Sharoni hakuwa Mkristo
bali alikuwa ni binti wa Kiislamu. Na wala hakuwa amewahi kujifunza habari za
Yesu na Ukristo. Lakini Bwana Yesu mwenyewe alimfuata na kujidhihirisha kwake. Je,
ilikuwaje, na nini kilitokea baada ya hapo? Tafadhali fuatilia ushuhuda huu
wenye nguvu na unaodhihirisha upendo na uweza na uungu wa Bwana Yesu.
……………………………….
Jina langu ni Sharoni
Sabina Natrajan. Kwa sehemu kubwa ya maisha yangu nilikulia Bombay. Familia yangu
si Wakristo. Kwa hiyo sikuwahi kupata mafundisho yoyote ya Kikristo. Natokea kwenye
familia ambayo inathamini sana elimu, na kila mtu ana elimu ya kutosha. Upande wa
mama yangu, anatokea kwenye ukoo wa Zaminda. Na hata nyakati zile, wavulana na
wasichana walikuwa na elimu kubwa.
Baba yangu ni injinia
ambaye amesoma kwenye chuo kinachoheshimika sana, na anashikilia cheo kikubwa
kwenye makampuni ya kimataifa hapo Bombay.
Sisi ni familia ndogo tu
yenye mimi, dada yangu, baba na mama. Tangu nikiwa mdogo, nilikuwa ni mtu ninayependa
masuala sanaa (creative arts). Nilisomea na kuhitimu katika sanaa za maonyesho
na pia uchoraji. Kwa hiyo, maisha yangu yote ya utotoni yalikuwa yamejikita
kwenye mambo haya.
Wazazi wangu walikuwa na
upendo sana na nilipata kila nilichohitaji. Sikupungukiwa na chochote maishani
mwangu.
Baba yangu alipenda sana
nisomee uinjinia, licha ya kuwa wakati nikiwa sekondari ya juu nilikuwa tayari
nikifanya sanaa za maonyesho kote nchini – kucheza ngoma, maigizo,n.k. Sasa,
kwa kuwa alitaka niwe injinia, nilituma maombi na kupata nafasi kwenye chuo
kizuri sana. Uinjinia haukuwahi kuwa jambo la moyoni mwangu, lakini nilifanya
hivyo ili tu kuwafurahisha wazazi wangu. Kwa hiyo, nilienda Puna kusomea
uinjinia lakini wakati huohuo nilikuwa nikifanya sanaa za maonyesho.
Nilipokuwa kule Puna
katika muhula wa pili, kuna jambo lililotokea ambalo lilibadili kabisa maisha
yangu. Nakumbuka siku moja nilikuwa chumbani peke yangu nikijisomea, maana
mitihani ilikuwa karibu. Nakumbuka vizuri sana siku hiyo nilikuwa ndani,
naandika huku nimefunga mlango kwa ndani ili nisisumbuliwe na watu.
Ghafla, nilisikia sauti
ikiniambia niombe! Cha kwanza nilichofanya ilikuwa ni kugeuka na kuangalia. Nilipogeuka
na nikawa sioni mtu, cha pili kilichotokea ni kuingiwa na hofu ya kwamba labda
nachanganyikiwa! Inakuwaje nasikia sauti? Kuna kitu kisicho kizuri hapa!
Niliamua kuipuuza ile
sauti na kuendelea kusoma. Lakini sauti ile iliniita tena jina langu na
kunitaka niombe! Sikuwa na uwezo wa kuipuuza tena sauti ile ambayo iliendelea
kunijia, ungedhani iko kila mahali kunizunguka.
Niliangalia saa yangu nikakuta
ilikuwa ni saa 7:30 mchana. Na nikakumbuka kwamba katika kukua kwangu, wazazi
wangu walinifundisha dini yao. Nami nilikuwa nikifanya yanayotakiwa kwenye dini
hiyo lakini kama mazoea tu kulingana na hayo niliyofundishwa.
Walinifundisha namna ya
kuomba lakini katika muda maalum. Kwa hiyo, nilipoangalia ile saa yangu,
niligundua kuwa muda wa swala ulishapita. Na sikujua namna ya kuomba. Nilikaa tu
pale nikiwa nimechanganyikiwa huku sijui cha kufanya. Wakati huohuo sikuwa na
uwezo wa kuipuuza ile sauti.
