Thursday, March 27, 2014

Unabii wa Kifo cha Yesu Kupitia Ibrahimu na Isaka




Kuzaliwa na kufa kwa Bwana Yesu si jambo lililoibuka tu. Hili lilikuwa ni jambo ambalo tangu wakati wa kosa la Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni lilitolewa unabii na Mungu mwenyewe. Mungu alimwambia shetani:“nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (mwanzo 3:15).

Hakuna mwanadamu anayeitwa uzao wa mwanamke. Uzao huwa unahesabiwa kwa manamume siku zote na duniani kote. Lakini ni Yesu peke yake ambaye hakuzaliwa na baba wa kibinadamu kama wanadamu wengine ndiyo maana anaitwa uzao wa mwanamke.

Wakati wa  Ibrahimu, Mungu alitoa tena unabii juu ya kufa, kufufuka na kulipa dhambi kwa Bwana Yesu. Unabii huu ulitolewa kupitia mtoto wa Ibrahimu, yaani Isaka. Je, ilikuwaje?


Maandiko yanatuambia kuwa: “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. ” (Mwa 22:1-2).

Sadaka ya kuteketezwa ni sadaka inayolipa uhai kwa ajili ya dhambi. Yaani, kulingana na torati, mtu alipotenda dhambi, basi alichukua mnyama aliye safi na kwenda naye kwa kuhani. Huko mnyama alichinjwa kisha aliteketezwa kwa moto. Maandiko yanasema kuwa: Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23).


Maana yake ni kuwa mtu akitenda dhambi yoyote, malipo yake ni mauti tu!

Lakini kwa sababu Mungu anampenda mwandamu, ndipo akasema: Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. (Walawi 17:11).

Kwa hiyo Ibrahimu alitakiwa kumtoa mwanawe wa pekee kama sadaka ya kuteketezwa, yaani ishara ya sadaka ya kulipia dhambi kama ambavyo Mungu naye angekuja kumtoa Mwanawe wa pekee, Yesu Kristo sadaka kwa ajili ya dhambi za ulimwengu.

Tunaendelea kusoma kuwa: “Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali.” (Mwa 22:3-4).

Tangu Ibrahimu alipokubali kumtoa mwanawe kwa Mungu, ni kama tayari Isaka alishakuwa mfu mbele zake. Alikuwa ameshakubali kuwa huyu si wangu tena; ndiyo maana akafunga safari kwa muda wa siku tatu kama ambavyo Yesu naye angekuja kufa kwa siku tatu.

Maandiko yanaendelea kusema kuwa: “Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na
kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili
pamoja." (Mwanzo 22:6).

Isaka alibeba kichwani mwake kuni ambazo ndizo zingeenda kumteketeka yeye mwenyewe. Huu ulikuwa ni unabii wa jinsi ambavyo Yesu naye angekuja kubeba msalaba ambao ndio ungenda kumaliza uhai wake.

Ndipo sasa walipofika kwenye mlima ambao Ibrahimu alielekezwa na Mungu: “Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.” (Mwa 22:10).

Lakini kwa kuwa huu ulikuwa tu ni mfano kwa ajili ya kutangaza unabii: “Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.” (Mwa 22:11-12).

Baada ya hapo, Mungu alitoa sadaka ya kuteketezwa Yeye mwenyewe kutoka mbinguni!! Imeandikwa: “Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.” (Mwa 22:13).

Huu ulikuwa ni unabii kwamba Mungu mwenyewe ndiye atakayetoa sadaka ya kuteketezwa iliyo kamilifu ya Kondoo mume. Ndiyo maana Yesu Kristo anaitwa Mwanakondoo wa Mungu (Yoh 1:29).

Hitimisho

Yesu ndiye sadaka kuu na ya pekee ya kuteketeza iondoayo dhambi za kila mwanadamu aliye tayari kuamini na kupokea kazi ya upendo aliyofanya Bwana msalabani.

Tangu zamani torati iliagiza kuwa NI LAZIMA kutoa sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya dhambi. Bila hivyo, hukumu ya Mungu ilikuwa juu ya kila mtenda dhambi.

Kama wewe hutoi sadaka kwa ajili ya dhambi, utasamahewa kwa sababu gani?

Ni damu SAFI PEKEE ndiyo inayofanya upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu; na damu hiyo ni ya sadaka ya kuteketezwa; na sadaka hiyo ni Yesu Kristo peke yake.


“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” (Matendo 4:12).

Njoo kwa Yesu sasa!

Tafakari
  
Hoji mambo

Chukua hatua!

2 comments: