Thursday, May 16, 2013

Injili ya Yesu na Muujiza wa Yesu Vyamfanya Nadereh Aachane na Uislamu





Nadereh ni mwanamke aliyekuwa Mwislamu ambaye aliishi kulingana na sheria na taratibu za dini ya Kiislamu. Lakini katika maisha yake ya kumtafuta Mungu, alikutana na vikwazo au upungufu kadhaa. Hatimaye, alijikuta akibadili mwelekeo wake na kupokea wokovu wa Yesu Kristo. Je, ni nini kilitokea? Ni kwa nini hajutii uamuzi wake huo? Ungana naye ili uweze kujifunza jinsi Mungu anavyokupenda na kile alichokuandalia kwa ajili ya maisha haya na yale yajayo.

******************

Nilikuwa Mwislamu na nilimwamini Allah. Allah kwangu alikuwa Mungu na niliamini; lakini Mungu ambaye alikuwa hafanyi chochote kwangu. Hakuwa maishani mwangu. Sikuwa na uhusiano na Mungu huyo.

Mungu huyu alikuwa kwenye ‘kabati’ ndani. Kila nilipokuwa nina hitaji fulani, ninamwambia halafu nasahau. Kwa hiyo, sikuwa na uhusiano naye ila tu ninapokuwa nina hitaji, ninamwomba. Hivyo, huo ndio uliokuwa uhusiano wangu na Allah.

Kwa kweli, nilikuwa mtupu ndani; hakuna amani, hakuna furaha kabisa! Japokuwa nililelewa kwenye familia nzuri na yenye upendo, lakini ndani yangu nilikuwa mtupu, mwenye huzuni, mkavu kabisa!

Kilichonifanya nianze kumjua Kristo ni mwujiza ulionitokea maishani mwangu. Mimba ya mwanangu wa kwanza iliharibika. Kisha baadaye nilipata mtoto wa kwanza. Nilipata ujauzito tena na baada ya miezi mitano, nilianza kutokwa damu, na nikampoteza tena mtoto yule hospitalini.

Baada ya hapo, nilijawa na huzuni sana. Nilimkarikia sana Mungu. Sikutaka kusikia chochote kuhusu Mungu; kuhusu Allah, maana nilikuwa na huzuni kubwa sana!

Kwa hiyo, nilikuwa nikilia, na hata nikaamua kujiua. Wakati huo sikutaka kuongea na mume wangu au hata na mwanangu. Nilikuwa najifungia ndani na kulia sana kwa huzuni.

Miezi michache baadaye, mume wangu, kwa kuwa aliona nilivyo na huzuni, alipendekeza kwamba tusafiri na aninunulie zawadi ili kunifanya niwe na furaha. Lakini sikupata furaha.

Baada ya muda, nilipata ujauzito tena. Baadaye nikaanza kutokwa damu tena. Wakati huo nilikutana na mama mmoja Mkristo ambaye anamwamini Yesu. Alinihubiria Injili na akaniambia, “Kwa nini usimwambie Mungu akuambie kweli?”
Nikasema, “Una maana gani?”
Akasema, “Wewe mwombe tu akuonyeshe ukweli.”

Kusema kweli, nilishangazwa sana na pendekezo hilo aliloniambia. Nakumbuka usiku ule nilipiga magoti pembeni mwa kitanda changu na kumlilia Mungu. Nikamwambia, “Nionyeshe kweli. Wewe ni nani? Wewe ndiwe uliyeniumba. Unaweza kunionyesha kweli. Sitaki kufuata tu dini yoyote. Maana hakuna anayeweza kubadili moyo wangu. Kama wewe ni wa kweli, basi nionyeshe ile kweli.”

Na nakumbuka nililala na niliamka usiku na damu zilizokuwa zikinitoka ziliacha kutoka! Na siku iliyofuata nilienda kwa daktari. Alisema, “Kila kitu kiko sawa; mtoto yuko vizuri kabisa. Ni muujiza! Sijui ni kitu gani kimekutokea!”

Nikasema, oh, oh. Kuna jambo limetokea kwangu. Ilikuwa ni muujiza kwangu. Kwa mwingine inaweza isiwe ni muujiza lakini kwangu ulikuwa ni muujiza maana nilimwomba Mungu ajidhihirishe kwangu. Kwa hiyo, nilimpigia simu yule mama Mkristo. Ilikuwa ni jumapili. Nikamwambia, imani yako ni ipi? Napenda kuisikia. Nilienda nyumbani kwake. Alianza kunieleza juu ya Injili ya Yesu Kristo; kwamba alikuwa ni Mungu katika mwili; ambaye alikuja na kufa kwa ajili yangu; kwa ajili ya dhambi zangu na kila kitu. Alilipa gharama kwa ajili yangu.