Kwa hiyo nilifunga tu
macho yangu na kukaa tu pale; kisha nikasema moyoni mwangu kwamba, “Sijui huyu
ni nani anayenitaka niombe, lakini kama kuna Mungu kwenye dunia hii, nataka
nikuone. Sijawahi kukuona; sijui kama kuna Mungu au hakuna Mungu. Lakini kama
kuna Mungu na ni halisi, basi nataka kumwona Mungu wa kweli.”
Nilisema tu hivyo moyoni
mwangu na kwa mara ya kwanza maishani mwangu, macho yangu yakiwa yamefungwa,
niliona maono. Nilimwona mtu amesimama mbele yangu. Kulikuwa na nuru kubwa. Sikuweza
kuona uso wake. Lakini nilitambua mara moja moyoni mwangu kwamba huyu alikuwa
ni Yesu! Hakukuwa na shaka yoyote. Yeye hakusema kuwa ni Yesu lakini nilijua tu
kuwa huyu alikuwa ni Yesu.
Kilichofuata hapo
nilijikuta nimepiga magoti na machozi mengi yakawa yananibubujika. Kulikuwa na
upendo mkubwa uliokuwa unatoka kwake. Nilikuwa nashindwa kujizuia kulia;
niliendelea tu kulia. Pia ilikuwa kama vile naweza kutazama moyo wangu; na
nikawa naona madoa mengi meusi; mambo ambayo hata sikujua kuwa nilikuwa nayo. Nilitambua
kuwa nilikuwa nina kiburi kikubwa; nilikuwa mwenye kujihesabia haki. Kila kitu
kilikuwa sawa tu maishani mwangu na sikujua kabisa kuwa nilikuwa na hali hiyo
ndani yangu! Nilikuwa mbinafsi sana. Nakumbuka nilipiga magoti na kulia na
kusema, “Yesu, mimi sijui wewe ni nani lakini nakuhitaji katika maisha yangu.” Niliendelea
kulia na kusema hivyo.
Baadaye alitoweka. Nilipofungua
macho yangu na kuangalia saa, ilikuwa ni saa 8:15. Nikatambua kuwa kwa dakika
45 nilikuwa katika hali ile!
Baada ya hapo niliingiwa
na woga. Niliwaza kuwa hapa ni lazima nimechanganyikiwa. Lazima kuna tatizo! Nilitoka
mbio chumbani na jina lililonijia kwanza akilini mwangu lilikuwa la msichana
mmoja ambaye alikuwa ni Mkristo pekee pale bwenini.
Nilienda kwenye chumba
chake na kukuta amelala. Nilimwamsha na kumwabia, “Unajua, nilipoomba nimwone
Mungu wa kweli, nimemwona Yesu! Kwa nini nimemwona Yesu wakati mimi si Mkristo?”
Nadhani na yeye aliogopa
kunitazama maana macho yangu yalikuwa mekundu kutokana na kulia. Hakujua cha
kufanya. Alikuwa ana Biblia. Alinipatia na kusema, “Soma kitabu hiki kama Yesu
amejionyesha kwako.” Niliichukua ile Biblia na kurudi nayo chumbani kwangu. Na kuanzia
saa 2 usiku nilianza kuisoma. Niliendelea kuisoma hadi saa 9 alfajiri! Sikuwahi
kusoma kitabu kama kile maishani mwangu! Ilikuwa kama vile maneno yanaongea na
mimi. Kilikuwa ni kitabu kilicho hai!
Kulipokucha, siku tatu
zilizofuata zilikuwa ni kama vita kwenye mawazo yangu. Kwa nini nimemwona Yesu?
Huyu Yesu ni nani?
Si kwamba kuna mtu alikuja
kunieleza kuhusu Yesu. Sikuwa nimewahi hata kuingia kanisani! Nilichokuwa najua
tu ni kwamba Yesu alikuwa ni Mungu wa Wakristo. Basi! Sikuwa na rafiki Mkristo;
wala sikuwahi kuwa na shauku yoyote ya kumjua Yesu au kwenda kanisani kabla ya
hapo. Na wala sikuwa namtafuta Mungu! Wala sikuwa napita kwenye jambo lolote
gumu. Sasa kwa nini nimemwona Yesu?
