Sunday, January 13, 2013

Jambo la Ajabu Linaendelea Kwenye Ulimwengu wa Kiislamu
Makala haya yanaelezea mahojiano yaliyofanywa na mtangazaji wa CBN, Chris Mitchel, kuhusiana na kile kinachoendelea katika ulimwengu wa Kiislamu, ambao kwa karne nyingi umekuwa ukipinga kabisa Injili kuhubiriwa kwenye sehemu hiyo. Mahojiano haya yanaonyesha jinsi ambavyo Bwana Yesu mwenyewe anabomoa kuta na vizuizi kwa namna ambayo hata tawala za kiimla zinazotumia mahakama, hukumu za kifo na sheria kali kuzuia Injili kuwafikia watu, hawana tena la kufanya. Ni wakati wa Waislamu kujihoji na kumpokea Mwokozi wao ambaye aliwafia msalabani.

Bwana Yesu ndiye Muumba wa dunia hii na wanadamu wote – ikiwa ni pamoja na Waarabu ambao viongozi wao wamefanya kila waliloweza kuhakikisha kwamba Neno la uzima haliwafikii. Kwa karne nyingi walionekana kama wamefanikiwa. Lakini Neno la Bwana ni juu ya wanadamu wote. Bwana amesema katika Neno lake: Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. (Mathayo 24:14).

Na tena akasema: Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. (Mathayo 5:18).

Viongozi katika nchi za Kiislamu watafanya kila wawezalo ili kulinda imani yao na kuzuia watu kupokea uzima kutoka kwa Mwokozi wao, lakini Neno la Bwana ndilo litakaloshinda. Na hilo ndilo tunalolishuhudia hivi sasa.


******************

Chris Mitchell anasema, “Mwito kwa Waislamu ili waende kuswali unasikika sehemu kubwa ya ulimwengu ambako watu zaidi ya bilioni moja hujiita Waislamu. Vilevile, kote kwenye ulimwengu wa kiislamu, Waislamu wengi kutokea Gaza hadi London, wanaitikia mwito wa kujiunga na jihadi ili kuifanya dunia iwe ya kiislamu. Kwa muda wote wa miaka 1400 ya historia ya Uislamu, imekuwa ikikataa Injili ya Kikristo. Kwa karne nyingi, Wakristo wengi wamejaribu kuufikia ulimwengu wa kiislamu kwa Injili, lakini bila mafanikio makubwa. Hata hivyo, kulingana na ripoti toka kote mashariki ya kati na duniani kote, historia yao inabadilika.”

Nizar Shaheen ni mwendeshaji wa kipindi cha Kikristo cha Light for All Nations ambacho hutazamwa katika mashariki ya kati yote. Nizar anasema, “Naona watu wengi wanaozungumza Kiarabu wakimgeukia Kristo na kumpokea kama Bwana na Mwokozi wao.” [Unaweza kusoma historia ya Nizar kwa ufupi hapa.]

Father Zacharia Boutros kutoka Misri ambaye ni mmoja wa wainjilisti wakubwa kwa ulimwengu wa kiislamu naye anasema kuwa Waislamu wa marika yote na wa kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wanaendelea kumpokea Yesu Kristo. Anasema, “Kile kinachotokea siku hizi kwenye ulimwengu wa kiislamu hakijawahi kamwe kutokea huko nyuma.”

Anaendelea kusema kuwa wale wanaompokea Kristo, “Wadogo kwa wakubwa; wenye elimu na wasio na elimu; wanaume na wanawake; hata wale ambao ni wa imani kali.”

Mmoja wa Waislamu wa imani kali ambaye alimpokea Yesu ni Samir Akhmed Mohammed. Humu alisoma kwa miaka mingi ili kuja kuwa shekhe wa imani ya wahabi (yaani mojawapo ya imani za kiislamu ya msimamo mkali sana iliyoanzia Saudi Arabia). Huyu aliwachukia Wakristo na Kanisa. Lakini moyo wake ulibadilika pale aliposikia Injili.