Niliguswa sana. Nikasema, “Sina Mungu wa namna hiyo. Mungu ninayemfahamu ni wa tofauti sana. Ninapenda nimjue Mungu huyo aliyekufa kwa ajili yangu. Napenda aje moyoni mwangu. Je, nifanye nini? Niende tu kanisani? Au nijue Biblia yote?”

Akasema, “Hapana. Mkaribishe tu Yesu moyoni mwako nawe utakuwa huru, utaokoka na utaponywa.”

Nilishangaa sana na nilijawa na furaha sana. Nikasema, “Aha! Nifanye nini sasa?”

Akasema, “Wewe omba pamoja na mimi sala hii.”

Tuliomba sala fupi tu. Nilimkaribisha Yesu moyoni mwangu. Na mara tu nilipomaliza kuomba, nilijisikia furaha kubwa sana; amani kubwa sana ambayo sikuwa nimewahi kuwa nayo! Na tangu wakati ule, maisha yangu yalibadilika kabisa.

Nimekuwa Mkristo kwa miaka 18 sasa. Yesu amebadili ufahamu wangu na kila kitu ndani yangu – uhusiano na mume wangu, uhusiano na wanangu, uhusiano na marafiki zangu au hata na watu wengine. Kila kitu ambacho nilikuwa napambana nacho, Yesu amebadili. Ni kwa sababu Yeye ni Mungu na amekuja kwenye maisha yangu na kubadili kabisa moyo wangu.

Nilikuwa na kila kitu maishani mwangu – mume mzuri, mtoto, wazazi wazuri, lakini ndani yangu sikuwa na furaha! Na mara nilipomkaribisha Yesu moyoni, nilipata furaha kubwa sana.

Na nilipofika nyumbani, nilikuwa naogopa kumweleza mume wangu juu ya jambo lile. Niliomba kwa wiki mbili ili niweze kumweleza. Nilipokuja kumweleza mume wangu, nilikuwa ni mtu niliyebadilika sana kiasi kwamba alifurahi sana. Hata yeye alikiri kuwa ndani ya zile wiki mbili aliona mabadiliko makubwa.

Kabla ya hapo sikuwa na furaha kabisa. Nilikuwa na kila kitu lakini sikuwa na furaha. Na binti yangu nilimzaa salama, sikutokwa na damu tena. Na binti zangu wanampenda Kristo.

Siku moja nilikwenda kwenye nyumba ya rafiki yangu na binti yao alikuwa na kansa. Ana miaka 22 na wao ni Waislamu. Nikawaeleza kuhusiana na uponyaji na amani na furaha na kweli ambayo wanaweza kuzionja.

Nilimweleza kuwa, Yesu alisema, kama ukitaka kuujua mti, basi angalia matunda yake. Na nikasema, wakati nilipokuwa kwa Allah, sikuwa na matunda yoyote. Sikuwa na furaha, hakuna amani, hakuna upendo, hakuna kitu! Nilikuwa mtupu! Na nikawaambia kuwa wanaweza kuona hata ndani yao ni hivyo hivyo – maana hata wao hawana kitu. Huo ndio ukweli.

Lakini sasa naweza kuwaeleza kuwa, kwa kumkaribisha Yesu mioyoni; kwa kuikubali kweli, ile kweli inakuweka huru. Kweli inakuponya na kukupa furaha – yote hayo yanaletwa na kweli maishani mwako. Wewe pokea tu.

Nikasema, mimi nilikubali na maisha yangu yakabadilika. Kwa nini na ninyi msipokee? Mkaribishe tu Yesu moyoni na uone jinsi ilivyo rahisi. Huwa nawashirikisha watu Injili. Na mara nyingi huwa naongea na Waislamu; na wengi wao unapowaeleza, kile wanachowaza ni kuwa labda unataka kuwaambia wabadili dini yao.

Mara zote huwa nasema, mimi siongelei kuhusu dini. Ninaongea kuhusiana na wokovu. Mungu anazungumza kuhusiana na wokovu. Si kuhusiana na dini. Maana Muhammad au mtu mwingine yeyote wanacholeta ni dini. Na Mungu hajaongea kuhusiana na dini. Yesu hakuwahi kuongea kuhusu dini. Tunaongea kuhusiana na wokovu. Kweli ndiyo inayokuweka huru.

**********************

Ndugu msomaji wa blog hii, umemsikia na kumsoma Nadereh. Unawaza nini juu ya maisha yako? Unampenda Mungu au unapenda dini?

Tafakari

Hoji mambo

Chukua hatua.

No comments:

Post a Comment