Kwa siku hizo tatu, vita
hii iliendelea kwenye akili yangu. Baba yangu alinifundisha mara zote kutumia
akili yangu katika kutafuta mantiki ya mambo mbalimbali ili kutatua matatizo
ninayokutana nayo maishani. Hicho ndicho nilichojifunza maishani mwangu. Lakini
kwa jambo hili lililokuwa limenitokea, sikuwa na namna kabisa ya kupata mantiki
yake; na wala sikuweza kujua cha kufanya kutokana na kile nilichokiona.
Kwa hiyo, baada ya siku
tatu nilienda kwa huyu rafiki yangu tena na kumwambia, “Inabidi unieleze zaidi
kuhusiana na huyu Yesu.” Hapo ndipo aliponipeleka kwenye mkutano wa wanafunzi.
Kuanzia siku hiyo,
nilianza kusoma zaidi Biblia na kujua mengi zaidi kuhusiana na Yesu. Mungu alifanyika
kuwa halisi kwangu. Ghafla tu alikuwa hai maishani mwangu na niliweza kuwa na
uhusiano na huyu Mungu. Niliweza hata kuonga naye; na kumwomba – si kama jambo
la mazoea tu (kama zamani), lakini nilikuwa sasa na uhusiano naye kibinafsi
sana.
Nilitambua kuwa, kama kuna
Muumba, basi Muumba huyu ni lazima atataka kuwa na uhusiano na viumbe wake. Na hicho
ndicho kilichotokea kwangu. Ilikuwa ni kama sasa nimeunganishwa na Muumba
wangu.
Kadiri nilivyoendelea
kusoma Biblia na kumjua zaidi Yesu, nilianza kuona mambo kwa namna tofauti
kabisa. Nilianza kuelewa nini maana ya huruma, kusamehe, rehema. Mambo haya
yalikuwa mageni kwangu. Sikuwahi kujua juu ya mambo haya kabla. Na maisha yangu
yalibadilika. Nilianza kuwaona watu kwa jicho la tofauti; na Yesu akawa rafiki
yangu.
Siku zilivyozidi kusonga mbele,
sikuweza kuelezea mabadiliko haya kwa wazazi wangu, na wao nao mwanzoni hawakuweza
kuelewa. Iliwachukua muda mrefu kuja kuelewa.
Nilifika mahali ambapo
ilinibidi kufanya uamuzi mgumu. Wazazi wangu hawakutaka mimi nimfuate Yesu. Ilinibidi
kuchagua kati ya kumwacha Yesu au kuwaacha wazazi wangu. Ikanibidi kufanya
uamuzi mchungu sana wa kuwaacha wazazi wangu; na nilijua kuwa lingekuwa ni
jambo la kitambo kifupi tu hadi pale nitakapopata uwezo wa kueleza mabadiliko
yaliyokuwa kwangu. Na ujue, mabadiliko haya hayakuwa jambo la nje tu; lilikuwa
ni jambo lililotokea ndani. Ilikuwa ni kama nimefunguka kwa namna fulani. Nilikuwa
gizani na ghafla nikawa nimeona nuru.
Kwa hiyo, ulikuwa ni
wakati mgumu sana nilioupitia ambapo sikuwa na mawasiliano yoyote na wazazi
wangu. Lakini Yesu alikuwa pamoja nami wakati wote; na alinipeleka hatua kwa
hatua maishani mwangu.
Nilikuja Chenai kutokea
Bombay na nikaanza kufanya kazi kwenye sekta ya matangazo ya biashara. Nilikuwa
nafanya vizuri sana. Nikaanza kushughulikia akaunti kubwakubwa za makampuni ya
kimataifa. Lakini mara katika mwaka mmoja, kulikuwa na anguko la kiuchumi
katika sekta hii. Makampuni yalikuwa yanafungwa. Ilinibidi nami niondoke kwenye
kampuni yangu ili niende kufanya kazi kwenye kampuni nyingine.
