Nabeel alizaliwa na
kukulia kwenye familia na maisha ya kiislamu. Uislamu ulikuwa ni kila kitu
kwake. Lakini wakati ulipofika wa yeye kujua jema na baya, alianza kujihoji
kuhusu maisha yake, Mungu wake, na hatima yake ya milele. Hatimaye alimwomba
Mungu amwonyeshe kweli. Je, nini kilitokea? Tafadhali fuatilia sehemu hii ya
kwanza ya ushuhuda huu.
……………………………………
Nilipokuwa mdogo, wazazi wangi walikuwa wacha
Mungu sana. Mimi nami nilikuwa mcha Mungu sana kwa sababu yao. Wazazi wangu
walinifundisha kumwomba Allah kila wakati. Niliswali sala tano kwa siku ambazo
ni za lazima. Lakini pia niliswali swala zaidi ya hizo. Swala ilikuwa ni sehemu
muhimu kabisa ya maisha yangu. Kila nilipoamka asubihi niliomba mara tu
nilipofungua macho yangu. Kisha nilipoenda bafuni, nilikuwa nikiomba swala ya
wakati wa kuosha mikono yangu. Pia niliomba swala kabla ya kusoma Quran na mara
baada ya kusoma Quran, ambayo niliisoma karibu kila siku.
Uislamu ulikuwa ndani
yangu kabisa. Hivyo, wazazi wangu walikuwa wananifurahia sana maana nilikuwa ni
aina ya mtoto wa Kiislamu ambaye walikuwa wanajivunia kumlea. Nilitokea kwenye
familia ya kimisionari. Allah na mtume Muhammad walikuwa wanaheshimiwa sana. Allah
alikuwa anaabudiwa muda wote.
Uislamu kwetu haukuwa tu
ni dini, bali ulikuwa ni maisha yetu kabisa. Halikuwa ni jambo tulilofuata tu,
bali zaidi sana hivyo ndivyo tulivyokuwa sisi wenyewe. Kwa hiyo, Uislamu
ulikuwa ndiyo sehemu kabisa ya utu wangu.
Kulikuwa na mjadala wa
wazi siku moja nikiwa niko chuoni. Ulikuwa ni mwaka wangu wa kwanza na nikiwa
na miaka 18. Nilikuwa nina rafiki yangu mmoja aliyeitwa David, ambaye alikuwa
kwenye timu ile ya wazungumzaji. Mimi na David tulikuwa tukikaa chumba kimoja. Usiku
ule kabla ya kulala, alitoa Biblia akaanza kusoma. Kusema kweli, nilikuwa
sijaona mtu akisoma Biblia wakati akiwa hana kazi (in free time). Nilikuwa tu nikiona watu wakisoma
wanapohubiri, au wananukuu maandiko wanapoongelea habari zake. Lakini sikuwa
nimeona mtu akiisoma wakati akiwa tu amepumzika.
Nilimwambia, “David,
unajua kuwa Biblia hiyo ilishabadilishwa na watu; si Biblia ileile ambaye alifunuliwa
Kristo?”
David alikuwa ni mtu
ambaye anasoma Biblia, anasoma kuhusiana na Biblia, anasoma sababu za kwa nini
tunatakiwa kuamini Biblia – kwa hiyo, alikuwa yuko tayari kabisa kwa swali kama
hilo kuliko ambavyo ningetegemea.
David aliniambia kwamba
Biblia haijabadilika. Kuna sayansi ambayo inaitwa ‘textual criticism’ ambayo
tunaweza kuitumia ili kubaini kama Biblia imebadilishwa au la. Tulifanya hivyo
na nikagundua kwamba Biblia haijabadilishwa kama inavyodhaniwa.
Niligundua kwamba hakuna
fundisho (doctrine) lililobadilishwa. Biblia imebakia ileile tangu mwanzo.
Biblia inasema kuwa Kristo ni Bwana; na kwamba alikufa kwa ajili ya dhambi
zetu; akafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu; na haijasema kitu kingine
chochote.
Kwa hiyo, ilikuwa ni baada
ya miaka michache, ndipo baadaye nikaanza kutambua kwamba, labda sikuwa kwenye
njia sahihi. Ilinichukua miaka kadhaa ya mijadala na utafiti kugundua ukweli
huu.
