Friday, March 1, 2013

Majibu Yangu Kwa Ibra Kuhusu Wana wa Ibrahimu - Isaka na Ishmaeli



 Ishmaeli na mama yake (Hajiri) 
wanafukuzwa nyumbani kwa Ibrahimu

Katika makala yangu yenye kichwa kisemacho: Je, Muhammad Ametabiriwa Kwenye Biblia? – Sehemu ya II, ndugu yangu Ibra amenipa changamoto kadha wa kadha ambazo naziheshimu na nimezitafakari vizuri. Unaweza kuzisoma kwa ukamilifu wake kwenye sehemu ya ‘comments’ mwisho kabisa wa makala yaliyo hapa.


Mjadala wangu na Ibra unatokana na hoja yake kwamba Muhammad alitumwa kwa watu wote lakini, Ibra anasema, Yesu alitumwa kwa ajili ya wana wa Israeli tu, kitu ambacho mimi nimemweleza kuwa si kweli kwamba Yesu alitumwa kwa Israeli tu. Hoja zake na majibu yangu viko kwenye sehemu ya hiyohiyo ya maoni (comments) mwishoni mwa makala yaliyo hapa.


Lakini nimeona ni vema nitoe majibu ya changamoto hizo kama makala kamili kwa ajili ya faida ya wengi, maana maswali haya yanajirudiarudia tena na tena kutoka kwa ndugu zangu Waislamu walio wengi.


Ibra umeanza kwa kunionya kwamba niache tabia ya kuwa nabii wa uongo maana Mungu hapendi na ni mkali sana juu ya upotoshaji wa Neno lake. Ninashukuru kwa hilo rafiki yangu Ibra. Ni kweli kabisa Neno la Mungu si la kuchezea hata kidogo. Ukilipindisha utakutana na mapigo makubwa mno maana si tu kwamba unasema uongo, bali pia unasababisha watu wa Mungu waishie jehanamu ya milele kutokana na uongo huo. Mungu hawezi kuwa radhi na tabia hiyo. Kwa hiyo, Ibra, ninakubali maonyo yako; lakini hadi sasa, ninapoangalia, sijadanganya mahali kokote katika yale niliyokwisha kuyasema. Yote ni mambo ambayo yana ushahidi wa kimaandiko juu ya ukweli wake.


Vilevile, Ibra umesema kuwa unashindwa kuelewa ni kwa nini mimi ni mgumu wa kuelewa maandiko, na pia ninayatafsiri kama ninavyotaka mimi. Ukaniuliza, “Kwa nini lakini unapingana na Mungu? Maandiko yako wazi kabisa we unamn'gan'gania Isaka kivipi? Mungu atafanya agano lake imara na la milele kwa Isaka kwa ajili ya uzao wake. Sasa hapo wewe unahusika kivipi hapo? We ni uzao wa Isaka?


Majibu yangu:
Najua Ibra, hapa unalenga kwenye maneno uzao wake. Unachomaanisha ni kwamba, mbona mimi ni Mswahili wa mbali huku? Je, ninahusika vipi na andiko hili wakati mimi si Myahudi?


Ibra, napenda nikujulishe wewe pamoja na wengine kuwa mimi ni uzao wa Isaka kabisa! Tena si mimi tu, bali hata wewe ni lazima uwe uzao wa Isaka, kama una nia ya kuingia mbinguni. Haya si maneno au mawazo yangu, bali ni maagizo ya Muumba wetu.


Kila mara nimekuwa nikisisitiza jambo hili ambalo namwomba Roho Mtakatifu aweze kuwafunulia ndugu zangu Waislamu ili muweze kutoka kwenye kifungo kilichowafunga.


Wapendwa wangu, mnajua kabisa kwamba Mungu ni roho, mbingu ni mahali pa kiroho, na hivyo hata ujumbe wa Mungu ni wa kiroho. Lakini mara zote ninyi mnaishia kuona mambo kimwili. Hapo ndipo mnakopigwa chenga kubwa sana inayowagharimu uzima wa milele.