Wakati ule nilikuwa
nashughulika akaunti za mteja wangu mmoja. Hivyo, nilimwendea na kumwambia kuwa
naondoka kwenye kampuni hii maana nimepata kazi kwingine. Mteja wangu alikuwa
ni mteja mkubwa kabisa miongoni mwa mashirika ya umma nchini. Aliniangalia na
kusema, “Ninafurahishwa sana na kazi yako. Ningependa uendelee kufanya kazi na
sisi.”
Nilimtazama tu kwa
mshangao na kujiuliza, “Nitaendeleaje naye ilhali kampuni niliyokuwa nafanyia
kazi zake imefungwa?”
Akasema, “Kinachotakiwa ni
wewe kuwa tu na kampuni kisha mimi nitakupatia kazi hizi zote.” Nilishangaa kweli!
Hapo ndipo nilipoanzisha kampuni yangu mwenyewe ya matangazo ya biashara. Nakumbuka
nilianzia kwenye duka la juisi. Nilikuwa nikikaa kwenye duka hilo na kufanya kazi zangu. Nilimwambia mwenye duka, “Uwe
unanipatia juisi kila baada ya saa mbili au tatu.”
Baada ya hapo hakukuwa
tena na kugeuka nyuma. Kazi niliyoifanya kwa ajili ya ile sekta ya umma
ilijulikana nchini kote! Kisha kazi zilifuatana moja baada ya nyingine. Niliweza
kupata ofisi yangu mwenyewe. Ilifika wakati ambapo nilikuwa na watu 150
wanaofanya kazi! Baada ya hapo nilianzisha kampuni nyingine na Wamarekani
wawili wanaoishi Wisconsin.
Katika yote haya, nimeona
jinsi Mungu wangu; Yesu wangu alivyonisaidia. Maana nilipolazimika kuiacha
familia yangu ili niweze kumfuata Yesu, wakati huo nilikuwa sina kitu. nilikuwa
tu na elimu yangu basi. Kisha nilianzisha kampuni yangu ambayo ilikua kutoka
hatua moja hadi nyingine.
Kwangu, ilikuwa ni Yesu
pekee aliyeniwezesha kuyafanya yote haya. Aliniongoza kwenye safari yote maana
Biblia ilifanyika kuwa kitabu changu cha kila siku. Niliisoma na kupata kila
maelekezo, na kutiwa moyo, na kutiwa hamasa. Ilinipa matumaini; ilinipa uzima
mpya. Kila kitu kuhusiana na maisha nilikikuta kwenye Biblia. Na hivyo ndivyo
nilivyotoka ngazi moja hadi nyingine.
Hatimaye, mimi pamoja na
baadhi ya marafiki zangu na mume wangu ambao nilikutana nao Chenai, tulithubutu
kuanzisha chuo cha sanaa na ubunifu (art and design).
Ninapotazama nyuma katika
maisha yangu, naona kabisa jinsi ambavyo Yesu amehusika sana kuanzia wakati
ambapo sikumjua Yesu na baada ya kumjua. Ilikuwa ni kama nimepata makusudi ya
kuishi kwangu. Haikuwa kana kwamba nilikuwa natafuta kitu au kwamba mambo
yalikuwa yanakwenda kombo maishani mwangu, hapana. Lakini kuanzia pale
nilipomgundua Yesu, na kuanza kumjua, mambo yalibadilika. Maisha hayakuwa tena
suala tu la kuwa na familia nzuri; elimu nzuri; kazi nzuri. Maisha yalikuwa
sasa na makusudi; yalikuwa na maana. Nilikuwa nina maono kwa ajili ya maisha
yangu. Hilo lilibadili mtazamo wangu mzima juu ya maisha.
Nilitambua kwamba Yesu si
dini, bali ni halisi kwangu. Na cha muhimu kabisa, baada ya miaka 10, hatimaye
nilipatana na familia yangu! Hivi sasa familia yangu wananikubali vivi hivi
nilivyo. Wanaona mabadiliko yaliyo ndani yangu, na wananikubali hivi nilivyo. Haya
yameweza kutokea kwa sababu tu ya imani yangu kwa Mungu wangu ambaye ni Yesu
Kristo!
No comments:
Post a Comment