Katika sehemu ya kwanza ya
ushuhuda huu wa Nabeel, aliyekuwa Mwislamu kisha akakutana na Bwana Yesu na
kupokea wokovu, tuliona jinsi ambavyo alimwomba Mungu ampe maono
yatakayomwonyesha imani ya kweli. Alionyeshwa misalaba kwenye maono lakini yeye
akasema labda ni macho yake tu yamemchezea mchezo. Kwa hiyo, alimwomba tena
Mungu kwamba, kama yale maono yalitoka kwake, basi ayathibitishe kwa ndoto. Je,
Mungu alifanya nini? Tafadhali endelea kusoma sehemu hii ya pili.
…………………………………
Mungu alinipatia ndoto ile
kwa uwazi sana kiasi kwamba sikuwa na ulazima wa kuitafsiri. Lakini ilikuwa
wazi hata zaidi kuliko nilivyotarajia. Saa chache baadaye niliwasiliana na
David na kumwambia kuwa nimeota hivi na hivi.
David aliniambia, “Sina
ulazima wa kutoa maoni yangu juu ya hilo. Kila kitu kiko kwenye Biblia.”
Nikasema, “Unasemaje?”
Akasema, “Nenda kwenye
Luka 13.”
Nilienda kwenye Luka 13
mstari wa 22 hadi 29. Niliposoma nikakuta kumeandikwa kuhusu kuingia kwenye
Ufalme wa Mungu, na Kristo akasema kwamba, wengi watajaribu kuingia lakini
hawataweza. Jitahidini kuingia kupitia mlango mwembamba. Na watu watakuwa
wamesimama kwenye mlango huo wakibisha hodi.
Na hicho hasa ndicho
kilichotokea kwenye ndoto yangu. Nilikuwa kwenye huo mlango ambao ulikuwa
haujafungwa bado. Fursa ya mimi kuingia humo kwenye kushiriki sherehe ile
ilikuwa bado ipo. Nilichotakiwa tu kufanya ni kukubali mwito.
Papo hapo nilitambua kile
ninachotakiwa kufanya. Nilibaini kwamba Uislamu haukuwa ile kweli. Mungu
alikuwa ananivuta nitoke humo. Japokuwa mimi nilikuwa siko tayari, lakini
aliendelea kunivuta.
Ikawa ni kama naingia
kwenye majonzi na msiba. Nilikuwa nalia ninapoelekea shuleni. Siku moja
nikamwambia Mungu, “Mungu, nipe tu siku chache ili niomboleze. Nahitahi
kuomboleza, maana nina watu wengi ambao nitawapoteza.”
Niliporudi kwenye chumba
changu, nilifungua Quran na hakukuwa na kitu cha kunisaidia humo. Nilifungua
Biblia kwenye kitabu cha Mathayo, na kabla hata sijamaliza sura ya 5,
nikakutana na maneno: Heri wenye huzuni; maana maana hao watafarijika. Na
nikasoma Ayubu, na uchungu wote niliokuwa nao ukaisha. Lakini kwenye Quran
sikuwa na msaada wowote! Quran ilikuwa ikinipa tu maelezo ya mambo ya zamani,
lakini hakuna kitu cha kunisaida sasa. Hakuna kabisa! Lakini kila mara
nilipofungua Biblia, msaada ulikuwa pale.
Ninamwomba Mungu kitu halafu
namwuliza, “Nitajuaje kuwa nitapata hiki?” Kisha ninafungua 1 Yohana 5:14-15 na
inasema: Na huu ndio ujasiri tulio nao
kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama
tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja
tulizomwomba – maana tunaamini mioyoni mwetu kwamba Yesu ni Bwana. Niliamini
moyoni mwangu kwamba Kristo ni Bwana lakini sikuwa nimekiri.
Warumi 10 nayo inasema
kitu hichohicho. Inasema: Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni
Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Na
mimi nilikuwa sijafanya hivyo.
Kisha akili yangu
ilifunguka nilipokuwa nasoma kwenye Mathayo, inaposema: Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu,
nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Na pia inasema: Bali, kila
mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye
mbinguni.
Ilikuwa ni hapo ndipo
sikuweza kumkana Kristo tena! Sikuweza kumkana Mungu tena! Sikuendelea
kushikilia tena maisha yangu na mitazamo yangu ambayo nilikuwa nayo, si kwa
sababu niliamini, bali kwa vile tu nilizaliwa na kukua katika hiyo. Nilianza
kutambua kwamba ile haikuwa kweli na nikaanza kumkubali Kristo maishani mwangu.
Nilimwomba Roho Mtakatifu
anibadilishe maisha yangu. Na baada ya kuomba sala ile, ulimwengu wote ukawa
tofauti. Niliposema maneno yale, nilishtushwa kana kwamba nimepigwa shoti ya
umeme. Yalikuwa ni maneno tu, lakini yalikuwa ni maombi ambayo Mungu
aliyatimiza.