Maandiko yanasema hivi: Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.  (Yohana 3:6). Ukiishia kuwaza kwamba Mungu alipotumia neno ‘uzao’ alimaanisha kuzaliwa kimwili, basi ni lazima utakwama tu. Mambo ya mwili ni ya hapa duniani. Lakini mambo ya Mungu si ya hapa duniani. Ni mambo ya mbinguni ambayo ni ya kiroho.


Sasa mimi ni wa uzao wa Isaka kwa vipi? Hebu soma andiko lifuatalo:

Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili;

bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu. (Warumi 2:28-29).


Hii ina maana kuwa kuna Wayahudi wa aina mbili: wale wa nje na wale wa ndani. Myahudi wa nje ni yule anayezaliwa kimwili; ni damu kabisa ya Isaka. Lakini Myahudi wa ndani ni yule wa rohoni. Anayezaliwa na Roho Mtakatifu kupitia Neno la Kristo, yaani kupitia kuiamini Injili.


Hilo ndilo linalonifanya mimi, wewe na mwingine kuwa uzao wa Isaka. Na ndiyo maana basi, Mungu akamwambia Ibrahimu kwamba:


Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? (Mwanzo 18:18).


nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. (Mwanzo 12:2-3).


na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. (Mwanzo 22:18).


Hebu niambie, Ibra, mataifa yote yanaingiaje ndani ya baraka za Ibrahimu wakati (kwa mtazamo wako) hajawazaa yeye?


Na ni kwa vipi basi Mungu alimwambia Ibrahimu kwamba: Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi (Mwanzo 17:4)?i


Ubaba wake unakujaje? Kwani alituzaa sote kimwili kama unavyojaribu kutafsiti neno ‘uzao’? Bila shaka hapana. Ibrahimu ni baba yetu kwa njia nyingine tofauti na uzazi wa kimwili. Ni watoto wake kwa njia ya kiroho. Na kama ni watoto wake, basi sisi ni uzao wake; na ni uzao wa Isaka pia.


Na kama ni uzao wake, basi tunarithi baraka zake alizoahidiwa na Mungu. Na huo uzao wa Ibrahimu na Isaka, ndio ambao Yesu Kristo aliujia. Maana Yesu anasema: Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.
(Mathayo 15:24).


Kila anayekataa kuingia kwenye uzao wa Isaka, hana nafasi katika mbingu za Mungu aliyeumba mbingu na nchi. Hana! Hana! Hana!

*****************

Ibra amenukuu Biblia katika Mwanzo 16:12 inayosema:

Mkono wake (yaani wa Ishmaeli) utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote.


Kisha Ibra akaniambia, “Tafsiri basi na aya hiyo. Mungu anamaanisha nini hapo?”


Ibra, nadhani andiko hili liko wazi kabisa. Na pia linaonyesha jinsi Biblia ilivyo kweli ni Neno la Mungu aliye hai. Hebu fikiria mwenyewe, andiko hili limeandikwa takriban miaka 1400 kabla ya Kristo.


Biblia inapoongelea Ishmaeli hapa, inaongelea uzao wake. Na wewe unajua uzao wa Ishameli ni nani – ni Waarabu kimsingi. Na unajua nini kinachoendelea leo.


Muhammad alitokea miaka 600 baada ya Kristo. Hiyo kusema, alikuja miaka 2000 baada ya andiko hili. Na kuanzia pale ndipo uhalisia na utimilifu wa andiko hili ulipokuwa wazi.


Je, si kweli kwamba uzao wa Ishmaeli (Waarabu/Waislamu) wako kinyume na dunia yote kiasi kwamba wako tayari hata kuua kwa jina la dini na la Mungu? Je, si kweli kwamba uzao huu unamwona kila asiyekubaliana na wao kuwa ni kafiri na adui? Na je, si kweli kuwa, kutokana na kwamba kile wanachojaribu kufundisha hakifundishiki na hakikubaliani hata na asili ya mwanadamu, matokeo yake inabidi wakilazimishe kwa nguvu? Na je, si kweli kwamba dunia nayo haikubaliani na hilo? Unaona sasa, Ibra, jinsi Biblia ilivyo Neno hai na la kweli la Mungu?


*****************

Ibra anasema:
Ndugu yangu maagano ya Mungu (sio ya shetani kama ulivyodai) yapo mawili: la Isaka kwa ajili ya uzao wake na Ishmaeli kwa ajili ya watu wote ambalo, amerithi kutoka kwa baba.