Samir mwenyewe anasema, “Niliyatoa maisha yangu kwa Yesu Kristo. Yesu alinisamehe dhambi zangu. Alinipa uzima wa milele na amani. Na jambo la pili ni kuwa, nilikuwa nikiteseka sana katika maisha yangu ya kila siku. Lakini nilipata amani, nilipata furaha kwa sababu Yesu aliingia moyoni mwangu.”

Chris anasema, “Lakini Mohammed ni mmoja kati ya Waislamu wengi wanaokuja kwa Yesu. Heidi Baker wa Iris Ministries anashuhudia maelfu ya Waislamu wa Kiafrika wakimpokea Yesu na kubatizwa.”

Heidi mwenyewe naye anasema, “Huenda Afrika ni mahali pekee duniani ambako watu wanakuja kwa Yesu kwa haraka kiasi hiki. Watu wengi wanaota ndoto. Wanamwona Yesu akiwatokea. Huenda nusu ya viongozi wetu walikuwa ni viongozi; maimamu kwenye misikiti. Walikuwa ni viongozi kwenye misikiti na sasa ni wachungaji.”

Chris anaendelea kusema, “Jambo jingine muhimu la kiinjili linaloendelea kutokea miongoni mwa Waislamu linahusisha China na Yerusalemu. Makanisa ya nyumbani nchini China yana mpango wa kupeleka angalau wainjilisti 100,000 kwenye mataifa ambayo hasa ni ya Kiislamu. Kundi hili lenye nguvu la kimyakimya la Wainjilisti wanaotembea huku na kule wanaleta ujumbe wa Yesu Kristo ndani kabisa ya ulimwengu wa Kiislamu. Teknolojia kama vile T.V za satelaiti na intaneti nazo zinapenya kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Lakini mbali na teknolojia, wengi wanasema kuwa nguvu isiyo ya kibinadamu nayo iko kazini kwenye maisha ya Waislamu.”

Nizar Shaheen anasema, “Tunapokea barua nyingi sana za watu wanaosema kuwa wamepata ndoto na maono juu ya Bwana na hata miujiza. Na wanapokuja kutazama vipindi, wanasema, ‘ndio, niliota ndoto au niliona maono.’ Kisha wanampokea Yesu kama Bwana.”

Chris naye anaendelea kusema, “Lakini Waislamu wanaompokea Yesu wanakabiliana na mateso na kutengwa au hata kifo. Hata hivyo, licha ya hatari zilizopo, wengi wanaendelea kushikilia imani yao na pia wanawaleta wengi kwa Yesu Kristo.”

Samir anasema, “Yesu anawapenda watu wote. Yesu anawabadili watu wote. Na Yesu ndiye anayetupa upendo na amani. Mimi sikuwa hivi kabla. Lakini Yesu alibadili maisha yangu. Na wala mimi siogopi kumwongelea Yesu kwa sababu sifa ni zake.”

Chris anasema, “Baadhi ya watu wanaamini kuwa Kanisa linatakiwa litangaze Injili bila woga kwa Waislamu. Kupitia maombi na uinjilisti wengi wanaona fursa kubwa kwa ajili ya Injili.”

Nizar Shaheen anamalizia kusema, “Natarajia jambo hili hivi karibuni. Na pengine ndani ya miaka miwili au mitatu tutaenda kushuhudia mavuno makubwa kabisa katika historia.”

*************

Ndugu uliye Muislamu, huu si wakati wa kuendelea kung’ang’ania mambo hata kama moyo wako unakushuhudia kabisa kwamba huna amani na wala hujafanikiwa kuyafanya mambo ya kumpendeza Mungu. Usishindane na hali halisi. Usikubali kuendelea kuishi katika maisha ambayo, mdomoni unasema hivi lakini moyoni unateketea kwa sababu hata wewe mwenyewe unajua kuwa kile unachokisema kwa kinywa chako, moyo unakikataa.

