uuaji kwa kuwa umesababisha mauti kwa roho iliyo mali ya  Mungu (yaani ni hiyohiyo roho ambayo ndiyo wewe). Hii ni kwa sababu Bwana anasema: Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa. (Ezekieli 18:4). Pia anasema: ... wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. (1 Wakorintho 6:19-20).

Na sasa, kwa kuwa una hatia ya mauaji kutokana na kutenda dhambi, kulingana na sheria, muuaji ni lazima naye auawe. Lakini kumbuka kwamba, hata kama ukiuawa, hiyo hailipii hatia yako na kukuwezesha kuingia mbinguni. Kwa nini? Kwa sababu unauawa tu kama adhabu, na si kama sadaka au dhabihu ya dhambi. Sisi hatukubaliki kama dhabihu kwa kuwa tumetiwa mawaa na dhambi.

Baada ya kusema hayo, hebu sasa tugeukie swali letu la msingi. Kwa nini Yesu alikufa?

Kutokana na shetani kufanikiwa kuvunja uhusiano kati ya mwanadamu na Mungu kwa kumfanya mwanadamu atende dhambi, mambo manne muhimu yalitokea:
1.    Sasa mwanadamu alikuwa mdhambi; muuaji, ambaye kulingana na sheria, naye ilibidi auawe.
2.    Hakukuwapo na dhabihu iliyokubalika mbele za Mungu kwa ajili ya kulipia dhambi ya mwanadamu.
3.    Juhudi zozote ambazo mwanadamu angefanya ili kujiokoa kutoka kwenye hukumu ya kifo ambayo Mungu alishamwonya dhidi yake,  zisingefanikiwa kamwe.
4.    Tayari mwanadamu alishapotea.

Kwa kusukumwa na upendo wake mkuu kwetu, Mungu kupitia Yesu alishuka chini kuja kutafuta na kuokoa kilichopotea, yaani sisi.

Kumbuka kuwa, Adamu na Eva walipomsikiliza ibilisi na kutenda dhambi, Mungu alikuja bustanini kama ilivyokuwa kawaida yake, lakini walikuwa hawaonekani. Ndipo Bwana akauliza: Uko wapi? (Mwanzo 3:9). Si kwamba Mungu alikuwa hawaoni, lakini walikuwa wamepotea kwenye mpango wa Mungu wa uzima wa milele. Walikuwa tayari wamekufa, japo walikuwa bado wanatembea.

Kwa hiyo, ilibidi kwanza Yesu apate mwili. Imeandikwa kuhusu Yeye: Kwa hiyo, ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari. (Waebrania 10:5). Mwili ndio uliomwezesha kuwa mwanadamu. Kulingana na 1 Cor. 15:45, Yesu alifanyika Adamu wa pili. Biblia inasema: Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. (1 Wakorintho 15:47). Kuwa na mwili, vilevile kulimwezesha kuwa na damu.

Kwa kuwa Yeye ni Mungu, hakuwa na dhambi na hakutenda dhambi katika maisha yake yote hapa duniani. Imeandikwa: bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. (Waebrania 4:15). Hali hii ilimfanya astahili kuwa Mwana-Kondoo asiye na mawaa (dhabihu kamilifu kabisa) kwa ajili ya dhambi.

Kisha dhambi ZOTE za ulimwengu ziliwekwa juu yake na Mungu kwa kuwa Yeye mwenyewe alishakubali kuzibeba kwa niaba yetu. Yohana mbatizaji alipomwona Yesu wakati fulani, alisema:  Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! (Yohana 1:29).

Lakini licha ya maisha yake matakatifu na yasiyo na dhambi, ulifika wakati ambapo Yesu alikamatwa, akateswa, na kuuawa kwa ajili ya dhambi zangu na zako.

Ndipo mambo makuu mawili yalitokea:
1.    Wakati tungali wenye dhambi ambao, kulingana na sheria ya Mungu, tulitakiwa kuuawa, Yesu alitimiza dai hilo la sheria kwa kubeba dhambi zetu juu yake na kuzifia kwa niaba yetu ili hukumu hiyo ya sheria itimie na kusiwepo madai tena.
2.    Kwa kuwa kama sisi tungekufa kwa sababu ya dhambi tungepotea milele, Yesu alitupatia kitu kingine. Japokuwa sasa Mungu alimwangalia Yesu kama mtu mwenye dhambi (kutokana na kubeba mzigo wa dhambi zetu), ukweli kwamba Yeye mwenye binafsi hakutenda dhambi yoyote, ulimpa haki ya kufufuliwa.

Kwa hiyo, si tu kwamba alikufa ili sisi tusamehewe makosa yetu, lakini pia alifufuliwa kutoka kwa wafu kwa sababu nyingine ya muhimu sana. Biblia inasema kwamba: ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki. (Warumi 4:25). 

Tunapoiamini kazi hii ambayo Bwana alifanya kwa niaba na kwa ajili yetu, tunasamehewa na kupewa haki ya kuwa watu wasio na dhambi kabisa mbele za Mungu, yaani ni watakatifu!

Hebu tafakari mfano ufuatao. Mwanafunzi anapoandikishwa shuleni, shule huwa na sheria kuwa ni LAZIMA kwanza mwanafunzi alipe ada ndipo aruhusiwe kuingia shuleni na darasani. Lakini, kwa kawaida,  mwanafunzi huwa hana kipato. Kwa hiyo, hawezi kabisa kulipa ada. Badala yake mzazi wake, ambaye hataenda kusoma, analipa ada na huyo mwanafunzi anahesabika kuwa ameshalipa ada kabisa.