Anachodai Ibra ni kuwa, Isaka (na hatimaye Yesu, walikuwa ni kwa ajili ya Israeli tu. Lakini Ishmaeli (na hatimaye Muhammad), walikuwa ni kwa ajili ya ulimwengu wote. Kwa hiyo, Ibra ametoa nukuu kadhaa za Biblia ili kuthibitisha hoja yake kama ifuatavyo:


Mwanzo 15:4. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.


Ishmaeli ni mtoto wa kiuno na Isaka ni mtoto wa ahadi. Kwa hiyo mrithi atatoka katika viuno.


Jibu langu:
Inaonekana rafiki yangu Ibra, wewe unafikiri kuwa andiko hili linamhusu Ishmaeli. Si hivyo. Hili linamhusu Isaka.
Lakini kabla hatujaangalia maana halisi ya andiko hili, hebu tuangalie kwanza muktadha uliozaa andiko lenyewe. Imeandikwa kwamba:

Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.

Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski?

Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu.

Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. (Mwanzo 15:1-4).


Hapa Ibrahimu alikuwa anamwambia Mungu kuwa, kwa kuwa hajapata mtoto na ameshakuwa mzee, basi wale waliozaliwa nyumbani kwake, (yaani wasio damu yake – watoto wa watumishi na wajakazi wake, maana alikuwa nao wengi), hao ndio angelazimika kuwaachia urithi wake.


Ndipo Mungu akampa majibu hayo hapo juu.


Lakini najua kuwa Ibra utasema, “Sasa aliyetoka kwenye viuno vya Ibrahimu na anayetakiwa kuwa mrithi wa baraka na kila kitu si ni Ishmaeli?”


Hata Ibrahimu naye aliwaza kwamba ni hivyo. Baada ya Ishmaeli kuzaliwa, na kabla Isaka hajazaliwa, imeandikwa kwamba: ''Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.


Lakini Mungu akasema: Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. (Mwanzo 17:18-20).

 
Kwa hiyo, agano la milele kati ya Mungu na Ibrahimu halikumhusisha Ishmaeli hata kidogo japokuwa alikuwa naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa maana hiyo, halimhusu Muhammad. Agano linatoka kwa Mungu – Ibrahimu – Isaka – Yakobo – Yesu. Si Ishmaeli wala Muhammad!

 
Maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa mwanadamu yeyote akitaka kuingia kwenye agano la kulindwa, kubarikiwa, kuponywa na kupata uzima wa milele, ni lazima apitie upande wa Isaka na kamwe si upande wa Ishmaeli.


*******************

 
Ibra ameniuliza:
Sasa basi, Ishmaeli anarithi nini kutoka kwa baba?


Jibu langu:
Kulingana na maandiko, Ishmaeli hana urithi wowote kutoka kwa Ibrahimu. Imeandikwa kwamba: 

Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. (Wagalatia 4:30). Ishmaeli alikuwa mwana wa mjakazi, yaani Hajiri; na Isaka alikuwa mwana wa mwungwana, yaani Sara.

Ibra umenukuu maandiko yafuatayo:

Mwanzo 17:2-4. Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana.
Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema,
Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi.
 
Mwanzo 12:2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka.

Mwanzo 17:20. Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu.

Wagalatia 4:21-25. Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria?

Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana.

Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.

Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.
 
Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.

Ibra anamalizia kwa kuniuliza, “Hapo napo inahitaji chuo?”

Jibu langu:
Asante sana Ibra kwa changamoto hizi. Ni wazi kwamba maandiko yote haya yanazidi kuonyesha jambo lilelile kwamba baraka na urithi wa kiroho unaweza kutufikia tu kupitia Isaka na si kupitia Ishmaeli.


Kwa upande wa Ishmaeli, alichopata tu kutoka kwa Mungu ni kuwa taifa kubwa. Na hili liko wazi hata sasa. Waarabu na hatimaye Waislamu ni jeshi kubwa kabisa. Lakini hapo ndio mwisho wa ahadi na baraka za Mungu.