Upo ushahidi mwingi sana
unaoonyesha kuwa Biblia imebakia ileile tangu mwanzo; jambo ambalo sivyo kwa
Uislamu. Ilinichukua miaka mitatu na nusu kufikia pale, yaani kutambua kuwa
mambo haya ni kweli; na kwamba kila kitu nilichowahi kufundishwa – nilimpenda Allah,
niliupenda Uislamu, nilimpenda Muhammad, niliwapenda wazazi wangu, nilipenda kila
kitu ambacho nilikulia humo. Lakini hilo halikufanya mambo hayo kuwa kweli.
Nilianza kumwuliza Mungu,
nikisema, “Mungu, siwezi kujua ukweli mimi binafsi. Tafadhali, nionyeshe kweli
ni ipi. Chochote ninachotakiwa kufanya; hata kama kitaniumiza – hata kama
familia yangu itanikataa; hata kama marafiki zangu watanikataa – vyovyote iwavyo,
nitafuata njia hiyo.”
Ninapotafakari leo,
nagundua kuwa hata sikujua sawasawa nilichokuwa nakiomba. Nilimwomba na
kumwomba sana Mungu. Siku moja nilikuwa hotelini na nilimwomba Mungu kwa
unyenyekevu mkubwa sana. Nilisema, “Mungu, sielewi. Siwezi kujua. Uzima wangu
wa milele umo mashakani. Nakuomba uniambie kweli ni ipi – iwe ni kwa maono, kwa
ndoto, au vyovyote vile.”
Usiku ule, nikiwa kwenye
chumba cha hoteli ile, baba yangu alikuwa amelala kwenye kitanda chake na mimi
kwenye kitanda changu pembeni yake. Yeye tayari alikuwa ameshalala. Kulikuwa na
nuru kidogo, lakini mara nilipomaliza kuomba hivyo, kila kitu kilikuwa giza. Hakukuwa
tena na nuru chumbani. Nikaona mbele ya macho yangu, mamia au hata maelfu ya
misalaba! Niliitazama kwa mshangao. Na mara ikapotea.
Nilijua nini kimetokea. Nilikuwa
nimeona maono, lakini bado sikutaka kuamini. Kwa hiyo, nilitazama juu na
kusema, “Mungu, hayo siyahesabu. Inawezekana ni macho yangu tu yamenichezea
mchezo.”
Kisha nikasema, “Unajua
Mungu, tusahau kuwa niliomba unionyeshe maono. Hebu nipe ndoto. Ndoto yoyote tu
ambayo inathibitisha yale niliyoyaona kwenye maono. Ukifanya hivyo, basi
nitakuwa Mkristo.”
Haikuchukua wiki;
haikuchukua mwezi; ilichukua saa chache
tu! Aliniletea ndoto usiku ule! Katika ile ndoto, nilikuwa nimesimama mlangoni
kwa nje. Vidole vyangu vya miguu vilikuwa vimegusa kizingiti. Ulikuwa ni mlango mwembamba wenye urefu na
upana wa kunitosha tu mimi. Kwa ndani,
alikuwapo rafiki yangu, David. Alikuwa amekaa mezani pamoja na mamia ya watu
wengine. Walikuwa wako tayari kula chakula ambacho kilikuwa mezani, lakini
walikuwa hawajaanza kula bado. Walikuwa wanamngoja mzungumzaji aje ili mlango
ufungwe na aanze kusema chochote kile kilichotakiwa.
Nilimtazama David na
kusema, “Nilidhani kuwa tutakula pamoja!” Bila hata kunitazama, David
alinijibu, “Haukuitikia mwito.” [You never responded].
Hivyo tu ndivyo ndoto
ilivyokuwa. Niliamka na mara moja nilitambua ndoto ile ilimaanisha nini. Chumba
kile kilikuwa ni mbinguni; kilikuwa ni Ufalme wa Mungu. Na mimi nilikuwa nimesimama nje tu ya mlango
wa Ufalme huo.
……………………………
Ndugu msomaji, tafadhali
fuatilia ushuhuda huu wa Nabeel katika sehemu ya pili na ya mwisho. Bwana Yesu
akubariki sana.
Tafakari.
Jihoji.
Kweli imo ndani yako.
No comments:
Post a Comment