Lakini huyo mwanafunzi akisema, “Mimi sina fedha za ada, kwa hiyo naondoka,” tatizo litakuwa la mzazi au la mwanafunzi? Anaweza akatokea mtu akamwambia, “Ada yako imeshalipwa. Wewe ingia tu darasani usome.”

Ndivyo alivyofanya Yesu kwa ajili yangu na yako. Alishalipa ada yetu ya mbinguni kwa uhai wake mwenyewe. Wajibu wangu ni kupokea tu kwa imani kile alichofanya kwa ajili yangu.

Mauti ya Yesu ilikuwa njia pekee ya mwanadamu kuokolewa. Hakika huu ni udhihirisho wa upendo mkuu sana; kukubali kufa ili mwingine aweze kuishi!

Hebu jaribu kupiga picha ya mwanadamu wa kawaida tu aamue kwenda gerezani kutumikia kifungo cha maisha ili muuaji, ambaye ndiye alihukumiwa, aweze kuwa huru na kwenda kuendelea na maisha nje ya gereza!

Yesu alifanya zaidi ya hapo! Nabii Isaya anapaza sauti yake kwa nguvu zaidi kuhusu Yesu akisema: Alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu; lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; na BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; kama mwana-kondoo apelekwaye machinjioni, na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatao manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa; na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; na pamoja na matajiri katika kufa kwake; ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

Lakini BWANA aliridhika kumchubua; amemhuzunisha; utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, ataona uzao wake, ataishi siku nyingi, na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake.  (Isaya 53:3-10).

Ilibidi Yesu, ambaye ni Mwana-Kondoo mkamilifu, afanye hivi kwa sababu masharti ya Muumba aliye mkamilifu hayawezi kamwe kutimizwa na kiumbe ambaye si mkamilifu!

Je, Sehemu Yangu ni Nini Basi?

Kama Mungu alishafanya yote yanayohitajika, sehemu yangu katika mpango wake wa wokovu ni ipi?
1.    Natakiwa kukubali ukweli ulio wazi kuwa mimi ni mwenye dhambi ambaye nimetengwa na Mungu kutokana na asili yangu ya dhambi. Imeandikwa:  kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. (Warumi 3:23).
2.    Ni lazima nikiri ukweli kwamba sitaweza kuacha kutenda dhambi kwa juhudi zangu mwenyewe.
3.    Ni lazima niamini kuwa Yesu alikufa na kufufuka kwa niaba yangu. Kwa njia hiyo Mungu atanichukulia kuwa nimeshalipa gharama ya dhambi zangu (yaani mauti) kupitia Yesu; kisha atanihesabia haki ya kuingia mbinguni kupitia ufufuko wa Yesu. Biblia inasema: ambaye Mungu amekwisha mweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. (Warumi 3:25).
4.    Ni lazima nitubu dhambi zangu na kukusudia kutozirudia tena, badala yake niishi kulingana na Neno la Mungu.
5.    Ni lazima nimwombe Yesu kwa imani anisaidie kwa Roho wake Mtakatifu kuishi maisha matakatifu. (kumbuka, Mungu ni halisi, Yesu ni halisi, Roho Mtakatifu ni halisi – wanasikia, wanaona, wanaelewa, n.k. Kwa hiyo, unapoomba au kusema nao, fanya kama ambavyo ungefanya kwa baba au rafiki yako wa kimwili); na Mungu ni mwaminifu; atakusaidia kuishi maisha ya ushindi. Imeandikwa: Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. (Warumi 5:10).

Kupokea Wokovu kwa Imani

Kila kitu tunachopokea kutoka kwa Mungu, tunakipokea kwa kuamini kile anachosema tufanye kwenye Neno lake. Bwana anasema: Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), au Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.) Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.  (Warumi 10:6-11).

Unaweza kubadili historia ya maisha yako milele sasa hivi hapa hapa! Tafadhali, sema sala ifuatayo kwa moyo wako wote na upokee wokovu wa bure kutoka kwa Bwana sasa hivi (ingawaje, neno bure halimaanishi ni wokovu wa bei chee, maana ulilipiwa gharama kubwa sana). Basi sema:

Bwana Yesu, Nakubaliana na ukweli kwamba mimi
ni mwenye dhambi; Pia nakiri kwamba siwezi kushinda
dhambi kwa nguvu zangu mwenyewe. Nakubali kuwa
siwezi kujiokoa mwenyewe; Vilevile, sina uwezo wa kutoa
sadaka yoyote kwa ajili ya dhambi zangu ambayo
inakubalika kwa Mungu mbali na uhai wako ambao uliutoa
kama sadaka kwa ajili ya dhambi zangu.

Nisamehe dhambi zangu, Bwana. Nisafishe kwa damu yako
takatifu ambayo ilimwagika msalabani kwa ajili yangu. Karibu kwenye moyo wangu na ukae nami daima. Nipatie Roho wako Mtakatifu.

Niwezeshe kushinda asili yangu ya dhambi ili niweze kuishi
maisha matakatifu yanayokubalika mbele zako.

Asante kwa kujibu maombi yangu na kwa kuniokoa.
Ni katika jina la Yesu, nimeomba, Amin

No comments:

Post a Comment