Lakini kwa kuwa shina la yote ni Ibrahimu, tumeona katika Wagalatia 4:30 hapo juu kuwa, ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu hakupewa mwana wa mjakazi. Badala yake, huyo alifukuzwa. Kwa hiyo, hana baraka hasa ile ambayo Mungu alisema kuwa hata mataifa yote watajibarikia.


Lakini nashangaa Ibra huogopi kunukuu Wagalatia 4:21-25!


Hebu itazame nukuu hiyo tena kwa makini:
Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria? 


Je, Ibra, andiko hili linawasifu au linawakemea wanaotaka kuwa chini ya sheria? Ni wazi kuwa linawakemea. Mwandishi anawashangaa watu hawa ambao wanaacha kukumbatia uhuru badala yake wanakimbilia kujiweka chini ya kongwa la sheria.


Sasa, ni nani anayetaka kuwa chini ya sheria leo? Je, si wewe Ibra na Waislamu wenzako? Mnataka kuwa  chini ya sheria ambazo mnajua fika kuwa ninyi wenyewe hamjawahi kuzitimiza hata siku moja. Ndipo sasa anawauliza, kwa nini mnataka kuwa chini ya utumwa badala ya kuwa huru? Hebu tuendelee kulisoma andiko hilo:

Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana. Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.

Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.
 
Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.


Ishmaeli na Isaka ni wana wa baba mmoja. Lakini pia kati wao Mungu ametupatia mfano. Ishmaeli alizaliwa kimwili. Yaani ni mtoto tu kama watoto wengine.


Lakini Isaka alitokana na ahadi ya Mungu mwenyewe. Maana mama yake (Sara) alikuwa tasa. Hivyo, kibinadamu, au kimwili, hakuwa kabisa na uwezo wa kuzaa. Kuzaliwa kwake ilikuwa tu ni kwa mwujiza wa Mungu, kwa sababu Mungu alishatoa ahadi kwa Ibrahimu.


Ni kwa vipi basi mambo haya ni mfano? Kwenye Mlima Sinai ndiko Musa alikopokea torati. Na Yerusalemu ndiko Bwana Yesu alikoleta Injili.


Ishmaeli ni ishara ya utumwa na kukataliwa, licha ya kwamba kwa kawaida mtoto wa kwanza ndiye aliyekuwa na haki ya kuwa mrithi wa baba yake. Vivyo hivyo, torati ni sheria ambazo kazi yake pekee ni kumwonyesha mwanadamu jinsi ambavyo amepungukiwa mbele za Mungu. Na mwanadamu yeyote anayejidanganya kuwa anaweza kutimiza sheria yote ya Mungu, huyo yuko chini ya utumwa na laana na kukataliwa – maana hakuna mwanadamu anayeweza kutimiza sheria yote ya Mungu kwa ukamilifu wote – hata wewe Ibra ni shahidi katika maisha yako mwenyewe.


Isaka ni ishara ya uhuru na kukubaliwa. Vivyo hivyo, Injili ya Yesu Kristo ni habari njema inayotangaza kusamehewa dhambi na kukubaliwa na Mungu kwa sababu yuko mmoja ambaye alibeba dhambi zetu, ili kwa kumwamini tu, sisi, japo hatustahili mbingu kutokana na dhambi zetu, tuweze kusamehewa bure.


Na kwa msingi huu, yeyote anayekumbatia Quran, (ambayo asili yake ni Ishmaeli au Uarabuni), anakumbatia utumwa na kukataliwa na Mungu. Lakini yule anayekubali Biblia (ambayo asili yake ni Isaka au Yerusalemu), anakumbatia uhuru na kukubaliwa na Mungu.

Tafakari.
Jihoji.
Jipime.
Chukua hatua.


****************

Mwisho ndugu yangu Ibra na Waislamu wengine, naomba majibu ya maswali yaliyoko hapa.

6 comments:

  1. Mr.James
    Mimi sijui wewe umekwama wapi. Nimekuonya mara ya kwanza juu ya kutaka kwako kuyapindisha aya za mungu.
    MITHALI 30:5-6 ''Kila neno la Mungu limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio.
    6 Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.''