Njoo kwa Yesu, Mwokozi wako, ili akuweke huru leo. Yesu ni Mungu aliye hai. Nimekuwa nikitoa changamoto hii – nataka niitoe tena na kwako pia.

Iwapo Yesu ni mwanadamu tu na si Mungu kama dini yako ilivyokufunza, basi ongea naye, maana anasikia. Mwambie hivi, “Bwana Yesu, kama wewe ndiwe Mungu wa kweli, basi nionyeshe ukweli uliko.”

Naamini hili si tatizo kwako. Maana kama Yesu ni mwanadamu, bila shaka hutapata tatizo lolote. Lakini kwa kuwa Yesu ni Mungu aliyekuumba na kukuokoa msalabani, nina uhakika kwamba atakujibu. 

Tafakari.

Hoji mambo.

Chukua hatua.

Waweza kuniandikia maoni yako pia kupitia: ijuekweli77@yahoo.co.uk
  

1 comment:

 1. Yaani we James ni mtu wa ajabu sana. Leo hii unakubali kwamba Yesu hakuja kuitengua taurati mpaka yote yatimie (mat 5:18). Sasa na huyu Paulo katika waef 2:15?
  Kwa kifupi nyinyi wakristo, hamjui mnachokiabudu, roho zenu zimezingirwa na tabaka la ushetani.
  Sasa kwa taarifa yako, kabla ya uislam, mashariki ya kati ilienea ukristo, kwa juhudi za bwana Paulo licha ya uyahudi ambayo ilikua ni dini ya walengwa.
  Baada ya kutia nanga uislam, watu walipoulewa wakaanza kujisalimisha wakiachana na ukristo. Mpaka leo hii, mashariki ya kati, ukristo karibu umepotea kabisa. Nguvu ya mungu sio mchezo, leo hii ukristo unashikilikiwa na kupewa nguvu na wazungu ambao hawaujui vizuri uislam.
  Kwa hiyo, kuwepo kwa watu wanaongea kiarabu wakristo sio kitu cha kushangaika. Wapo wakristo wenye asili ya kiarabu. Ndugu, tambua ya kwamba watu wote hawawezi kulingana akili, ndio maana kuna vichaa, mapunguani.nk.
  Sasa kama ulikua hujui leo hii nakujulisha ya kwamba bara la ulaya linakadiriwa baada ya miaka hamsini mbele, uislam utakua juu kuliko dini yeyote.
  Nenda nchini Ufaransa, Ujerumani, na uingereza ukajionee mwenyewe namna gani wazungu wanavyoachana na ukristo baada ya kusoma na kuelewa uislam.
  Leo hii card za krismasi na vipeperushi vya dini ya ukristo ni marufuku nchini uingereza na Spain.
  Wazungu wameanza kuelewa, ukweli upo wapi.
  Mwanasayansi wa uingereza juzi juzi tu hapa, kaachana na ukristo na kwa sababu, test zake zote alizofanya amekuta kwenye quran imebainisha.
  NDUGU, HAUNA HOJA HATA MOJA UNAYOSEMA KWA NINI HAUKUBARI UISLAM. TOA MAKOSA YA UISLAM ILI WATU TUKUELEWE TUWEZE KUKUFUATA. SIO UNAKAA TU NA KUSEMA TUMKUBARI YESU. SISI MBONA TUNAMKUBARI NA TUNATEKELEZA KILE ALICHOHUBIRI. NYINYI WALA HAMTAKI KABISA KUMSIKILIZA, BADALA YAKE MNASIKILIZA MANENO YA KISHETANI YA PAULO.
  YESU NYIE HAWAUSU!!!
  INJILI YA YESU HAKUNA! KUNA injili kama ilivyoandikwa yaani sio yenyewe. Ubabaishaji kibao! Hakuna hata neno moja lenye pumzi ya mungu.

  ReplyDelete