Wednesday, June 10, 2015

Mtume Paulo Anavyowanyima Usingizi






Kati ya watu wanaowasumbua sana ndugu zetu Waislamu ni shujaa wa Bwana Yesu, Mtume Paulo. Na hii haikuanza kwa Waislamu pekee, bali kuanzia kwa washika torati waliokuwako wakati wake, yaani mafarisayo, wakuu wa makuhani, waandishi pamoja na Wayahudi wa kawaida waliofuata dini ya Kiyahudi.

Waislamu wanaendeleza tu ili roho ya upinzani dhidi ya Injili iokoayo ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Zifuatazo ni baadhi ya sababu ambazo Waislamu wanasema zinawafanya wamkatae Mtume Paulo, kama nilivyozitoa kwenye facebook kwenye post mojawapo ya ndugu mmoja wa Kiislamu.



Wanasema:
MOJA: Eti aliweka amri ya watu wasitahiriwe, ndio maana Wakristo wengi leo wana magovi


JIBU:
Tohara ni suala la afya ya kawaida wala halina uhusiano na kwenda mbinguni. Yaani, ukitaka kufanyiwa tohara, ni faida kwa mwili wako tu na wala sio kwa roho yako. Kinachoenda mbinguni ni roho na wala sio mwili. Mwili uwe umetahiriwa au haujatahiriwa, ukifa ni kuozea tu ardhini. Kwa hiyo, Mungu alilitumia hilo suala la tohara kama ishara ya mambo halisi ya rohoni, na sio ya mwilini:

(Kumb 10:16) Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu.


(Kumb 30:6) BWANA, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.


(Yer 4:4) Jitahirini kwa BWANA, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.


MBILI: Eti alikuwa gaidi wa kuwaua wanafunzi wa Yesu kisha akadai ni mtume wao ili azidi kuwaua kifkra

JIBU
Hii ni hoja kichekesho. Tangu lini mkawa na huruma na wanafunzi wa Yesu? Mnasemaje kuhusu makundi yenye itikadi kali ambayo yanaua Wakristo duniani hivi leo, yanavunja makanisa  na kuwalazimisha kufuata miungu yao? Je, nayo mnayalaani?

Paulo alikuwa muuaji KABLA ya kumjua Kristo kama ambavyo SISI SOTE nasi tulikuwa wenye dhambi kabla ya kumjua Kristo. Na Yesu anasema:

(Luk 5:31-32)  wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.

Yesu anawaita wenye dhambi ili Yeye ndiye awape mioyo mipya iliyojaa upendo, huruma na msaada kwa wanadamu wengine. Yeye hakuja kumtafuta Paulo asiye na dhambi, maana hakuna Paulo wa hivyo au mwanadamu yeyote wa hivyo.
Kama Paulo alikuwa mwuaji, wa kulalamika alitakiwa awe Kristo Yesu mwenyewe na wala sio wewe uliye na chuki na Paulo.


TATU: Eti ndiye aliyeleta ushoga duniani

JIBU
Huu ni uongo kutoka kwenye shimo la kuzimu. Paulo anasema:
Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, (1Kor 6:9)

Jipime mwenyewe kama usemayo ni mambo yanayoingia akilini au la. Unayejidanganya ni wewe mwenyewe wala si mtu mwingine.


NNE : Eti ndiye aliyesema pombe ni dawa ya magonjwa.

JIBU :
Huu ni uongo kutoka kwenye shimo la kuzimu. Alichosema Paulo ni kwamba unaweza kutumia mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo.


Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara. (1Ti 5:23) 

Wala hapa Paulo haongelei kunywa kimpumu, mbege, kangara, komoni na safari kama kiburudisho au kukata kiu. Anasema, ‘Mvinyo kidogo! Na mvinyo huo kidogo ni kwa kusudi maalum – kwa ajili ya magonjwa ya tumbo.

Maana yake ni kuwa, kama huumwi na unataka tu huo mvinyo, wewe ni mlevi tu wa pombe. Shauku yako si kupona ugonjwa bali kunywa pombe. Na zaidi ya hapo, kwa dunia ya leo dawa za magonjwa ya tumbo ziko tele.

Ni Paulo huyohuyo ambaye anasema  katika Waefeso 5 :18  --- Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho.


TANO : Eti ndiye aliyesema; Mungu haangalii mwili bali roho. Ndio maana leo Wakristo wanatembea nusu uchi tena mpaka wakienda makanisani.

JIBU
Kwanza, sio Paulo tu anayesisitiza juu ya roho kwanza mwili baadaye. Yesu mwenyewe anasema:

Ole wenu waandishi na mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.
Ewe farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.” (Mat 23:23-27).

Pili, sio kweli kwamba Paulo au Yesu au Biblia inakubaliana na watu kuwa uchi.
Paulo anasema : Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu. (1 Kor 8:13). Maana yake ni kuwa, jambo linalokwaza wengine na kuwatendesha dhambi, ukilitenda, hukumu iko juu yako ; hata kama jambo lenyewe lingekuwa ni jema kama kula chakula, sembuse kukaa au kutembea uchi!!

Je, hujui kuwa Paulo huyohuyo ndiye anayesema haya?

Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani (1 Tim 2:9)

Yesu anasema : Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! (Mathayo 18:7)


SITA : Eti ndiye aliyesema watu wasalimiane kwa kupigana busu tena akaliita ni takatifu.

JIBU
Mtu akiwa na chuki na wewe, chochote utakachofanya atatafuta neno linalobeza ufanyacho. Kwa hiyo, suala sio ubaya wa tendo bali ni chuki iliyo moyoni mwake.