    Mr.James pamoja na biblia kuwa na utata mwingi, swala la Ibrahim linaeleweka vizuri. Hapa ndipo penye msingi wa imani.
    Ni kweli kabisa kwamba, Ishmaeli na mama yake walifukuzwa nyumbani kwa Ibrahim. Aliyowafukuza ni Sara, sio Ibrahim, baada ya yeye(Sara) kupata mtoto ambaye ni Isaka, ili mali za nyumbani arithi Isaka peke yake (Mwanzo 21: 9 Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.
    10 Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.
    11 Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. )
    Mungu kwa kuepusha shari, kwa mambo kama haya ya kibinadamu, akamwambia Ibrahim akubaliane na matakwa ya Sara.
    14 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.
    Sasa je! baada ya kutengwa na Sara, mungu na Ibrahim waliwatenga (Hajiri na mtoto wake)?
    Neno la mungu linasema hapana, hawajatengwa.
    Mwanzo 21:13 Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.
    Mwanzo 21:15 Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.
    16 Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.
    17 Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.
    18 Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.
    19 Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.
    20 Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.
    Maandiko ya wazi kabisa, mungu akawa pamoja na huyo kijana.

    19 Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.
    Kwa maana hiyo Ibrahim yupo beer-sheba aliko Ishmaeli.

    KWA HIYO ISHMAELI NA MAMA YAKE WAMEFUKUZWA NA SARA NYUMBANI KWA IBRAHIM KWA SHINIKIZO LA SARA. SIO MUNGU WALA IBRAHIM. AHADI YA MUNGU IPO PALEPALE YA KUMFANYA ISHMAELI KUWA TAIFA KUU KAMA BABA YAKE IBRAHIM. MTOTO HUYU, ANARITHI BARAKA ZA BABA YAKE.

    Mwanzo 18:18 AKIWA IBRAHIM ATAKUWA TAIFA KUU, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa?

    Mwanzo 17:20 Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, NAMI NITANFANYA AWE TAIFA KUU.

    Mwanzo 16:12 Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote.
    KWA AYA HII, YEYOTE YULE ANAEJIJUWA KWAMBA NI MTU INAMHUSU, NDUGU( ISAKA NA WENGINE), INAWAHUSU PIA. NDIO MAANA YA TAIFA KUU. HAPA NDIO CENTER WA IMANI ZOTE, MWISHO WA IMANI. HAPA HACHAGULIWI MTU, WOTE NI SAWA KATIKA KUMWABUDU MUNGU.


    ReplyDelete
    Replies
    1. Ndugu Ibra, Mungu akubariki kwa jitihada zako na shauku yako ya kutaka kuhakikisha kwamba KWELI ya Mungu inapewa kipaumbele. Kwa kuwa hoja zako za kumtetea Ishmaeli zinatokana na Biblia (na si Quran), basi ni vizuri, kama ulivyoanza kuiamini Biblia katika aya hizi, uamini Biblia yote.
      Nasema hivi kwa sababu, anayezungumza katika kitabu cha Mwanzo ndiye huyohuyo anayezungumza katika vitabu vyote – hadi kitabu cha Ufunuo. Maana yake ni kuwa, tunapoongelea aya YOYOTE katika Biblia, NI LAZIMA kuitazama katika muktadha wa Biblia nzima. Hadi hapa nimeshakupatia ushahidi unaoonyesha kuwa Ishmaeli hayupo kwenye urithi wa baraka za Ibrahimu ambazo Mungu alimuahidi Ibrahimu.
      Safari hii umesema kuwa aliyemfukuza Hajiri hakuwa Ibrahimu wala Mungu, bali ni Sara. Pia unasema kwamba, “Mungu kwa kuepusha shari, kwa mambo kama haya ya kibinadamu, akamwambia Ibrahim akubaliane na matakwa ya Sara.”
      Ibra, kusema kwamba Mungu alikuwa anaepusha shari, hayo ni maneno yako mwenyewe wala hakuna sehemu yoyote kwenye Biblia ambapo Mungu anasema hivyo. Lakini badala yake nilikuonyesha sababu ya kufukuzwa kwa Hajiri. Ngoja niirudie tena hapa. Ibrahimu alitaka Ishmaeli arithi baraka ambazo Mungu alimuahidi. Tunasoma kwamba: ''Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.”
      Lakini ni lipi lilikuwa jibu la Mungu? Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. (Mwanzo 17:18-20).
      Nirudie kusema tena kwamba, Ishmaeli hayupo kwenye ramani ya kiroho ya ukombozi wa mwanadamu. Si kwamba alikuwa mtu mbaya, hapana. Ila tu lile agano LA MILELE (yaani linalovuka maisha haya ya duniani), linapatikana upande wa Isaka tu.
      …………………………..
      Jambo jingine linalothibitisha kwamba Ishmaeli hana nafasi kwenye wokovu wa mwanadamu ni namna Mungu anavyoitwa kwenye Biblia yote. Utakuta anaitwa Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Hakuna hata nusu mstari, achilia mbali aya nzima, inayosema kuwa Mungu ni Mungu wa Ibrahimu na Ishmaeli. Tazama mifano ifuatayo:
      Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, MUNGU WA IBRAHIMU baba yako, na MUNGU WA ISAKA; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. …, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. (Mwanzo 28:13-14)

      Hapa Mungu anasema na Yakobo. Na unaona kuwa Mungu anamwambia, “katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa.” Ni ahadi ileile ya Ibrahimu, babu yake.

      ………………………………………
      Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, MUNGU WA IBRAHIMU, MUNGU WA ISAKA, NA MUNGU WA YAKOBO. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. (Mwanzo 3:6)

      ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba Bwana, MUNGU WA IBRAHIMU, MUNGU WA ISAKA, MUNGU WA YAKOBO, amekutokea (Mwanzo 4:5)

      Ee Bwana, MUNGU WA IBRAHIMU, NA WA ISAKA, NA WA ISRAELI, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, …. (1 Wafalme 18:36)

      Ee Bwana, MUNGU WA IBRAHIMU, NA WA ISAKA, NA WA ISRAELI, …(1 Nya 29:18)

      Enyi wana wa Israeli, mrudieni Bwana, MUNGU WA IBRAHIMU, NA ISAKA, NA ISRAELI, …(1 Nya 30:6)

      Mimi ni MUNGU WA IBRAHIMU, NA MUNGU WA ISAKA, NA MUNGU WA YAKOBO? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. (Mt. 22:32)

      …Mimi ni MUNGU WA IBRAHIMU, NA MUNGU WA ISAKA, NA MUNGU WA YAKOBO? (Mk. 12:26)

      … hapo alipomtaja Bwana kuwa ni MUNGU WA IBRAHIMU, NA MUNGU WA ISAKA, NA MUNGU WA YAKOBO. (Lk. 20:37)
      MUNGU WA IBRAHIMU NA WA ISAKA NA WA YAKOBO, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, … (Matendo 3:13)

      Vilevile Ibra, Mungu anaitwa ni MUNGU WA ISRAELI. Israeli ni jina jingine la Yakobo. Na Yakobo ni mwana wa Isaka, mwana wa Ibrahimu. Unaweza kuona mifano michache tu kwenye aya zifuatazo: (1 Wafalme 22:53, 2 Wafalme 9:6, 18:6, 19:15, 21:12, 1 Nya. 5:26, 15:14, 2 Nya. 2:12, Lk 1:68).
      Kwa hiyo rafiki yangu Ibra, bado ukweli uko palepale kwamba wokovu wa mwanadamu unapita kwenye mstari wa Ibrahimu – Isaka – Yakobo – Yesu. Basi!

      Delete
    2. nahitaji kuuliza kitu nje ya mada
      Mwanzo 29:20-30 inaelezea habari za Nuhu pamoja na kukaa uchi na kulewa
      suala langu 'Kaanani alilaaniwa na Nuhu na baadae Nuhu na Mungu wakashirikiana na kusema Kanaani awe mtumwa kwa ndugu zake, Jee Kaanani kafanya kosa gani?

      Delete
  2. Umeeleweka Jems John. Mungu akutie nguvu ili uendelee kutuelimisha

    ReplyDelete
  3. Ubarikiwe sana James
    Neno la MUNGU kulielewa ni lazima uongozwe na roho Mtakatifu. Nawashauri wote wanaosoma neno la Mungu yaani Biblia waombe kwanza Roho Mtakatifu awaongoze kulielewa, tofauti na hapo wataishia kulipinga tu na si kulielewa.

    ReplyDelete
  4. James ubarikiwe mtumishi kazi yako njema

    ReplyDelete