Na Roho Mtakatifu
alipoingia ndani yangu wakati huo, nikawa nimeshikwa kwa dakika zipatazo kumi
kama mtu aliyenaswa na umeme. Kwa dakika kumi nilikuwa siwezi hata kusogea! Na
pale nilipoweza kusogea, niliutazama ulimwengu ulionizunguka na ulikuwa mzuri
sana! Kulikuwa kumejaa matumaini; kulikuwa kumejaa maana! Nilitambua nini maana
ya maisha.
Si suala tu la kuishi kama
mtu mwema - ni kweli unatakiwa kufanya
hivyo. Lakini lengo la msingi kabisa la maisha yetu ni kumsifu na kumwabudu
Mungu mmoja wa kweli, aliyekuja kwenye ulimwengu huu, na kufa kwa ajili ya
dhambi zetu ili tuweze kuona jinsi anavyotujali; ili tuweze kumwabudu Yeye
kikamilifu, kwa furaha – kama ambavyo Paulo anasema kwenye Wafilipi: Furahini
wakati wote – maana Mungu yuko karibu.
Maisha yangu yalikuwa na
maana sasa, maana nilikuwa sasa naweza kwenda nje na kuhubiri. Haikuwa ni kukaa
tu na kusema, “Kila mtu anayefanya mema, atakwenda mbinguni.” Hapana! Sasa
kulikuwa na suala la kwamba, watu wanahitaji kujua Mungu ni nani; na nini
amefanya. Watu wanahitaji kujua nafasi yetu ni nini kwa habari ya uhusiano wetu
na Mungu; wanatakiwa kujua kuwa tunatakiwa kumwabudu Mungu mmoja wa kweli na
Mwanawe, Yesu Kristo ambaye alikuja kufa kwa ajili ya dhabi zetu.
Tunatakiwa kuwaambia watu
kuwa, ndiyo, Mungu ni mmoja. Hata hivyo, Yeye ni mmoja katika Utatu, na Utatu
katika mmoja. Iwe tunaweza kuelewa hilo au hatuwezi, ni jambo lililo nje ya
uwezo wetu. Si lazima tuelewe. Cha msingi ni kujua tu kuwa Yesu ni Mungu;
kwamba Mungu aliamua kuja duniani kama mtu.
Waislamu wanaona kuwa hilo
haliwezekani. Hakuna sababu ya hilo kutowezekana. Mungu anaweza kuamua kuja
duniani kama mtu. Nionyeshe kwenye Quran panaposema kwamba Mungu hawezi. Badala
yake, Quran inaonyesha kuwa Mungu anaweza kufanya chochote atakacho.
Siku ya mwisho, ya kiama
kama Quran inavyosema, tutahukumiwa. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbinguni, hata
Waislamu, kwa juhudi zake mwenyewe. Ni lazima iwe kwa neema ya Mungu. Hata
mtume wa Uislamu alisema watu waombe msamaha kwa Mungu mara nyingi kwa siku
maana hajui kama ataingia mbinguni au la. Ni kwa neema ya Mungu pekee.
Hiyo neema sasa, ambayo
hata Waislamu nao wanaitegemea siku ya mwisho ili kuingia mbinguni, ni neema
ileile ambayo Wakristo wanaitegemea. Tofauti tu ni kwamba, Wakristo wanaamini
kuwa neema hiyo tayari ilishatolewa kwenye msalaba miaka 2000 iliyopita Mungu
aliitoa hiyo neema kwa ajili yetu. Ni neema ileile, si nyingine tofauti, tunatakiwa
tu kutafuta kwa mioyo yetu yote. Naamini kwamba yeyote anayemwomba Mungu kwa
moyo ulio wazi aonyeshwe kweli, ataonyeshwa kweli!
…………………………………..
Mpendwa msomaji, umemsikia
Nabeel jinsi alivyokuwa na shauku ya kumjua Mungu wa kweli. Mungu si kiziwi. Yeye
hujibu haja na shauku za mioyo yetu za kutaka kumjua na kumpendeza. Kwa nini
usimwambie akuonyeshe njia ya kweli? Yesu ni njia, kweli, na uzima. Hakuna mtu
anayeweza kwenda mbinguni – hata kama ni Mkristo – kama hajamkaribisha Yesu
kuwa Bwana na Mwokozi maishani mwake na moyoni mwake.
Tafakari.
Jihoji.
Chunguza mambo.
Kweli imo ndani yako.
Hakika Mungu anatenda mema na kutuonyesha njia ya kweli bila kumkaribisha Yesu Kristo kuwa bwana na mokozi wa maisha yako kwamwe hauwezi kuona ufalme wa Mungu
ReplyDeleteNi kweli kabisa Stepha. Mwanadamu alifukuzwa Edeni kwa sababu ya dhambi. Hakuna mwanadamu asiye na dhambi. Hiyo ina maana kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuingia mbinguni kwa jitihada za kutunza sheria za Mungu. Hiyo maana yake pia ni kuwa, kuingia mbinguni ni LAZIMA iwe ni kwa njia nyingine. Yesu ndiye njia hiyo. Yesu ni NEEMA ya Mungu kwa mwanadamu. Kumwamini Yesu ndiyo njia PEKEE ya kuingia mbinguni. Ubarikiwe na Bwana.
Delete