Je, kwani hujui tofauti kati ya jambo takatifu na jambo lisilo takatifu? Nikikwambie, “Uwe unakunywa maji safi” ubaya wangu uko wapi? Huoni kuwa hapa ninakuambia, “Usinywe maji machafu”?

Paulo anasema watu wasalimiane kwa busu takatifu. Sasa kama busu ni takatifu, wewe mwenzetu unapata shida gani?


SABA: Eti ndiye pekee aliyesema kila chakula ni halali.

JIBU
Si Paulo pekee aliyesema hivyo. Hata Yesu alisema:

Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi. (Mat 15:15-20)

Kila watu hapa duniani wana utamaduni na vitu wanavyokula WAO. Wanaokula mbwa, acha wale. Wewe kama huwezi, usianze kuwahukumu. Wanaokula nyoka, acha wale; chura, konokono, nk. Kama utamaduni wao unawaruhusu kula vitu hivyo, acha wale. Hata wewe unayekula keki, kila kiingiacho tumboni, hakiendi rohoni bali mwisho wake ni chooni!


NANE : Eti  ndiye aliyeleta dini mseto ya ukristo duniani.

JIBU
Sisi tunamfuata Kristo Yesu kama ambavyo Paulo naye alimfuata Kristo Yesu. Je, wewe unamjua Paulo kuliko Petro ambaye aliishi naye kwenye nyakati zilezile ; alikutana naye uso kwa uso na aliyapima mafundisho yake?


Petro anasema :
Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe. Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. (2 Petro 3:15-17)



Kama mtu ataamua kukusikiliza wewe mpinzani wa Paulo aache kumsikiliza Mtume Petro hiyo ni juu yake na roho yake. Lakini sisi hatutaacha kusikiliza watumishi waaminifu wa Yesu Kristo tukae kusikiliza chuki zako wewe zisizo na msingi wa kweli ya Mungu.  


TISA : Eti ndiye pekee aliyedai Yesu ni Mungu Mkuu hali ya kuwa Yesu alikana hilo.

JIBU
Je, Paulo aliandika kitabu cha Isaya?----Maana kwa ajili yetu MTOTO amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, MUNGU MWENYE NGUVU, BABA WA MILELE, Mfalme wa amani. (Isaya 9:6)


Je, Paulo aliandika Injili ya Yohana? ---- Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. (Yoh 1:1) 



KUMI: Eti  ndiye pekee aliyekuja kuleta injili kwa mataifa wakati ni kwa ajili ya Waisraeli pekee.

JIBU
Tangu karne na karne huko nyuma, Mungu wa Israeli alishasema haya :

Msikie Yesu mwenyewe anachosema: ---- Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19)


Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. (Yohana 3:17).


Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. (Yohana 12:47).


Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. (Yohana 10:15-16).


Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. (Mat  24:14).


KUMI NA MOJA : Eti ndiye pekee aliyekuja kuitukana torati kwa kuiita ni laana.

JIBU
Torati sio laana, bali torati ni amri ambazo kwa kuwa wewe mwanadamu hauna uwezo wa kuzitimiza zote, unaishia kubeba laana. Sheria ikisema USIIBE maana yake kuiba ni kitendo kinacholeta laana kwa mwibaji sio lile neno lenyewe la sheria. Unapoiba, unayelaanika ni wewe kibaka na sio sheria iliyosema usiibe!!

Sasa msikie Paulo mwenyewe asemavyo juu ya torati:


Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa (Warumi 7:12-13).



Habari ya kusema Paulo kaita torati kuwa ni laana ni uongo, uzushi na upotoshaji wa maandiko.


KUMI NA MBILI : Eti Paulo ndiye aliyekuja kuitangua torati na kudai kuwa sasa torati isitumike tena. Kumbuka Yesu Alisema: Kwa maana, amin, nawaambia , Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie. (Mat 5:18)

 JIBU
Nikikwambia kosa hili hautasamehewa hata utakapolipa senti ya mwisho, je, maana yake kosa hilo ni la milele au lina mwisho?

Haihitaji ujuzi wowote mkubwa kubaini kuwa maana ya maneno hayo ni kuwa kosa hilo lina mwisho. Na mwisho wake ni pale utakapolipa kikamilifu kile unachodaiwa.

Hicho ndicho Yesu anachosema katika aya hiyo. Kila neno kwenye torati halitatanguka hata yote yatimie. Maana yake ni kuwa andiko litafikia mwisho pale tu litakapotimia. Kwa mfano, torati ilisema kuwa Yesu  atazaliwa.

Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. (Mathayo 2:6)

Sasa kama wewe hadi leo bado unashikilia ATATOKA, ATATOKA, ATATOKA kisa tu eti imeandikwa yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka basi ujue kuwa  umekula hasara. Andiko hilo LILISHATIMIA.

Lakini kwa mantiki ya wale ndugu zangu Waislamu wanaopindisha maandiko ya Biblia, ukiwaambia Yesu alishazaliwa, bila shaka kulingana na Mat 5:18 watasema, hapana. Yesu alisema neno HALITANGUKI, kwa hiyo bado liko vilevile.

…………………..

UTADANGANYWA HADI LINI?

UTAKUMBATIA UANGAMIVU HADI LINI?

Chuki humfanya mtu atiwe giza la moyo hata asiweze kuona mbele yake. Halafu huanza kuzusha uongo dhidi ya wengine, kisha akauamini yeye mwenyewe ili kujipa namna fulani ya amani ya uongo kwamba yuko sahihi.

………………………..

Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. (Mat 13:14) 

2 comments: